21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 4, 2022

TUSIONE AIBU KUKIRI UDART IMESHINDWA

NA MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM


SINTOFAHAMU iliyopo sasa katika mradi wa mabasi yaendayo kasi, inaonyesha kuwa Kampuni ya Uda-Rapid Transit (UDART) inayouendesha haina uwezo, ujuzi na dhamira ya dhati ya kuuendesha.

UDART ambayo mbia wake mkubwa ni Kampuni ya Simon Group, inaandamwa na rundo la lawama na tuhuma katika uendeshaji wa mradi huo huku ikiwa haina majibu ya moja kwa moja ya kuiondoa kwenye lawama za kushindwa.

Katikati ya tuhuma na lawama zinazoiandama UDART, wananchi ambao ndio watumiaji wa usafiri wa mabasi ya mwendo kasi, wanazidi kuumizwa na huduma mbovu na pia Serikali imepoteza mamilioni ya fedha kipindi ambacho imejifunga mkanda kukusanya kila Sh yake kwa ajili ya kuitumia kuinua maisha ya watu wake.

Watanzania tunatambua kuwa kipindi hiki ukusanyaji wa mapato ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli na timu yake nzima wamekuwa na kauli moja kuwa wanawahitaji wawekezaji kwa sharti moja muhimu la kufuata sheria za nchi.

Kauli hii inayosisitizwa kila mara na viongozi wetu, inaonekana kutopewa uzito unaostahili na UDART na au kushindwa kuitekeleza kwa sababu mwekezaji huyu hana uwezo wa kuendesha mradi mkubwa na muhimu kwa wananchi, kinyume na ilivyotarajiwa na Serikali yenyewe na pia wananchi.

Sababu zinazoashiria kushindwa kwa UDART zipo nyingi; ya kwanza ni mgomo baridi wa wafanyakazi uliofanyika Aprili 24, mwaka huu. Wafanyakazi waliogoma kushinikiza walipwe mishahara yao walikuwa wakikatisha tiketi katika vituo vya mabasi vya mwendokasi.

Ikumbukwe kuwa UDART ni mbia wa Serikali katika mfumo wa PPP, hivyo Serikali ina wajibu wa kuisaidia kampuni hii ambayo lengo lake ni kurejea mikononi mwa wananchi kwa kuuza hisa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Yapo mashaka kuhusu kufikiwa kwa lengo hilo kwa sababu kwa mujibu wa Meneja Uhusiano wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), William Gatambi, mradi huo ambao wakati unaanza mwaka 2016 ulikuwa na uwezo wa kusafirisha abiria 75,000, idadi ya wasafiri imeongezeka hadi kufikia 200,000 kwa siku na hivyo kuielemea UDART ambayo inaonekana haina uwezo wa kuhudumia kiasi hicho cha wasafiri.

Hili DART inalijua na ndiyo maana imekwishakiri hadharani kuwa inatambua usumbufu wanaoupata abiria na hivi sasa upo mchakato wa kumpata mwekezaji mwingine ambaye baada ya kuanza kazi, kutakuwa na mabasi 305 yatakayosaidia kukabiliana na idadi kubwa ya abiria walioielemea UDART.

Mbali na hilo, kuna sakata la mapato yanayotoka kwa abiria ambao kila mmoja hulipa Sh 650 kila anapotumia usafiri huo na hivyo kufanya mapato ya jumla kwa siku kuwa Sh milioni 130,000.

Katika mgomo wa wafanyakazi wa Aprili  24 pamoja ule uliofanyika Mei 16, mwaka huu, inaelezwa kuwa Serikali ilipoteza zaidi ya Sh milioni 300.

Upotevu wa mapato haya ulisababishwa na uzembe na ama kukosekana usimamizi mzuri wa UDART ambayo licha ya kuwa  na kitengo cha habari na uhusiano, imeshindwa kutoa maelezo ya kina kwa umma kuhusu sababu za kutokea kwa upotevu huo.

Na kama ilivyo kwa UDART, ni hivyo hivyo pia kwa DART kwa sababu nao hawajaeleza kwa kina ni nini kilichotokea na hatua zitakazochukuliwa kwa upotevu huo.

Kinachoelezwa na baadhi ya watumishi wa mradi huo ni kwamba mtikisiko wa mgomo baridi wa wafanyakazi ulitoa fursa kwa baadhi yao kujikusanyia fedha watakavyo baada ya kukwama kwa ukatishaji wa tiketi za Kieletroniki.

Katika mgomo huo, baadhi ya madereva wa magari yanayofanya safari zake kutoka Kimara-Mbezi, walichota fedha milangoni huku abiria wengi wakipanda bure kwenye vituo vingi vya mabasi hayo.

Taarifa za upotevu huo wa mamilioni ya fedha ambazo Serikali ina sehemu yake, hazikuwa za siri kwa sababu ziliripotiwa na vyombo vya habari kuwa zilichukuliwa kwenye makusanyo milangoni nyakati za asubuhi, wakati abiria wengi wasiokuwa na kadi maalumu za UDART wakikata tiketi za Kiletroniki chini ya Kampuni ya Maxcom Afrika Plc ambayo wakati huo ilikuwa imesitisha kutoa huduma.

Haikuishia hapo kwani iliripotiwa zaidi kuwa ukwapuaji huo uliendelea tena Juni 2 na 3, siku ambazo mabasi ya mwendokasi yalitoa huduma bure kwa sababu wakatisha tiketi walikuwa kwenye mgomo wa kudai mishahara yao.

Wakati wafanyakazi hao wakiwa katika mgomo wao, UDART walikusanya watu wao na kuanza kukatisha tiketi kama zile zinazotolewa kwenye usafiri wa daladala, hata hivyo walinzi wao walishindwa kuwazuia baadhi ya abiria kuingia bila kukata tiketi, jambo ambalo lilizua vurugu katika baadhi ya vituo kiasi cha kutishia usalama wa abiria.

Katika moja ya ripoti zake, gazeti hili lilieleza kwa kina jinsi hali ilivyokuwa kwa kuvitaja vituo vilivyokumbwa na vurugu kubwa  iliyotishia usalama wa abiria kuwa ni Kimara, Korogwe, Kivukoni, Morocco na Gerezani.

Pamoja na kuwepo kwa vurugu hizo, hali ndani ya mabasi nayo ilikuwa ya wasiwasi na roho mkononi kwa sababu abiria walikuwa wakijazana kupita kiasi kwa sababu ya kuingia bila kulipa nauli na miongoni mwa hao walikuwemo vibaka waliokuwa wakipanda kwa lengo la kuwaibia abiria.

Katika sakata hilo, fedha iliyopotea kwa abiria kupanda bure ni nyingi, pesa iliyopotea kwa kuibwa na watu waliokuwa wakikatisha tiketi ni nyingi. Serikali ilipoteza kiasi kikubwa cha mapato kwa sababu UDART ilishindwa kutekeleza jukumu lake la kusimamia utoaji huduma hiyo kwa namna inavyotakiwa na haikuwa na majibu ya uhakika kuhusu tukio hilo.

Maxcom waliokuwa wabia wakitoa huduma ya tiketi, walitoa taarifa yao kwa umma iliyoeleza kuwa UDART iliwatisha na pia ilitumia nguvu kuwaondoa wafanyakazi waliokuwa wanatoa huduma ya tiketi za kielektroniki katika vituo vya mabasi hayo.

Taarifa ya Maxcom iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Deogratius Lazari, ilieleza kuwa hatua zilizochukuliwa na UDART kuwatisha na kuwaondoa kwa nguvu wafanyakazi hao kisha kuweka wengine, hazikufuata taratibu zilizoainishwa kwenye mikataba ya ajira zao.

“Kuanzia Aprili 13, mwaka huu, kumekuwa na hali ya sintofahamu katika vituo vya mabasi ya mwendo kasi ikiwa ni pamoja na uuzwaji wa tiketi za karatasi (za vishina) ambazo hazitolewi kwenye mfumo wa tiketi za kielektroniki ulioidhinishwa na wasimamizi wa mradi huo.

“Katika mkataba, Maxcom ilihusika kuweka mifumo, rasilimali watu, teknolojia na wasimamizi katika mradi.

“Hivi karibuni UDART walitumia nguvu kuwatisha na kuwaondoa wafanyakazi waliokuwa wanatoa huduma ya tiketi za kielektroniki katika vituo vya mabasi ya mwendokasi bila kufuata taratibu zilizoainishwa kwenye mikataba ya ajira zao,” alikaririwa Lazari na vyombo vya habari.

Haya yote yametokea wakati DART ambayo ina dhamana ya kusimamia mradi huo ipo lakini imeshindwa kukiri mtoa huduma UDART ameshindwa kuendesha mradi huo na badala yake kuwasababishia usumbufu wasafiri.

Mbali na DART, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) nayo haijatoa kauli au kuchukua hatua kuhusu upotevu wa mamilioni ya fedha za Serikali na usimamizi mbovu wa UDART katika mradi huo uliokwishaonyesha sura ya kuhatarisha usalama wa abiria.

DART na Tamisemi wasisubiri wananchi wapaze sauti zao kwa viongozi wakuu wa nchi kuhusu adha wanayoipata  wanapotumia usafiri wa mabasi yaendayo kasi na pia upotevu wa mamilioni ya fedha  za Serikali, bali wajitokeze sasa wakiri kuwa UDART imeshindwa na waeleze mkakati wa kuukwamua mradi huo na jinsi ya kudhibiti upotevu wa fedha wa Serikali.

Mwisho

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,654FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles