31.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 29, 2023

Contact us: [email protected]

Gambo, Lema wamuibua Dk. Slaa

Dk. Willibrod Slaa
Dk. Willibrod Slaa

NA WAANDISHI WETU,

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amemshambulia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo huku akimtaka aache siasa za majitaka.

Dk. Slaa alitoa kauli hiyo kupitia taarifa aliyoiweka kwenye mitandao ya kijamii, huku akisema cheo alichonacho Gambo ni kikubwa, lakini alichokifanya na propaganda anazopiga, amemdharau na kumpuuza.

Hatua  ya Dk. Slaa imekuja siku moja baada ya Gambo na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kuvutana hadharani kuhusu uzinduzi wa mradi wa maendeleo wa Sh bilioni 9 wa ujenzi wa hospitali ya itakayohudumia bure mama na mtoto, huku sehemu kubwa ya gharama zake ikiahidiwa na wafadhili kutoka Marekani.

Kutokana na taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, MTANZANIA lilimtafuta Dk. Slaa kupitia simu yake ya kiganjani akiwa nchini Canada, ambapo alisisitiza taarifa hiyo ni ya kwake na kwamba ametumia haki yake ya kukemea bila kuangalia uso wa mtu kwa masilahi ya Taifa.

Pamoja na mambo mengine, Dk. Slaa aliyejiengua katika uongozi wa Chadema Septemba mosi, mwaka jana, alisema aibu ambayo ameiletea Taifa mkuu huyo wa mkoa wa Arusha imemlazimu kupiga kelele huku akisema analijua vizuri chimbuko la ardhi hiyo.

Alisema anafahamu vizuri historia ya mradi huo tangu mwanzo, na kwamba propaganda zinazoenezwa kwamba hopitali hiyo ni ya mke wa Lema, zipuuzwe.

“Mkuu wa Mkoa nakuheshimu kwa kuwa cheo chako ni kikubwa sana. Hata hivyo, ulichokifanya leo (juzi) na propaganda unazopiga zimenifanya nikudharau na kukupuuza.

“Ningeliweza kuishia katika kukudharau na kukupuuza, lakini aibu uliyoiletea Taifa letu leo, inanifanya nipige kelele kuwa  siasa za majitaka si wakati wake huu.

“Wewe kama Mkuu wa Mkoa unayo au mamlaka au vyombo vya dola kukusaidia kufanya utafiti wa maana kuliko aibu kubwa uliyoiletea Taifa letu mbele ya wahisani/wafadhili wetu kupitia Maternity Africa.

“Hukufanya hivyo, umeamini propaganda kuliko busara na hekima. Kwa hilo siwezi kukusamehe wala kukuheshimu pamoja na cheo au vyeo vyote ulivyonavyo.

“Mrisho Gambo, ungelikuwa wa busara iwapo ungelimwomba kiongozi au mwakilishi wa ADF (ulikuwa na uwezo wa kujua ADF ni nani na historia yake ni ipi – kwa kupenda propaganda hukufanya hivyo) au mwakilishi wa Maternity Africa hasa Happy (ambaye alisaini pia barua ya kukualika kuwa mgeni rasmi), au hata Lema ambaye kimsingi ndiye chimbuko la upatikanaji wa ardhi hiyo kutoka kwa marehemu Advocate Mawala (Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi) na pia chimbuko la upatikanaji mradi kutoka kwa wafadhili wetu.

“Kutokupenda kushauriwa na hao wenye kujua mradi imekufanya “kuonekana juha” na “mwongo” kwa kuwa historia haifutwi kwa “propaganda za jukwaani”. Lakini kwa bahati mbaya athari ya propaganda imeenda mpaka kuchafua Taifa letu kwa wahisani.

“Mrisho Gumbo, busara na hekima ya kawaida ingelikuwezesha kuelewa barua ya mwaliko ambayo imesisitiza mara mbili hivi kuwa wahusika ni taasisi isiyojihusisha na siasa.

“Eti unasoma historia! Unajua historia au unaota ndoto! Nimepiga kelele kwa kuwa ninaijua vizuri hiyo historia A to Z. Sikuambii ungeliniuliza, lakini wapo kwenye kikao hicho ambao wasingelihitaji kuisoma bali kuitoa kichwani historia hiyo, tangu kupatikana kwa ardhi, mchakato wa kuchora ramani, kuisajili na kupata vibali vyote vya kituo hicho cha afya (japo kwa kweli ni hospitali inaitwa kituo cha afya tu kwa sababu za kisheria),” alisema Dk. Slaa.

Alisema kwa alichokifanya Gambo, Watanzania wa Mkoa wa Arusha wenye kujua ukweli hawatamsamehe kwa aibu aliyoifanya.

Katika hilo, alimtaka kama atakuwa na chembe ya busara kukaa chini na kutafakari amekosea wapi  huku akiwaita wahusika ili wampe historia kamili ya mradi huo.

“Kwa unyenyekevu mkubwa waombe msamaha wahisani wetu kwa kuwaingiza katika “siasa ya Arusha” ambayo hawahusiki nayo; awaombe uongozi ni busara na hekima siyo mabavu wala nguvu ya mamlaka.

Nimeyasema haya kwa uchungu mkubwa. Mimi siko kwenye siasa, na wala sina interest na siasa. Siangalii uso wa mtu. Kama ambavyo niliaga kuwa nastaafu Party Politics, lakini nitapiga kelele pale masilahi ya Taifa langu yanavyokanyagwa,” alisema.

ZITTO

Kwa upande wake, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema anakasirishwa  kuona viongozi vijana wanafanya mambo ya ovyo.

“Mkuu wa Mkoa wa Arusha, mdogo wangu Mrisho Gambo, una dhamana zaidi kwa vijana. Mnapofanya mambo ya kijinga mnaharibu nafasi ya vijana kuaminiwa zaidi. Kaa na Lema mnywe kahawa pale New Arusha ma muanze upya.

“Ndugu yangu Lema, nashauri punguza munkari. Juhudi zako Arusha haziwezi kufutika kirahisi. Nakushauri kaa chini na Mkuu wa Mkoa wako mpige mstari muanze kazi upya kwa pamoja.

Viongozi jiepusheni kuonyesha hasira zenu hadharani. Sio hekima,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini.

 DK. MASHINJI

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, alieleza kusikitishwa na kitendo wa Gambo kuvuruga sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya kituo cha huduma za mama na mtoto.

“Nalaani tabia hizi za kihuni zisizo na tija kwa Taifa. Ikumbukwe tu kwamba mwanzo wa ngoma ni lele. Tabia ya mkuu huyu wa mkoa inajenga chuki na yaweza kuleta machafuko yasiyo ya lazima. Mtu wa hivi hafai kabisa katika jamii,” alisema.

GAMBO AIBUKA

Katika hatua nyingine, Gambo aliwataka wananchi  kupuuza taarifa za uzushi zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikidai Rais Dk. John Magufuli amelazimika kutengua uteuzi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles