22.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Ukimjali msichana wa kazi atawajali watoto wako

CHRISTIAN BWAYA

TULISHAWAHI kujadali nafasi ya dada wa kazi katika malezi. Tuliona kuwa pamoja na unafuu wa huduma zao, wamekuwa wakikabiliana na uhusiano hafifu na waajiri wao. 


Kwa kuwa huduma za malezi kupitia wadada hawa zinaweza zisikwepeke, ni muhimu kujadili namna gani tunaweza kupunguza uwezekano wa kumfanya msichana wa kazi akose ari na hamasa ya kufanya kazi yake kwa bidii.

Makala haya yanajadili mapendekezo ya namna ya kuboresha uhusiano na wadada wanaosaidia kazi na kulea watoto majumbani.

Fahamu historia yake

Ipo haja ya kujitahidi kufahamu msichana ametoka familia gani, aliishi vipi na familia yake, misimamo yake, imani, angalau mambo ya msingi. Ili hayo yawezekane, ni vizuri kumpata kupitia watu wanaomfahamu vizuri.

Unapokuwa na fursa ya kumfahamu binti unayeishi naye vizuri, unaweza kufanya uamuzi sahihi mapema ikiwa unaweza kukaa naye ama la.

Mwelimishe majukumu

Mitafuruku mingi kati ya waajiri na hawa mabinti wakati mwingine inachangiwa na kutokufahamika kwa majukumu yake ipasavyo. Waajiri wengi huwa na matarajio makubwa kwa akina dada na hivyo hawawasaidii kujua wanachopaswa kukifanya.

Ni vyema mara baada ya kukubaliana naye kuwa anaishi na familia yako kwa lengo la kumwangalia mtoto, uhakikishe anajua utaratibu kamili wa kazi. Ukifanya hivyo unapunguza uwezekano wa makosa yanayotokana na kutokujua jambo sahihi la kufanya.

Kujenga uhusiano mzuri

Mfanye binti wa kazi awe sehemu ya familia yako. Mfanye ajisikie kupendwa kama mwanafamilia mwingine. Unapofanya hivyo, unamfanya achangamke moyo na hivyo kuwa na hamasa ya kujituma.

Kwa mfano, unaweza kumtambulisha kwa wageni kama sehemu ya familia yako na unaweza kufikiria kumweka kwenye picha rasmi za familia unazoning’iniza ukutani.

Sambamba na hilo, epuka uhusiano usio wa kimaadili na wasichana hawa. Unapofanya hivyo, unajenga mazingira ya kudharaulika. Ukidharaulika, ni rahisi mwanao kuwa mhanga.

Mpe huduma anazostahili

Hakuna mfanyakazi ambaye hatamani kupata marupurupu. Hata wewe unahitaji mkubwa wako wa kazi akuangalie kimaslahi, na atambue kazi nzuri unayomfanyia.

Vivyo hivyo, nawe fikiria kumpa msichana wako wa kazi huduma zinazomvutia. Mtengenezee mazingira bora ya kazi.

Kwa mfano, unaweza kufikiria kumtengenezea utaratibu wa kujiendeleza kitaaluma. Pia unaweza kuhakikisha unatambua kazi anazozifanya kila siku jioni unaporudi nyumbani. Kwa kufanya hivyo unamjengea ari ya kazi.

Onesha mfano mzuri

Huwezi kutarajia binti wa kazi aishi vizuri na watoto, wakati wewe mwenyewe huoneshi kuwajali. Onesha kwa vitendo namna unavyotarajia mtoto ahudumiwe. Binti atajifunza kwa vitendo.

Kadhalika, kuwa mfano kwa kufanya kazi za ndani kama unavyotarajia afanye yeye. Pika, tenga chakula mezani, fua nguo inapobidi ili kuonesha kuwa unaishi matarajio yako. Unapofanya hivyo, binti atakuheshimu.

Tumia muda wa kutosha na mtoto

Mtu anayetumia muda mrefu na mwanao ndiye mwenye nafasi zaidi ya kuwekeza. Kwa sababu binti ndiye anayekaa na mwanao kwa muda mrefu, upo uwezekano wa mwanao kufundishwa mambo usiyoyatarajia.

Ni vizuri kuhakikisha unafuatilia maendeleo ya kitabia ya mwanao mara unaporudi nyumbani. Jitahidi kuzungumza na mwanao kubaini ikiwa yapo yasiyofaa aliyojifunza. Unapoyabaini, weka mbadala wake mapema.

Pamoja na kuchukua hatua hizi, hatusemi kuwa mambo yatakuwa sawia. Zinaweza kuwapo changamoto, lakini si kama ambavyo hautajenga utamaduni wa kuwafatilia watoto.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754 870 815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,415FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles