24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAANZA KWA KISHINDO, HATUFIKI POPOTE

Na Markus Mpangala,

PROFESA Joseph Mbele alipata kuchapisha andiko lake mwaka 2009 lililohoji: ‘Maendeleo ni nini?’ Katika andiko hilo, alijaribu kuoanisha dhana ya maendeleo katika nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea. Andiko hilo linapatikana katika kitabu chake cha “Changamoto: Insha za Jamii.”

Naomba ninukuu sehemu ya maelezo ya Profesa Mbele: “Dhana ya maendeleo iko kila mahali, katika maisha yetu binafsi na katika maisha ya jamii na nchi kwa ujumla. Sote tunaamini kuwa tunahitaji maendeleo. Tusipofanya jitihada katika maendeleo, tunashinikizwa kwa namna moja au nyingine tufanye hiyo jitihada au tunaburuzwa tuendelee.

Anaongeza kwa kusema: “Katika kuziongelea nchi, watu hutumia dhana ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea au zisizoendelea. Kwa mujibu wa dhana hizo, nchi kama Marekani, Uingereza, Sweden, Ujerumani na Japan zinahesabiwa kuwa zimeendelea. Lakini nchi kama Tanzania, Kenya na Uganda zinahesabiwa kuwa nchi zinazoendelea. Dhana hizi zimejengeka vichwani mwa watu, tangu zamani. Je, tunapotumia dhana hizi, tunaelewa tunachoongelea? Dhana hizi zina mantiki yoyote? (mwisho wa kunukuu)

Kuanzia hapo ndipo dhana ya maendeleo ni nini inatufikisha kwenye mipango, mikakati ya kijamii, kiuchumi, kidiplomasia na kadhalika. Kila uchaguzi unapofika tunaambiwa kuwa mradi fulani utaanzishwa. Vile vile bila hata uchaguzi yaani wakati wowote tunaweza kuambiwa na wenye mamlaka kuwa unaanzishwa mradi fulani kwa manufaa ya jamii.

Tunaweza kuambiwa mradi katika kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa, kanda hadi taifa. Tunaweza kukutana na maelezo mengi yenye lengo moja la miradi ya maendeleo. Mathalani ipo mipango ya Mkukuta, Mkurabita, Mkuza zimetajwa kuwa nyenzo ya maendeleo.

Hoja yangu ni shughuli ambazo zinatuwezesha kutafsiri haya ni maendeleo. Shughuli hizo ndizo hunishangaza pale zinapoanza kwa nguvu kubwa lakini hazifiki mwisho (yaani kukamilisha mradi).

Kuna miradi mingi ndani ya nchi yetu. Tuna mipango pomoni ndani ya taifa hili, lakini ipo kasoro moja kubwa imeota mizizi ya kutokamilisha mipango au mikakati yetu.

Nitatoa mfano, tunayo miradi ya kuanzisha vituo vya afya kwa kila kata ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Lakini mradi huu tangu Serikali iliyopita haukuwahi kukamilika.

Nakumbuka namna ambavyo Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, alivyokuwa akisisitiza juu ya uanzishwaji wa vituo hivyo. Ninakumbuka namna suala hilo lilivyopokewa kwa shangwe.

Tunafahamu kuwa ndani ya taifa letu tunalo tatizo kubwa la huduma za afya. Tunafahamu mahitaji ya huduma ya mama na watoto kote nchini. Tunafahamu namna watu wanavyotembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.

Ujenzi wa vituo vya afya kila kata au hata vijiji ni jambo ambalo lilitakiwa kutiliwa mkazo na kuhakikisha linafanywa kwa ufanisi. Bahati mbaya mpango huo haujawahi kukamilika. Tuliuanza kwa mikakati lakini hatukuweza kukamilisha. Tutakuwa watu wa kuzua mapya hadi lini ilhali ya zamani tunashindwa kukamilisha?

Ndani ya nchi yetu tunafahamu kumekuwa na mpango wa kuanzisha ‘high school’ za kata. Tumefanikiwa kuanzisha sekondari za kata ambazo zimefikisha baadhi ya watu kwenye ajira (kwamba walisoma na kuhitimu, kisha kwenda vyuo vikuu na baadaye kuajiriwa).

Tunafahamu changamoto zinazozikumba shule hizo ambazo ninaamini zinarekebishika. Lakini ni lini tutafanikisha suala la ujenzi wa ‘high school’ za kata ili kusaidia jamii yetu? Ni kwanini hatukumaliza mradi huo?

Hivi karibuni nimesoma habari za wananchi wa Kata ya Kisesa wilayani Magu katika Mkoa wa Geita. Wananchi hao wanacho kituo cha afya, lakini dawa hawana. Wanalazimika kwenda kununua dawa hizo madukani. Swali linalokuja hapa ni kwa vipi tulifanikiwa kukamilisha mradi huo nusu?

Hivi kujenga majengo na kuyaita kituo cha afya halafu hakuna dawa kuna maana gani? Ama matofali hayo ndiyo yatageuzwa dawa za kutibu wananchi wetu kwa njia za mazingaombwe?

Hakuna jambo muhimu la kujali kama afya za wanajamii wetu. Kujengewa kituo cha afya maana yake ni pamoja na kupatiwa wahudumu, manesi, waganga na kuwepo kwa dawa zinazohitajika kwa wananchi wetu.

Ni jambo la fedheha kila mara tukijigamba kuanzisha mradi fulani lakini haukamiliki. Unajenga maghorofa ya hospitali halafu hakuna dawa, vitanda wala huduma muhimu kwa wagonjwa.

Nchi yetu iliwahi kuwa na mradi wa Mtwara Corridor. Ninakumbuka safari za meli za Malawi katika bandari ya Mbamba Bay wilayani Nyasa zilikuwa nyingi. Kutokana na ubovu wa barabara, Malawi wakatukimbia. Biashara ikawa ngumu. Mzunguko wa fedha ukakwama. Watu wakaishiwa fedha mifukoni.

Hadi leo mradi huo haujakamilika. Ni mwaka 2014 pekee ndipo nilimsikia Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akisema Benki ya Maendeleo ya Afrika imekubali kujenga barabara ya kiwango cha lami kuunganisha Mbinga na Mbamba Bay.

Pamoja na Serikali kutokuwa na mpango, lakini ukweli unabaki kuwa haijagundua fedha zitakazopatikana kama mradi huo endapo utakamilishwa. Sijui ni kitu gani tumekamilisha kwenye miradi yetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles