24.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

UJENZI BOMBA LA MAFUTA FURSA NZURI KWA WATANZANIA

Na Said Ameir

– MAELEZO

HIVI karibuni Rais Dk. John Magufuli na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwa pamoja waliweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga Tanzania.

Mradi huu unaojulikana kama Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), unatekelezwa kwa ubia kati ya washirika wa sekta binafsi na sekta za umma za nchi za Tanzania na Uganda.

Washirika hao ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya Taifa ya Petroli ya Uganda (UNOC), Kampuni ya Mafuta ya Total ya Ufaransa, Kampuni ya TULLOW yenye makao makuu yake London nchini Uingereza na Kampuni ya China National Offshore Oil Company (CNOOC).

Bomba ambalo litagharimu Dola za Marekani 3.5 bilioni, sehemu yake kubwa yaani kilomita 1,115 kati ya kilomita 1,445 litajengwa katika ardhi ya Tanzania na kupita mikoa 8, wilaya 24 na vijiji 184.

Kutokana na hali hiyo, inaelezwa kuwa mradi huu wakati wa ujenzi na utakapokamilika, utatoa na fursa nyingi za kiuchumi ambazo zitasaidia sana kuchangamsha shughuli za kiuchumi, hivyo kuchangia ukuaji uchumi na kuinua kiwango cha maisha ya Watanzania kwa namna mbalimbali.

Mradi huu ni mfano wa ushirikiano kati ya nchi za Tanzania na Uganda na kwa upande mwingine ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta za umma katika nchi hizi.

Katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake, mradi huu utahitaji ushiriki wa sekta binafsi katika nchi zote mbili na wakati mwingine hata taasisi nyingine za umma ambazo zinatoa huduma zitakazohitajika na mradi.

Kwa hiyo, wakati tukisifia kuwa ni mfano wa mradi wa ubia wa sekta ya umma na sekta binafsi katika nchi zetu, Watanzania hawana budi kuelewa kuwa wana wajibu mkubwa wa kuzitumia vyema fursa za mradi huu.

Kwa Tanzania, mradi huu unaweza kuonesha picha halisi ya ushirikiano wa sekta hizo kwa kuzingatia namna makampuni na taasisi za humu nchini zitakavyoweza kushiriki na kufanikisha mradi huu.

Kwa maana nyingine ni mradi ambao unaweza kutumika kupima utayari, umakini, uwezo na ujasiri wa Watanzania katika kuchangamkia fursa za kiuchumi.

Kama alivyoeleza Rais Magufuli wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi kuwa katika mradi huu, Serikali imesamehe mambo mengi ili uweze kutekelezwa kwa kuishirikisha Tanzania. Wataalamu wa nchi walichambua na kupembua hadi kubaini kuwa kusamehe huko kutafidiwa na fursa nyingi zitakazoletwa na mradi huu.

Kwa maana hiyo bila ya Watanzania kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha wanazitumia kadiri itakavyowezekana fursa hizo, uamuzi huo wa Serikali kusamehe hivyo ilivyovisamehe hautakuwa na maana yoyote.

Kuja kwa mradi huu Tanzania, Watanzania hawana budi kuipongeza Serikali chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa jitihada kubwa kwa kutumia ushawishi wa kisiasa, kidiplomasia, uchumi na ukaribu wa viongozi wa nchi hizo mbili pamoja na hoja nyingine hadi kufanikisha mradi huu kuja Tanzania.

Jitihada hizi ni kielelezo cha dhamira ya kweli iliyonayo Serikali ya Awamu ya Tano ya kutafuta kila aina ya fursa za kiuchumi ambazo zitasaidia kutimiza ahadi zake kwa Watanzania ya kujenga Tanzania yenye uchumi imara.

Serikali imejitwika mzigo mkubwa wa kushiriki katika kutekeleza mradi huu mkubwa wa aina yake, lakini imefanya hivyo kwa kuamini kuwa Watanzania wako tayari na wako imara kuupokea kwa hali na mali.

Imeelezwa mara kwa mara kuwa mradi huu utaliingizia Taifa mapato makubwa, utaleta teknolojia na utaalamu na fursa za kiuchumi ambazo watekelezaji wake kwa kiwango kikubwa ni kutoka sekta binafsi. Kwa mnasaba huo, Serikali hapa imefanya zaidi ya wajibu wake ambao ni wa kujenga mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji.

Wale wahenga wa Cambrigde walisema ‘give us the tools and lets finish the job’ na hivi ndivyo ilivyofanya Serikali kwa mradi huu. Imeleta mradi na kufungua fursa tele ambazo Watanzania wanapaswa kuzitumia kujenga uchumi wao binafsi na uchumi wa Taifa.

Haitakuwa na maana hata kidogo katika ngazi ya Serikali na katika ngazi ya Mtanzania mmoja mmoja kufika wakati fursa za mradi huu kuchukuliwa na wageni kwa sababu zozote na katika mazingira yoyote yale. Ikifikia hatua hiyo Watanzania watakuwa wamewaangusha viongozi wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,454FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles