23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

ILI UFANIKIWE, EPUKA KUWEKA MALENGO YASIYOTEKELEZEKA

Na Christian Bwaya


WATU wengi wana utaratibu wa kujiwekea malengo hasa mwaka unapoanza. Bahati mbaya kadri siku zinavyoenda ndivyo wanavyosahau malengo yao. Tafiti za utekelezaji wa malengo zinaonesha kuwa katika watu 10 wanaojiwekea malengo yao, mmoja tu ndiye anayeweza kuyasimamia na kuyatekeleza.  Tisa huishia njiani na wakati mwingine hupanga malengo mengine ambayo nayo huwa hayatekelezeki.

Kuna sababu nyingi zinazofanya watu washindwe kutekeleza maazimio wanayoyaweka. Moja, kuweka maazimio kwa msisimko usioenda sambamba na tafakari ya kina ya kile wanacholenga kukitekeleza. Pili, kuweka malengo mapana mno yasiyopimika, pia kutokujua uliko mzizi wa mabadiliko ya tabia hasa pale malengo hayo yanapohusisha mabadiliko ya tabia.

Je, unawezaje kusimamia malengo yako na kuyatekeleza? Katika makala haya tunaangazia siri kubwa tano unazoweza kuzitumia.

 

Melengo yapimike

Usiweke malengo mapana yasiyolenga jambo mahususi. Vunja vunja wazo kuu ulilonalo kuwa malengo madogo madogo yanayolenga jambo moja utakaloliishi kila siku.

Kwa mfano, badala ya kuazimia kujenga tabia ya jumla kusoma, azimia kusoma kitabu kimoja kwa juma moja. Lengo la kusoma kitabu kimoja kila juma ni mahususi, lakini lengo la kusoma ni pana kwa sababu halieleweki ni kusoma vitabu vingapi kwa mwezi, miezi sita au hata miezi 12.

Kama unataka kuwa na uhusiano imara na familia yako mwakani, fafanua kwa namna gani. Je, ni kuwahi nyumbani kila siku baada ya kazi? Ni kutoka na wanao kila mwisho wa juma? Fanya malengo yako yapimike kwa muda maalumu.

 

Mfumo wa uwajibikaji

Unapokuwa na malengo makubwa yasiyokufanya uwajibike kila siku, itakuwa vigumu kufanikiwa. Muhimu kuweka mfumo mzuri wa kujipima kila siku kwa sababu huwezi kubadili tabia usiyoweza kuipima.

Hakikisha malengo yako yanapimika kadri unavyoendelea kuyatekeleza. Ili uweze kupima, weka muda maalumu wa kuyatekeleza. Andika malengo yako mahali ikusaidie kukumbuka ulichopanga.

Kwa mfano, kama unalenga kupanua biashara yako, fikiria utakavyoweza kupima upanuzi huo. Je, utatazama kiasi cha mtaji unaoongezeka? Je, ni kiasi cha bidhaa unachoouza, idadi ya wateja unaowapata? Utapimaje?

 

Shirikisha watu unaowaamini

Wakati mwingine ni rahisi kuachana na mipango uliyojiwekea kadri muda unavyokwenda. Sababu ni kuwa unajikuta huna mfumo wa kukuwajibisha pale unapoteleza. Ni muhimu kuwa na watu watakaokufanya ujisikie vibaya kuachana na mpango wako.

Baada ya kuhakiki malengo yako, fikiria watu wako wa karibu unaoweza kuwaambia kile ulichokipanga. Kama maazimio yako yanamhusu mkeo/mumeo, mwambie mapema. Kama kinawahusu wanao, waambie. Kwa kufanya hivyo, unatengeneza mfumo wa kukuwajibisha pale unapoanza kususua susua.

Kadhalika, ikiwa unataka kuacha sigara, pombe au tabia fulani wanazozijua rafiki zako, tangaza wazi wazi. Wanapojua mpango wako unajiweka katika mazingira ya kulazimika kutekeleza usionekana mtu wa maneno yasiyotekelezeka.

 

Usingoje kesho

Mara nyingi watu husahau malengo yao kwa sababu wanasubiri kuanza kesho. Wanajifariji kuwa bado wanajipanga ili kuanza utekelezaji. Lakini kadri muda unavyokwenda, wanajikuta wakikosa hamasa.

Usisubiri kesho kuanza kufanya kitu sahihi. Anza mara moja, kama lengo ni kuanza kusoma, kanunue kitabu anza kukisoma. Muda haukusubiri, utengeneze. Azimia kutengeneza muda wa kusoma, utaweza.

Kama unalenga kuongeza akiba kila mwezi, usisubiri mwezi ujao. Anza mwezi huu. Weka akiba kabla ya kufanya matumizi.

 

Usikate tamaa kwa hatua ndogo

Huwezi kutekeleza lengo kubwa bila hatua ndogo. Jifunze kufurahia hatua ndogo unayopiga kuelekea kwenye lengo kubwa. Usisubiri utekelezaji mkubwa ili ufurahie.

Hata unapokwama, usikate tamaa na kughairi malengo yako. Songa mbele. Kama unataka kupunguza uzito, usikate tamaa unapogundua uzito ndio kwanza unaongezeka. Mwili unapenda mazoea, mara nyingi mabadiliko huchukua muda kuendana na mwili.

Pia unapopiga hatua ndogo, ifurahie. Usirudi nyuma kwa sababu tu hujaona mabadiliko makubwa kama ulivyotarajia. Furahia hatua yoyote ndogo unayopiga kuelekea kwenye hatua kubwa unayoitarajia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles