RC MBEYA AAGIZA VIONGOZI KUWA KARIBU NA WAKULIMA

0
449

Na ELIUD NGONDO, MBEYA


MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala, amewaagiza wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote na wakuu wa wilaya kuwa karibu na wakulima ili kuwasaidia kutoa majibu juu ya uchelewaji wa pembejeo za kilimo, hasa mbolea na mbegu.

Makalla alitoa agizo hilo wakati alipofanya mkutano na wakulima wa zao la tumbaku wa Wilaya ya Chunya, ambao walilalamikia pembejeo hizo kuchelewa kuwafikia.

Alisema endapo viongozi hao watakuwa karibu na wakulima, itakuwa ni rahisi wakulima hao kuwa na uhakika wa kupata pembejeo hizo kwa wakati ama kutumia njia mbadala ya kuzipata kwa sababu watakuwa na taarifa za kutosha kuliko kuwaacha wakiwa na matumaini ambayo hayana tija kwao.

“Wakulima wanatakiwa wawe na taarifa za kutosha kuhusu upatikanaji wa pembejeo katika msimu wa kilimo husika, ndiyo dawa pekee kama tunataka kuzalisha kwa tija, wakuu wa wilaya na wakurugenzi hakikisheni mnalitekeleza hilo kwa vitendo,” alisema Makalla.

 

Hata hivyo, aliwasisitiza viongozi hao kufuatilia pembejeo hizo kabla msimu haujaanza, ili na wao wawe na uhakika wa kuzipata na kuwapa wananchi taarifa sahihi na za uhakika.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Tumbaku Wilaya ya Chunya, Hadson Mwamwembe, alisema kwa miaka mingi wakulima wengi wamehamasika kutumia mbinu za kisasa katika uzalishaji wa mazao, lakini kikwazo ni pembejeo ambazo hufika kwa kuchelewa.

 

Alisema kitendo hicho kinawafanya washindwe kulima mazao kwa kuendana na msimu husika, hivyo kusababisha hata mavuno kutokuwa ya kutosheleza mahitaji ya soko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here