24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

UCHUMI WA MAKAA YA MAWE WAANZA RASMI NA TANCOAL

 

 

Na Mwandishi Wetu,

KUNA kicheko kwenye Kampuni ya Uchimbaji Makaa ya Mawe Nchini (Tancoal Energy) kwa kuweza kufikisha na kuzidi mahitaji ya viwanda vya saruji ya makaa ya mawe  nchini kwa kuzalisha zaidi ya tani 80,000 kwa mwezi kuanzia Desemba mwaka jana.

Hofu ya kuonekana hawawezi imekwisha na sasa wanajiimarisha kudhibiti soko la ndani kwa maelezo ya uongozi wa Kampuni ya TanCoal.

Madai hayo ya Kampuni yanatolewa huku Kamati  ya Bunge ya Viwanda, Biashara  na Mazingira  kupitia Mwenyekiti wake, Stanslaus Nyongo, ikidai  wiki liyopita bungeni kuwa Serikali iruhusu tena uagizaji makaa ya mawe kutoka nje kwani Tancoal imeshindwa kutosheleza mahitaji.

Kampuni ya kutoka Australia ya Intra Energy Corporation ambayo inamiliki asilimia 70 ya hisa za Tancoal, imesema mafanikio hayo yametokana na sera mpya ya Serikali ya kuzuia uagizaji wa makaa ya mawe kutoka nje na mwitikio chanya kutoka kampuni za saruji nchini kununua kutoka kwao.

Wachunguzi wa mambo ya uchumi  wanadai kuwa uchumi wa makaa ya mawe kuwa umeanza rasmi sasa na kushauri Ngaka Coalfield itoke kwenye utafutaji makaa (exploration) na iwe mzalishaji mali ili ianze kulipa kodi rasmi za Serikali kwani bila kubadilisha hadhi  yake watachelea kulipa kodi na TRA itashindwa kuwaadhibu vilivyo.

Kampuni hiyo imesema wateja wake wa viwanda vya saruji  nchini wameagiza wastani wa tani 60,000 za makaa ya mawe kwa mwezi na hivyo kupunguza kutoelewana na Serikali iliyokuwa inafikiri kuwa haina uwezo wa uzalishaji mkubwa na sasa wanajizatiti kuongeza uzalishaji zaidi.

Kampuni hiyo imeweza kuongeza uzalishaji  baada ya kununua mitambo mipya ya uchimbaji,  uchakataji na ya ubora wa bidhaa zake (quality assurance).

Ofisa Mtendaji Mkuu, James Shedd, anasema kupigwa marafuku makaa ya mawe kutoka nje Agosti mwaka jana imeongeza mahitaji ya ndani na kufikia tani  za ujazo 60,000 kwa mwezi na wanazimudu kuchimba na hivyo wako imara kufanya mengine makubwa ikiwamo kuzalisha umeme kwa siku za usoni na kuanzisha matofali ya makaa ya mawe kwa kupikia majumbani.

Mipango ya Ngaka Coal Mine ambayo Serikali inamiliki asilimia 30 kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) ambapo Intra Energy (T) Limited  inamiliki asilimia 70, iko wilayani Mbinga, Mkoa Ruvuma kilomita 40 kutoka Ziwa Nyasa na kilomita 1,100 toka Dar es Salaam. Kufikia Januari mwaka jana, ilitumia Dola za Marekani milioni 23 kwa utafiti na matayarisho ya awali ya uchimbaji.

Mradi huo wa PPP utazalisha umeme wa MW 200 na kinu kitajengwa Mbinga katika mradi uliopangwa kugharimu Dola za Marekani  milioni 236.

Kabla ya Serikali kuzuia uagizaji wa makaa ya mawe kutoka nje hasa Afrika Kusini, Tancoal ilikuwa ikipata hasara, jambo ambalo Waziri Mkuu alipotembelea Mgodi alilipinga  kwa kuonesha takwimu ambazo hazikuwemo kwenye taarifa ya Tancoal kwake. Majaliwa alitembelea mgodi huo miezi miwili iliyopita.

Uzalishaji wa jumla kwa mwaka  jana  ulikuwa tani 248,468 na mauzo yalikuwa tani 246,197 kwa wastani wa asilimia 10, ambayo ni kiwango cha chini sana.

Mapato ya mauzo ya mwaka jana yalikuwa dola ya Australia (AUD) milioni 14.408 sawa na Sh bilioni 23.9, hii ilitokana na kuagiza makaa ya mawe nje na kuingiza katika soko la ndani ambayo yalikuwa yanaathiri  mauzo na bei.

Takribani tani 150,000 ziliingia nchini kati ya Desemba 2015 na Aprili, 2016 ambayo ilisababisha kushuka kwa mauzo kutoka tani 137,055 kufikia  na  Dola za Australia 109, 142 katika nusu  mwaka badala ya kuongezeka. Matokeo hayo yalisababisha hasara ya AU$million 2.1 sawa na Sh.milioni 718.8 nusu ya kwanza ya mwaka lakini sasa mambo ni mazuri.

Tancoal wametakiwa kujieleza mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, baada ya ripoti yao ya mahesabu kutoendana na uhalisia na hivyo kuleta hisia za ufisadi kwenye mradi huo.

Hatua hiyo ilimlazimu Waziri mkuu kumwagiza Msajili wa Hazina  kufanya uchunguzi wa kina na wa kijinai (forensic investigation) katika mapato na matumizi ya kampuni ya Tancoal kama yanaendana na mahesabu yaliyotolewa awali na kudai Serikali ipate gawio lake kinyume na maelezo ya Tancoal.

Jambo la makampuni ya migodi nchini kuonesha hasara tu bila faida ni kero kwani pamoja na hali hiyo huwa hawataki kuachia migodi hiyo ikimaanisha  kuwa wanafaidika ila wanasema uongo ili kuinyima Serikali haki yake. Hata Rais John Magufuli alikemea kampuni za dhahabu wakati alipokuwa ziarani Simiyu  na kuasa kuachwa kwa tabia hiyo chafu.

Waziri Mkuu Kasim Majaliwa alipotembelea mgodi huo wa Ngaka wa Tancoal alishangaa kuona tofauti za hesabu na kudai uchunguzi kamili kwani Serikali ina asilimia 30 kwenye hisa na umiliki wa Tan Coal Mine Ngaka.

 Alisema: “Hesabu ya kampuni hiyo inaonyesha kuwa mmepata hasara kila mwaka, lakini rekodi nilizonazo zinanionyesha kuwa mwaka 2013 mlipanga kuzalisha tani 50,000 na mliuza zaidi ya hapo.

 “Desemba 2013 mliuza tani 39,000 kwa wamiliki wa viwanda vya nguo, pia mliuza tani 2,000 kwa Kampuni ya Saruji ya Zambia, Novemba 2013 mliingia makubaliano ya kuuza tani 165,000 kwa kampuni ya saruji ya Tanzania na ziliuzwa. Mbona ‘financial statement’ zenu zinasema mwaka huo nao mlipata hasara?” Aling’aka Majaliwa.

“Mnasema gawio hutolewa baada ya mtu kutangaza faida. Mbona mlivuka lengo lakini mkatangaza kuwa kampuni imepata hasara katika mwaka huo wa fedha,” alihoji Waziri Mkuu.

Oktoba mwaka jana, kampuni ya kutoka China ya Sino Hydro Corporation iliingia makubaliano ya kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 270 kwa kutumia makaa ya mawe utakaoitwa Ngaka Power Station.

Mitambo ya Ngaka Power Station inatarajia kutumia kiasi cha tani milioni 1.2 kwa mwaka kutoka Tancoal, ambayo ina hifadhi ya tani milioni 423 wakati bonde la Ruhuhu lina hazina ya makaa ya mawe tani bilioni 2.1.

Kwa maelezo ya Tancoal inaonyesha Mradi wa Ngaka utakapomalizika utaweza kuchangia asilimia 15 ya umeme katika gridi ya Taifa na bonde la Ngaka ndani ya Ruhuhu linakadiriwa kuwa na hifadhi ya kutosha ya makaa.

Aidha, Tancoal huuza makaa ya mawe katika nchi jirani, kama Malawi asilimia 1.5, Kenya asilimia 2.8 na Rwanda asilimia 9.

Inakadiriwa kuwa sekta ya saruji inahitaji tani 500,000 kwa mwaka ambayo Tancoal  kirahisi ina uwezo wa kufikia kiwango hicho.

Kuna viwanda saba vya saruji na kila kimoja kina mahitaji yake ambayo Tancoal imeahidi kuyatekeleza vilivyo na hivi kuleta taswira chanya ya mchango wa rasilimali hiyo kedekede katika ukuaji wa uchumi wa nchi hii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles