24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ummy asema idadi ya watoto wanaozaliwa nchini inapungua

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema kwa hivi sasa takwimu zinaonesha wastani wa mwanamke mmoja kuzaa umepungua kutoka watoto saba hadi watano.

Kutokana na hali hiyo, alisema ongezeko la watoto wanaoandikishwa shule, linatokana na mpango wa elimu bure na si kwamba watoto wengi wanazaliwa nchini.

Ummy alitoa kauli hiyo jana katika hafla ya kutiliana saini kati ya Mbunge Mariamu Ditopile (CCM Viti Maalumu) na wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mkoani hapa ambao atawasomesha 100.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ummy alisema watoto 500,000 walikuwa wanabaki majumbani baada ya wazazi wao kushindwa kuwahudumia, lakini kutokana na mpango wa elimu bure, sasa wanaenda shule.

“Sasa ongezeko hili mtu anaweza kusema ni kwamba watoto wengi wanazaliwa, hapana, takwimu zetu zinaonesha kiwango cha mwanamke mmoja kujifungua kinazidi kupungua kutoka watoto saba hadi watano, kwa hiyo watoto wanazidi kupungua,” alisema.

Alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika elimu kwa kuwa ni moja ya uwekezaji muhimu.

“Takwimu zinaonesha zipo sababu kubwa za kuwafadhili watoto wa kike, kwa mfano mwaka 2017 watoto wa kike ambao walimaliza kidato cha nne walikuwa 1,025,700 wakati wa kiume ni 965,305, sasa wangapi wanaoenda kidato cha tano na sita?

“Kati ya wanafunzi 100 wanaotakiwa kwenda kidato cha tano na sita, 51 ni wasichana. Lakini takwimu zinaonesha hao wasichana 51 si wote wanaokwenda kidato cha tano kutokana na kushindwa kuendelea na elimu,” alisema Ummy.

Alihimiza kuwepo na msukumo wa elimu kwa watoto wa kike na ufadhili uliofanyika utasaidia kujiepusha na mimba za utotoni ambapo hivi sasa mabinti  27 kati ya 100 wanapata mimba hizo.

Awali, Dittopile alisema ametimiza ahadi yake aliyoiweka ya kusomesha watoto wa kike waliofaulu kuingia kidato cha tano katika shule za Serikali na tayari ameshatoa Sh milioni 20 kusomesha watoto 100.

“Kuna watu wanajiuliza kwanini watoto wa kike mara nyingi wamekuwa wakisahaulika, tukitoa misaada kwa vijana wa bodaboda unakuta ni watoto wa kiume tupu, tukisaidia michezo unakuta vijana wa kiume, hata kwenye halmashauri zikitoka nafasi za kuhusisha vikundi vya kijamii unakuta kundi lina vijana wa kiume tupu, hapa kama viongozi inabidi tuliangalie hili na tubadilike,” alisema Ditopile.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles