29.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

TUSIWANYIME WATOTO FURSA YA KUFAHAMIANA NA FAMILIA TANDAA

Na Christian Bwaya


SUALA la malezi limepewa uzito mkubwa katika mila zetu za Kiafrika. Tangu mtoto anazaliwa, familia nzima iliwajibika kumtunza mama aliyejifungua na hivyo mtoto na mama walipata muda wa kutosha kujenga uhusiano wa karibu.

Hata baada ya mama kupata nguvu na kuendelea na shughuli nyingine za kawaida, bado mtoto aliendelea kuwa na nafasi muhimu kwenye ratiba za mama. Ilipolazimu, mama alifanya shughuli zake akiwa amembeba mwanawe mgongoni. Kumbeba haikuwa na maana ya mama kujichosha bali kumwangalia mwanawe kwa karibu.

Nyakati za jioni zilikuwa fursa ya wazazi na watoto kukaa pamoja. Watoto walikusanyika kusikiliza hadithi, methali na vitendawili. Desturi hii ilikuwa darasa muhimu lililokuza uelewa wa watoto na kuwafunza kuhusu jamii yao na wajibu walionao kama sehemu ya jamii.

Sambamba na hayo, michezo ilikuwa sehemu muhimu ya maisha ya mtoto. Jamii iliheshimu hitaji la mtoto kucheza na wenzake. Katika michezo, vifaa vingi vilitengenezwa kwa kutumia vitu vya kawaida vinavyopatikana kwenye mazingira yao kukuza ubunifu.

Pia, mtoto alitarajiwa kushiriki kazi za mikono. Mama, kwa mfano; alihakikisha watoto wanaanza kutumwa kufanya shughuli ndogo ndogo za nyumbani tangu kungali mapema. Watoto walifagia nyumba, waliosha vyombo, walikaa na wadogo zao. Baba naye aliwashirikisha watoto wa kiume kwenye majukumu ya kuchunga au kutafuta majani ya mifugo inayofugwa nyumbani.

Kufanya hivi haikumaanisha wazazi hawakuwa na uwezo wa kufanya kazi hizo. Lengo lilikuwa kuwafundisha watoto tabia ya uwajibikaji. Kupitia ushiriki wa kazi za mikono tangu wakiwa wadogo, watoto walijifunza ujuzi mwingi bila kutumia mtaala rasmi.

Jamii zetu zilithamini uhusiano na ukoo wa pande zote mbili. Wazazi, wajomba, akina shangazi, mama na baba wadogo, binamu, wapwa, bibi na babu walikuwa sehemu muhimu katika uhusiano wa familia. Kufahamiana na kuitambua familia tandaa lilikuwa ni sharti la msingi kwa kila mtoto.

Wakati mwingine, kulikuwa na mwingiliano wa kimaisha baina ya familia na familia. Ndugu walisaidiana kwa shida na raha. Kadhalika, ndugu walitembeleana mara kwa mara. Mwingiliano huu ulisaidia kuimarisha uhusiano ya karibu katika jamii. Mtoto alishuhudia uhusiano wa namna hii na kuuchukulia kuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku. Pia, ilimsaidia kuuelewa ukoo wake na hivyo alijitambua mapema.

Kwa bahati mbaya tumeanza kuipa mkono desturi hii ambayo imekuwa sehemu ya utambulisho wa jamii yetu kwa muda mrefu. Uhusiano na familia umeanza kufifia. Watoto wa siku hizi wananyimwa fursa ya kufahamiana kwa karibu na familia tandaa. Hawaoni wazazi wakitembeleana na ndugu wengine wa ukoo. Hawaoni mawasiliano ya karibu na ndugu wengine.

Kadhalika, jamii zetu zilikuwa na mfumo rasmi wa mafundisho maalumu kwa ajili ya watoto wanaopevuka kimwili. Balehe haikuachwa ipite hivi hivi. Watoto wa kiume, kwa mfano; wafanyiwa tohara iliyoambatana na utaratibu wa kuwafunza kuelewa nafasi yao kama wanaume wanaotegemewa na jamii.

Mtoto wa kike naye hakuachwa nyuma. Ingawa hatuungi utamaduni wa tohara kwa wanawake, kazi ya kumfundisha binti majukumu yake kama mwanamke anayejitambua ilikuwa muhimu. Katika kipindi cha mpito kuelekea utu uzima, msichana alisaidiwa kujua yeye  ni nani na jamii ina matarajio gani kwake. Kwa ujumla desturi kama hizi zilisaidia kuwaandaa vijana timamu, wanaojielewa na kufahamu wajibu walionao katika jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,225FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles