ASANTE RAIS WA UTURUKI KUTUTEMBELEA WATANZANIA

Rais Erdogan Wa Uturuki.KUNA  methali inayosema: ‘Mgeni njoo mwenyeji apone’ inayoakisi neema anayoleta mgeni akikutembelea si tu kwa zawadi atakazokuja nazo, lakini pia ukarimu wa kufunga safari ndefu kuja kubadilishana fikra na kufahamiana vyema.

Methali hiyo ina muktadha wa ujio wa ugeni wa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, aliyetutembelea hivi karibuni kwani tungetarajia angeelekea kwingine lakini aliamua kuanzia kwetu miongoni mwa nchi tatu za Afrika katika ziara yake ya siku tano, ikidhihirisha kuwa ametuthamini.

Naamini hata Msumbiji na Madagascar alikoelekea alipotoka kwetu wamefarijika kwa ziara yake, ingawa si mara ya kwanza kwake kuja Afrika kwani mwanzoni mwa mwaka jana alitembelea Senegal, Ivory Coast, Ghana, Nigeria, Guinea, Uganda, Kenya na Somalia, amebainisha kuwa haitakuwa mara ya mwisho kutembelea Afrika kwamba ni mwendelezo wa mfululizo wa safari nyingi zijazo barani hapa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kiuchumi na kidiplomasia baina ya taifa hilo na nchi zetu.

Amekuja kutafuta uwekezaji katika nyanja mbalimbali hivyo aliambatana na wajumbe wa bodi ya uhusiano wa kiuchumi wa kimataifa kutoka nchini mwake waliolenga kutathmini na kujadiliana fursa za uwekezaji katika nyanja za kilimo, utalii, huduma za kibenki na fedha, ujenzi, miundombinu, madini na nishati. Ni sekta nyeti na muhimu walizochagua kushirikiana nasi hususani kwa kulenga mazao ya kibiashara yakiwamo kahawa, pamba, chai, tumbaku, korosho, shayiri, sukari, mpunga na mtama kwa kuwa takwimu zinaonesha ukuaji wetu kiuchumi umefikia asilimia 6.9.

Licha ya yote hayo Rais Erdogan ana mvuto wa pekee kutokana na matukio ya kisiasa yanayojiri nchini mwake, nilitamani sana Rais huyo angepata mahojiano mahususi ya vyombo vya habari yenye maswali magumu kama katika kipindi cha ‘Hard Talk’ cha BBC kinachoendeshwa  na Stephen Sackur, ili atufahamishe mengi tunayoyashuhudia kwenye vyombo vya habari kuhusu hamkani za kisiasa nchini mwake.

Kwanza ningetamani angeulizwa kuhusu muswada tata uliowasilishwa  bungeni mwaka jana na chama chake cha AKP wa kuhalalisha ndoa za wabakaji na wabakwaji wenye umri chini ya miaka 18, kwa madai kuwa wanataka kuokoa watoto wanaozaliwa wasikose malezi lakini ilizua hamkani kubwa na maandamano ya kupingwa katika miji ya Instanbul, Izmir na Trabzon.

Lakini pia kungekuwa na swali la nyongeza kwamba kwanini  mihimili mbalimbali nchini mwake inafanya kazi kwa kukubaliana kinyemela, hivyo kulazimisha mambo yanayopingwa na wananchi? Mathalani, baada ya mahakama ya juu ya kikatiba kubadilisha kifungu kilichobainisha kuwa kujamiiana na mtoto chini ya miaka 15 ni unyanyasaji kijinsia ndipo chama chake kikaandaa muswada wa kuozesha wabakaji na wabakwaji?

Mwenyewe Rais Erdogan anafahamu kuwa Taifa lake lina takwimu mbaya kuhusiana na matendo ya unyanyaswaji kijinsia  kwa wanawake unaohusisha mauaji, lakini pia hulka ya mtazamo wake kwao kwani alikaririwa akisema kuwa mwanamke kwa asili ni mlegevu kulinganisha na mwanaume na kwamba mwanamke wa kweli ni anayejifungua kwa njia ya kawaida na sio upasuaji, kwamba wanawake wajawazito wanapwaya kiutendaji kazi ofisini na wanawake wanapaswa kudai kuheshimiwa na wanaume badala ya kudai usawa walionyimwa tangu dunia ilipoumbwa.

Ningependa pia mahojiano hayo yangegusia kuhusu mapigano na mashambulizi ya kigaidi yanayorindima mara kwa mara nchini mwake, kwa kuwa mojawapo ya kinachochochea msimamo wa kutotafuta suluhu na wapiganaji wa PKK (Partiya Karkeren Kurdistane) wenye asili ya Kikurdi ambao licha ya kuhasamiana naye lakini pia wanapigana kulizuia kundi la ISIL kujipenyeza zaidi ndani ya Uturuki. Kwamba haoni kuwa akisuluhishana na  Warkudi anaweza kuwageuza washirika muhimu katika kukabiliana na ugaidi kuliko kuwachukulia kuwa mahasimu? Pengine ingepunguza maguruneti yanayorindima kila mara hadi katika mji mkuu wa taifa lake!

Lakini pia swali muhimu ingekuwa kuhusu ‘sarakasi’ za jaribio la Mapinduzi takribani miezi saba iliyopita ambalo halieleweki hasa lilivyojiri, licha ya muda kupita lakini bado kuna askari kadhaa wako korokoroni wakishtakiwa kutokana na kadhia hiyo. Kioja hicho kinahusisha vifaru vilivyoingia mtaani na ndege vita kuvurumishia makombora  jengo la Bunge na Mkuu wa Vikosi vya Jeshi, Hulus Akar, kutekwa na walinzi wake pia jinsi wananchi wa kawaida wenye ujasiri walivyozuia vifaru vilivyoingia mitaani na baadaye Serikali kutangaza kuzima Mapinduzi hayo ambayo hamkani yake ilisababisha vifo vya watu 241 na kujeruhi wengine 2,194.

Lakini lawama za jaribio hilo zikatupwa kwa mkimbizi wa kisiasa mpinzani wa Rais Erdogan, Fethullah Gulen, anayeishi Marekani tangu mwaka 1999 anayeshutumiwa kutumia mtandao wake wa kidini wa ‘Hizmet’ unaomiliki taasisi za misaada, vyombo vya habari na shule kadhaa ndani na nje ya Uturuki. Swali la kiuchokozi kwa Rais Erdogan lingekuwa, ilikuwaje waliotaka kumpindua walizingira ndege aliyokuwa anasafiria kwa ndege vita bila kuitungua kama walidhamiria kumuondosha madarakani?

Isije kuwa jaribio hilo la Mapinduzi lilitayarishwa kupatikana sababu ya kuwafagia wasiotakiwa! Hakika maswali yangekuwa mengi kwake lakini tunamshukuru kwa kututembelea, tunamkaribisha tena ili tupate fursa ya kujibiwa yanayotusumbua nafsi kutokana na siasa za hamkani nchini mwake na staili yake ya uongozi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here