23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Huwezi kufurahia uhusiano ikiwa unatoa zaidi ya unachokipata

Christian Bwaya

NILIMSIKILIZA mzungumzaji mmoja, kiongozi wa dini, akieleza kuwa matatizo mengi ya ndoa tunayoyaona yanatokana na tabia ya wanawake kukosa utii kwa waume wao.

Utii wa wanawake, kwa mujibu wa kiongozi huyo, ni ule usikivu anaouonesha kwa amri anazopewa na mume wake, kufanyia kazi maelekezo anayopewa na kutambua nafasi ya mume wake katika ndoa.

Akitoa mifano mingi kutoka kwenye Biblia, mtumishi huyo wa Mungu aliwaonya wanawake kuwa wao ndio hasa wamekuwa tatizo kwenye ndoa.  Tabia yao ya kupimana ubavu na waume zao ndio inayowakera wanaume ambao kwa mujibu wa maandiko, ndio vichwa vya familia. 

Ndio kusema, kwa mujibu wa kiongozi huyo, suluhisho kubwa la misuguano ya ndoa ni wanawake kubadilika na kuwa watii kwa waume zao.

Sikusudii kupinga hoja ya mtumishi wa Mungu. Nafahamu kwamba kimaumbile ni kweli mwanamume anatafsiri upendo kama heshima anayopewa na mwanamke.

Huwezi kumpenda mwanamume kwa maneno. Huwezi kugusa moyo wake kwa kumwambia kuwa unampenda. Mwanamume anachukulia heshima anayopewa na mwanamke kuwa ndio upendo.

Lakini pia, nafahamu kuwa uhusiano kati ya mwanamume na mwanamke umejengwa katika misingi ya usawa. Hakuna anayestahili kupokea zaidi ya kile anachotoa. Unapata sawa na kile ulichokitoa. Kisaikolojia ni kwamba, huwezi kufurahia uhusiano wa karibu na mtu ikiwa unatoa kuliko kile unachokipata.

Na ilivyo ni kwamba kadri unavyopokea ndivyo unavyosukumwa kutoa zaidi. Na kadri unavyotoa ndivyo unavyomhamasisha yule uliyempa kukupa zaidi. Hii ni kanuni ya kimaumbile.

Kanuni hii ya kimaumbile inapochezewa kwa sababu zozote zile, uhusiano wa watu wawili huanza kuzorota. Fikiria rafiki unayemsaidia mara kwa mara lakini yeye haonekani kuguswa pale wewe unapojikuta kwenye matatizo. Urafiki wa namna hii hauwezi kwenda mbali kwa sababu mosi, anayetoa mara kwa mara huanza kujiona anatumika.

Lakini pili, anayepokea huanza kujihesabia haki kwa  yale anayoyapokea. Mawili haya hayawezi kuwa afya ya uhusiano wa wawili hawa.

Hapa ndiko ninapodhani maoni ya mtumishi yule wa Mungu yanahitaji kuchukuliwa kwa tahadhari. Ingawa ninatambua kuwa mwanamume anastahili kupata utii wa mke wake, sifikiri kama ni sahihi kumbebesha mwanamke mzigo wote wa wajibu katika ndoa. Hapa nina maana kuwa si afya kumdai mwanamke amtii mume wake bila kutazama wajibu wa mume kwa mwanamke huyu.

Nikitumia maelezo niliyoyatanguliza hapo juu, mwanaume ana kazi ya kumpenda mke wake. Biblia imelisisitiza hilo. Enyi wanaume wapendeni wake zenu. Huo ndio wajibu mkubwa wa mume kwa mke wake, yaani kumpenda kwa maneno na vitendo.

Wajibu wa mume kwa mke wake ni kumhakikishia kuwa yeye ndiye mtu muhimu katika maisha yake.

Ikiwa angetakiwa kuchagua kati ya mke wake na watu wengine wote duniani, mume anayempenda mke wake, hatapata shida kufanya uamuzi kwa sababu kwa vyovyote vile atamchagua mke wake.

Mume anayempenda mke wake, atamhakikishia usalama. Hataruhusu mazingira ya mke wake kuwa na wasiwasi na uaminifu wake kwake. Upendo wake unajionesha kwa vile anavyohakikisha kuwa mke wake anakuwa salama dhidi ya maadui wote wakiwamo familia yake mwenyewe.

Ndio maana, Biblia hiyo hiyo imewaasa wanandoa ‘kuachana’ na familia zao na kuambatana na kuwa mwili mmoja. Kuachana na familia inaweza kutafsiriwa kama kipimo cha uaminifu (loyalty) kwa mke kwa sababu, kama nilivyotangulia kusema, mume anayempenda mke wake ni mlinzi wake nambari moja.

Ikiwa mume atafanya wajibu huo, sioni itawezekanaje mwanamke huyu ashindwe kuwa na utii kwake. Mume anayemfanya mke ajisikie mtu wa kwanza muhimu kwenye maisha yake, hawezi kudai utii kutoka kwa mke wake. Mume anayemfanya mke wake ajisikie salama dhidi ya kila maadui wanamshambulia, hawezi humwomba mke wake amtii.

Ninachojaribu kukibainisha hapa ni kwamba utii wa mke kwa mume wake ni matokeo ya uwekezaji wa mume kwenye uhusiano. Mume anayewekeza upendo, anapokea utii.

Ikiwa tunakubaliana hapo, maana yake ni kwamba  inapotokea mke hana utii kwa mume wake, ni muhimu mume ajiulize ikiwa kweli amefanya wajibu wake ipasavyo kwa mke wake. Je, amempenda mke wake kwa dhati? Je, amelinda hisia za mke wake dhidi ya uwepo wa wanawake wengine wanaowinda moyo wake? Je, amemfanya mke wake ajikie kulindwa vya kutosha?  

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles