24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

UKAWA YAVUNA ILICHOPANDA

Na ELIZABETH HOMBO


 

0D6A8268JUMAPILI iliyopita ulifanyika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 20 za Tanzania Bara pamoja na kiti cha ubunge wa Jimbo la Dimani visiwani Zanzibar.

Katika uchaguzi wa kata hizo, CCM ilishinda 19 huku mgombea wake Juma Ali Juma akinyakua Jimbo la Dimani kwa kura 4,860 dhidi ya Abdulrazak Khatib Ramadhan wa CUF aliyepata kura 1,234.

Wakati CCM ikinyakua kata hizo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilifanikiwa kutetea kata yake ya Duru iliyopo Babati mkoani Manyara huku CUF ikipoteza kata yake ya Kimwani- Muleba mkoani Kagera.

Baadhi ya wachambuzi wa Sayansi ya Siasa wanayatazama matokeo ya uchaguzi huo wa kwanza tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka juzi kama kipimo kipya cha hali ya siasa hapa nchini.

Awali waliutazama uchaguzi huo kwamba ungetoa mwelekeo wa kura za hasira kutokana na mwenendo wa utawala wa Rais Dk. John Magufuli ambao wapinzani na baadhi ya watu wengine wamekuwa wakiulalamikia.

Kwamba kitendo cha Rais Magufuli kupiga marufuku kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, mwenendo wa demokrasia na ugumu wa maisha ungewafanya wananchi kupiga kura za hasira.

Wapo pia wanaouchukulia matokeo ya uchaguzi huo kuwa hauwezi kuwa kipimo cha siasa za nchi kwa maana kwamba idadi ya kata 20 na jimbo moja haviwezi kutumika kama sampuli ya kupima hali ya siasa katika kata na majimbo yote ya uchaguzi hapa nchini.

Kabla ya uchaguzi huo kufanyika, CCM ilikuwa na presha kwamba wangepoteza walau kiti kimoja au viwili ingemaanisha kwamba wameshindwa. Hilo liliwafanya watumie nguvu nyingi kuhakikisha hawapati aibu hiyo.

Lakini kwa upande wa upinzani hawakuwa na presha kiasi hicho kwa sababu walikuwa hawana cha kupoteza kwa vile viti hivyo vilikuwa vikiongozwa na CCM isipokuwa kata moja ya Duru iliyorudi Chadema.

Kudorora kwa Ukawa

Hoja nyingine inayotajwa kuipa ushindi CCM ni pamoja na kudorora kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita Ukawa unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD ulileta hamasa kubwa katika uchaguzi mkuu uliopita.

Lakini kutokana na mgogoro unaofukuta ndani ya CUF, umoja huo umeonekana kutokuwa na mvuto kama ilivyokuwa mwanzo.

Mvuto huo ulipotea pale aliyekuwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu nafasi yake Agosti mwaka juzi wakati ambao chama chake kilikuwa kikimuhitaji kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Pamoja na kujiuzulu kwa msomi huyo wa uchumi nchini, hilo halikusababisha Ukawa kudorora kwani vyama hivyo vilifanya vizuri katika uchaguzi huo.

Lakini kilichosababisha kupungua kwa mvuto wa Ukawa ni pale ambapo Profesa Lipumba alipotengua barua yake ya kujiuzulu Agosti mwaka jana kabla hata ya kujibiwa na chama chake.

Kitendo cha Profesa Lipumba kutengua barua hiyo ndicho ambacho kimesababisha mgogoro uliozaa makundi mawili moja likimuunga yeye na lingine likimuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharrif Hamad.

Kwa asilimia kubwa mgogoro huo ndio ambao sasa umeikosesha ushindi Ukawa kwa sababu CUF ya Profesa Lipumba nayo ilisimamisha wagombea katika kata zote.

Mbali na CUF, jambo lingine ambalo limeshangaza wengi ni kutokana na NCCR-Mageuzi na Chadema kusimamisha wagombea katika baadhi ya kata.

Pengine hilo lilitokea kwa sababu baada ya mgogoro huo wa CUF, kila chama imebidi kijipiganie chenyewe.

Pia sababu nyingine ambayo imesababisha upinzani kushindwa ni kutokana na uwanja wa mapambano kutokuwa huru.

Nikiwa na maana kwamba wahusika ambao wanasimamia na kutangaza matokeo wameteuliwa na Rais hivyo kwa vyovyote iwavyo uchaguzi haungekuwa huru na haki.

Siku chache baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage alisema NEC inatakiwa kuwa na watumishi wake na si wakurugenzi wanaoteuliwa na Rais.

Endapo kauli hiyo ya Jaji Kaijage itakuwa ni ya kweli na ikifanyiwa kazi, ni wazi malalamiko haya kwamba chama tawala kinabebwa na NEC yatakwisha.

Prof. Kitila

Akitoa tathimini yake kuhusu uchaguzi huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo anasema alishangazwa katika uchaguzi huo kuona kwenye kata moja Chadema na NCCR-Mageuzi wamesimamisha wagombea.

“Nilielewa kwa CUF kwa kuwa zipo mbili. Sasa kama Ukawa ni CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD. Kisiasa NLD haipo, ipo kisheria tu. CUF ndio hiyo.  Kwa hiyo kisiasa Ukawa ya sasa ni Chadema na NCCR-Mageuzi.

“Ukitaka kuwa ‘serious’ zaidi utaona kwamba NCCR-Mageuzi inakoelekea ni kubaki kuwa chama kilichosajiliwa tu kisichokuwapo katika ulingo wa kisiasa.

“Ni kwa sababu hii David Kafulila alihamia Chadema. Vinginevyo Kafulila alikuwa hana haja ya kuhama. Kwa hiyo, kiufundi na kisiasa, Ukawa ya sasa ni Chadema. Na zaidi Ukawa ya sasa ni jina! Hapa ndipo pa kuanzia.

“Tunahitaji kujiunda upya kama tunataka ushirika. Hatua ya kwanza kabisa katika kushirikiana ni kuheshimiana. Kubezana hakuwezi kuzaa ushirikiano na hii imetugharimu miongo yote tangu mfumo wa vyama vingi uanze.

“Kila mara chama chenye nguvu zaidi huvidharau vyama vingine na kuvipa majina mabaya. Tujisahihishe,”anasema Prof. Kitila ambaye pia mshauri wa chama cha  ACT-Wazalendo.

Mtatiro

Kwa upande wake mchambuzi wa masuala ya siasa, Julius Mtatiro anasema kwa vyovyote vile vyama mbadala haviwezi kujivunia matokeo hayo kwani havikuweza kuishinda CCM na kwamba CCM haina cha kutambia.

“Hali halisi inaonyesha kuwa kama vyama mbadala vingeshirikiana vingelishinda kata si zaidi ya saba, bahati mbaya mashirikiano haya yalikosekana tangu mwanzo baada ya mgogoro wa CUF.

“Baada ya CUF ya Lipumba kujipanga kuvuruga uchaguzi huu na kushusha spirit ya Ukawa, vyama vya NCCR na Chadema pia vilionelea kila kimoja kijipiganie jambo ambalo ni kosa kubwa na madhara ya mgawanyiko yote yalijulikana,”anasema Mtatiro.

Anasema uzoefu unaonyesha kuwa kuishinda CCM kwenye chaguzi ndogo ni nadra mno kwa sababu mkakati wa chama hicho tawala ni kuvitumia baadhi ya vyama au baadhi ya viongozi kwenye vyama (mamluki) ambapo unaelekea kufanikiwa.

Mtatiro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF, anasema huenda ACT-Wazalendo ndicho chama kilichofanikiwa kwenye uchaguzi huu kuliko vyama vyote pamoja na uchanga wake kimevishinda baadhi ya vyama vikongwe kwenye kata chache.

“Matokeo haya hayana athari zozote za kufaulu kwa Rais Magufuli katika sera zake, yaani CCM ya Magufuli haijawa na ushawishi wa ziada kwa wapiga kura ili kupata ushindi huu kwenye ngome zake.

“ Sijaona uhusiano wowote kati ya matokeo haya na siasa za 2020. Vyama vyote vinayo fursa ya kuendelea kujipanga na kama tutafanikiwa kuuvunja mfumo dola unaoathiri vyombo vya uchaguzi na uhuru wake, unaondoa mazingira sawa kwa vyama kufanya siasa.

“Mabadiliko ya kikatiba kwenye NEC na sheria za uchaguzi na mengine mengi, siasa za 2020 zitakuwa mbichi sana,”anasema Mtatiro.

Lissu

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu anasema uchaguzi mdogo wa ubunge au udiwani huwa ni ngumu kushinda katika mazingira halisi ya nchi yetu.

“Hatujanyang’anywa iliyokuwa yetu, hatujanyakua zilizokuwa zao. Hata hivyo, funzo kubwa zaidi la historia ya chaguzi hizi ni hili hapa: licha ya kupigwa kwenye chaguzi ndogo hizi, tumeendelea kufanya vizuri zaidi katika kila Uchaguzi Mkuu uliofuatia kipigo cha uchaguzi mdogo.

“Hoja yangu hapa ni kwamba uchaguzi wa marudio hauna athari zozote kwenye matokeo yetu ya Uchaguzi Mkuu unaofuatia. Badala yake, uchaguzi wa marudio unatupa fursa ya kupanda mbegu ambayo, ikitunzwa vizuri inakuwa na mazao bora kwenye chaguzi zinazofuatia.

“Kwa upande mwingine, uchaguzi wa marudio kwa sababu ya udogo au uchache wa maeneo yanayogombaniwa, yanawapa CCM fursa ya kutumia nguvu kubwa za rasilimali na za kidola ukilinganisha na tunazotumia sisi wapinzani.

“Kwenye Uchaguzi Mkuu unaofuatia, nguvu hizo zinasambazwa nchi nzima na kwa hiyo ‘ufanisi wake unapungua.

“Ndio maana tumefanya vizuri zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu kuliko kwenye uchaguzi mdogo wa marudio. Hili, kwa maoni yangu ndilo fundisho kuu la chaguzi hizi za marudio. Hatuna sababu kubwa ya kushangilia kutokana na matokeo ya jana. Hata hivyo, hatuna sababu yoyote ya kuomboleza pia.

“Tutathmini kazi tuliyoifanya na matokeo tuliyoyapata. Tupate mafundisho sahihi ya kazi hiyo na matokeo yake. Tutumie mafundisho hayo kwa kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya ‘the real prize’: 2020,”anasema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.

Zitto

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe anasema pamoja na kwamba chama chake hakijashinda lakini matokeo yameonyesha kukua kwa kasi kubwa kwa chama chake.

Pamoja na mambo mengine kwa sasa uchaguzi umekwisha hivyo badala ya kutumia muda mwingi kujadili matokeo, anasema wakubali kuwa wameshindwa na kwamba kinachotakiwa ni kujipanga upya.

“Tuwaunge mkono walioshinda lakini pia tuwakosoe wanaposhindwa kuwajibika. Tusiache kuwasemea wananchi na kuhangaika na changamoto zao za maisha,”anasema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles