21.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

‘Scorpion’ afunguliwa shtaka jipya

Mtuhumiwa wa kesi ya kujeruhi, Salum Henjewele ‘Scorpion’, akisindikizwa na polisi kuingia katika chumba cha Mahakama ya Ilala, Dar es Salaam jana.
Mtuhumiwa wa kesi ya kujeruhi, Salum Henjewele ‘Scorpion’, akisindikizwa na polisi kuingia katika chumba cha Mahakama ya Ilala, Dar es Salaam jana.

Na FARAJA MASINDE, DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, imemsomea shtaka jipya Salum Henjewele (34) maarufu ‘Scorpion’  mkazi wa Yombo Machimbo kwa kumtoboa macho, Saidi Mrisho.

Mbali ya shtaka hilo, Scorpion pia anakibiliwa na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, ambalo lilikuwapo katika hati ya mashtaka ya awali yaliyofunguliwa Septemba 28, mwaka huu.

Awali mahakama hiyo ilimfutia mashtaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha yanayomkabili ‘Scorpion’ baada ya upande wa mashtaka kuomba shtaka hilo liondolewe mahakamani kwa sababu hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Kutokana na maombi hayo, Hakimu Adelf Sachore alikubaliana na ombi hilo kwa kuzingatia kifungu namba 91 kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ambacho kinampa mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuondoa shtaka mahakamani muda wowote ili mradi kama kesi hiyo haijatolewa hukumu.

Lakini kifungu hicho kinampa mamlaka DPP kumshtaki upya mshtakiwa huyo kama ana nia ya kuendesha shtaka hilo.

Akisoma shtaka hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule, Wakili wa Serikali, Chensensi Gavyole, alidai mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 6, mwaka huu saa 4 usiku maeneo ya Buguruni Sheli, Dar es Salaam.

“Mtuhumiwa unakabiliwa na shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha, uliiba cheni ya silva yenye uzito wa gramu 38, ikiwa na thamani ya Sh 85,000 na black bendi ya mkononi, fedha taslimu Sh 330,000 na waleti vyote vikiwa na thamani ya Sh 476,000 mali ya mlalamikaji, Said Mrisho.

“Mtuhumiwa pia inadaiwa kabla na baada ya kutekeleza tukio hilo ulimchoma kisu Mrisho ambaye ni mlalamikaji sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwamo machoni, tumboni na mabegani ili kurahisisha kupata mali hizo,” alidai Chensensi.

Hata hivyo, ‘Scorpion’ alikana kutenda kosa hilo na kurudishwa rumande kutokana na shauri hilo namba 305 la mwaka 2016 kutokuwa na dhamana.

Upelelezi wa shauri hilo, bado haujakamilika ambapo litarudi tena Novemba 2, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Shtaka hilo lilikuwa ni jipya, baada ya kuondolewa kwa lile la kwanza lililofunguliwa Septemba 28, mwaka huu.

‘Scorpion’ ambaye alifikishwa mahakamani hapo saa 2:18 asubuhi akitokea Gereza la Segerea, alipandishwa kizimbani saa 3:30 mbele ya Hakimu Mkazi, Adelf Sachore kwa kuongozwa na  Wakili wa Serikali, Munde Kalombola kwa ajili ya kutajwa kwa shauri lake la unyang’anyi wa kutumia silaha dhidi ya Said Mrisho.

Hata hivyo, mahakama hiyo ililazimika kuliondoa shtaka hilo ambalo lilifunguliwa Septemba 28, mwaka huu kutokana na maombi yaliyowasilishwa na Mwendesha Mashtaka, ambaye aliiomba mahakama kuliondoa baada ya upande wa mashtaka kutokuwa na nia ya kuendelea nalo.

“Kutokana na maombi yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka, mahakama imeliondoa shtaka hili kama ilivyoombwa kupitia kifungu cha 91(1),” alisema Hakimu Sachore.

Kesi hiyo inayomkabili ‘Scorpion’ ambaye jana alivalia kanzu ndefu nyeupe, viatu vyeusi na kibaraghashia anayetajwa kuwa mwalimu wa mashwati (karate), ilivuta hisia za watu wengi mahakamani hapo.

Kila mmoja alikuwa akitaka kumshuhudia mtuhumiwa huyo kutokana na kitendo chake anachodaiwa kufanya cha kumtoboa macho, Mrisho na kumsababishia upofu wa kudumu.

Licha ya manyunyu ya mvua yaliyokuwa yakiendelea mahakamani hapo nyakati za asubuhi, bado umati wa watu uliendelea kufurika nje ya chumba cha mahakama ambako kesi hiyo ilikuwa ikiendelea kusilizwa.

‘Scorpion’ ni msanii wa maigizo ya filamu na tamthiliya, pia alishiriki shindano la ‘Dume Challenge 2012’ na kuibuka mshindi ambapo alijipatia Sh milioni 20 pamoja na mkataba wa kuwa balozi wa mipira ya kiume maarufu ‘dume’.

Pia aliwahi kushiriki kucheza tamthiliya tatu, ikiwamo Red apple, Mirrosos na Thilipina ambayo inaendelea kukamilishwa ambazo zinaandaliwa na msanii Tuesday Kihangala maarufu kama Mr Chusi.

Baadhi ya wasanii aliowahi kushiriki nao katika tamthiliya hizo ni pamoja na Mohamed Olotu maarufu kwa jina la Mzee Chilo.

Mzee Chillo ambaye ameshiriki na Scorpion katika tamthiliya ya Thilipina miezi mitatu iliyopita, alisema walikutana katika kazi na hajui undani wa mtuhumiwa huyo.

“Mimi huyo kijana kwanza hata jina nilikuwa simjui, nyie mnaonipigia na kuniuliza ndio mnaofanya nimfahamu.

“Kifupi mimi nilikutana naye miezi mitatu iliyopita ndani ya mwaka huu kwenye tamthiliya, lakini nilikuwa simfahamu, hivyo kama utahitaji taarifa zaidi unaweza kuzipata kwa Mr Kihangala, maana hata tamthiliya yenyewe bado haijatoka,” alisema Mzee Chillo.

Kwa upande wake, Mr Chuzi alisema: “Ni kweli namtambua kijana huyu, namtambua kama kijana mpole sana na anayependa kumcha Mungu kwa kuswali sana pamoja na kufanya mazoezi ya ukakamavu.

“Ni kweli kwamba nimekuwa naye na alikuja kujiunga kwenye kampuni yangu ya Tuesday mwaka 2010 na kushiriki tamthiliya zangu mbili ambazo ni Mirrosos na Red Apple.

“Baadaye alitoka na kwenda kushiriki kwenye shindano la ‘Dume Challenge’ na akafanikiwa kushinda na kupata mkataba mpaka pale ulipoisha na kurejea tena,” alisema.

Miezi mitatu iliyopita mwaka huu aliomba kushiriki tamthiliya ya Thilipina ambayo bado inaendelea,” alisema Kihangala.

Alisema kabla ya kwenda kushiriki ‘Dume Challenge mwaka 2012, alikuwa na mkataba tofauti na sasa ambapo hana  mkataba bali anakuja kucheza  vipande vyake na kuondoka.

“Mara nyingi amekuwa ni mtu anayependa sana kufanya mazoezi na ni mwalimu wa karate na amekuwa akiwasisitiza watu kufanya mazoezi na hata kuwa kiongozi tunapokuwa ‘location’,” alisema.

Kihangala aliongeza kuwa katika kufanya kazi pamoja na Scorpion, hakuwahi kufahamu makazi yake zaidi ya kukutana ofisini pamoja na mahali wanaporekodi kazi zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,656FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles