24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ubunge wa Mwambe wazua mtanziko

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya aliyekuwa Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe, kudai kuwa atatinga bungeni na kukaa upande wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kueleza kutotambua barua ya Chadema kuhusu ukomo wa ubunge wake, wachambuzi wameonya kuwa jambo hilo linaweza kuleta hatari.

Juzi Jioni gazeti dada la hili la MTANZANIA Jumamosi lilifuatilia kuona kama Mwambe ataingia bungeni lakini hakuonekana.

Mwambe ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Ndanda, Februari 15 mwaka huu alitangaza kujivua uanachama wa Chadema akiwa ofisi ndogo za Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Lumumba, Dar es Salaam na kupokewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho tawala, Humphrey Polepole.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana kuhusu sakata hilo Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC),  Onesmo Olengurumwa alisema hilo ni jambo ambalo liko wazi kwamba kilichofanyika ni uvunjaji wa Katiba ya nchi.

“Mimi nadhani hivi ni vitu ambavyo viko kinyume kabisa na sheria na Katiba sababu ukiangalia katika ibala ya 71 imebainisha fika sababu zinazoweza kusababisha mbunge kukoma kuwa mbunge ikiwamo ile ya mbunge kuhama chama chake kwenda kingine.

“Hivyo hii ipo wazi kwamba mbunge akihama chama anakuwa amekosa sifa moja kwa moja wala huhitaji barua kutoka kwa chama chake na hata ukiangalia Chadema wamefanya vema kwa kumfahamisha Spika kupitia barua.

“Hivyo kilichofanyika na Spika wa Bunge, Ndugai ni bayana kwamba ni uvunjaji wa Katiba wa hali ya juu ikiwamo kutokuzingatia utawala wa sheria sababu ameona kwamba ameshafanya mambo mengi kinyume na Katiba na hakuna mtu aliyeweza kumchukulia hatua yoyote hivyo hii tunasema kuwa ni mwendelezo tu kwa kuamini kuwa hakuna wa kuchukua hatua ikiwamo pia mifumo yetu ya kisheria kutokuwa rafiki,” alisema Olengurumwa.

Alisema kama taifa bado kuna changamoto ya kuondoa madaraka kwa mtu binafsi na kuachia taasisi kama inavyotokea hivi sasa.

 “Hivyo masikitiko ni makubwa ndani ya jamii juu ya kitendo cha juzi, unapomwona mtu ambaye amejivua uanachama na kupoteza sifa ya ubunge unapomrejesha tena bungeni na kumkingia kifua ni jambo la kusema kwamba tunamwachia Mungu tu kwani kama ni sheria zetu kama nchi zimekiukwa na Watanzania wenyewe wanaona,” alisema Olengurumwa.

Alisema iwapo itatokea Mwambe akalipwa stahiki zake kama mbunge basi ni dhahiri kuwa itakuwa ni matumizi mabaya ya ofisi.

“Kama itatokeo yakafanyika marekebisho ya Katiba basi ni dhahiri  kuwa kutakuwa na haki ya kusema kuna matumizi mabaya ya ofisi na hasa iwapo mbunge husika atalipwa stahiki zake.

“Hivyo ni lazima baadaye iangaliwe namna alivyotumia nafasi yake ya Uspika kwani kuna mambo mengi yamefanyika kwa Maspika wote waliopita lakini hakujawahi kutokea matukio mazito yaliyo bayana kama haya yasasa, kwani kuna vitu vingine vinafanyika unaona fika kwamba viko kinyume na sheria kiasi kwamba kwasasa hata mtoto mdogo anajua kabisa hili lililotokea ni kosa, hivyo mimi nitaendelea kufuatilia jambo hili kuona iwapo kuna nafasi ya kuwajibishwa kwa Spika baada ya kustaafu,” alisema Olengurumwa.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha Iringa, Profesa Gaundence Mpangala, akizungumzia sakata hilo alisema kuwa jambo hilo liko kinyume kabisa na sheria na Katiba ya nchi.

“Mimi nashangaa kwa nini Spika anavunja sheria na Katiba ya nchi nashangaa? Kwa sababu miaka yote hata hivi karibuni wakiwamo wabunge wengi waliohama kutoka Chadema kwenda CCM walipoteza ubunge wao hadi ulipofanyika uchaguzi ndipo wakawapitisha.

“Lakini mbunge aliyeingia bungeni kwa chama fulani cha siasa anapojiuzulu chama hicho moja kwa moja kwamba anakuwa amepoteza sifa siyo mbunge tena, sasa nashangaa kuona Mwambe anaendelea kuruhusiwa kuendelea na ubunge wakati alishajiuzulu rasmi Chadema wote tunashangaa.

“Unajua katika nchi hata baba wa taifa (Hayati Julias Nyerere) aliwahi kusema kwamba mnapoanza kukiuka Katiba mnakuwa mnaipeleka nchi kwenye machafuko kwani hivi ni vitu vya kuvishemu sana kwenye nchi, unadhani hili linaleta taswira gani katika taifa?,” alihoji Profesa Mpangala.

Akizungumzia hoja zilizotolewa na Spika Ndugai kwamba Chadema walishindwa kuambatanisha baadhi ya nyaraka kwenye  barua waliyomwandikia Spika Ndugai, alisema; “hoja hiyo haina mashiko”.

“Mimi siioni hii kama sababu, maana sote tunakumbuka kuwa kujiuzulu kwa Mwambe kulikuwa ni wazi ambapo kila mtu alijua baada ya kutangaza kwenye vyombo vya habari kwamba anajiondoa ndani ya chama hicho baada ya kushindwa uchaguzi waliposhindana na Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe).

“Madhara ya hili ni kukiuka Katiba na sheria za nchi, kwani Spika wa Bunge ambaye ana kazi ya kulinda vitu hivi viwili inasikitisha kuona kwamba kama taifa tunaenda wapi, kwani upendeleo na ubaguzi wa waziwazi unafanywa sasahivi kitu ambacho siyo kizuri hata kidogo na hii inaweza kusababisha hata nchi kutumbukia kwenye machafuko.

“Kwani mengi tu yanayofanyika wananchi wanayaona sababu wamekuwa ni kinyume cha Katiba na sheria, hivyo hata hii nchi tunayosema kwamba ni nchi ya amani itakuja ifikie ukomo kwani msingi wa amani ni demokrasia na utawala bora ndiyo msingi wake hivyo haya yakikiukwa msingi wa amani unaweza ukayumba na nchi ikawa na vurugu tu kwani tunapaswa kutoa haki kwa wote,” alisema Profesa Mpangala.

Kwa upande wake Mwanasheria Jebra Kambole akizungumzia suala hilo alisema “Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 71(1) (e) ubùnge wa Mwambe ulikoma alipojiunga na CCM, hana uhalali wa kuendelea kuwa mbunge, yeye pamoja na spika wanakiuka ibara ya 26(1) ya Katiba ambapo watu wote wanapaswa kuheshimu Katiba.

“Siku hizi ukiwa na madaraka kukiuka Katiba na sheria ni jambo la kawaida sana, wanaharakati na vyama vya siasa hili sio la kulifumbia macho,” alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles