24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

HOMA YA TRUMP YAPAMBA MOTO

Na Markus Mpangala,

WOTE hawajui kitu gani kitafanywa na Rais mpya wa Marekani, Donald Trump. Jumuiya ya Ulaya imehoji mwelekeo wa siasa za Trump, lakini haijapata jibu. Umoja wa Afrika bado unamsoma Trump, kwa kuwa haujamwelewa.

Bara la Asia nao wanaendelea kumsoma Trump, hawajui atafanya nini. Hayo ni sehemu ya mambo yanayoendelea kote duniani kutokana na uongozi mpya wa Marekani.

Kifupi viongozi wengi duniani ni kama wamekumbwa na ugonjwa. Ni homa ya dunia iliyoletwa na Trump. Ndani ya Marekani homa hiyo imefikia nyuzi joto 90. Hivi sasa kiongozi huyo anafanya mambo yake kwa matamshi mazito na msimamo mkali. Katika makala haya yapo baadhi ya mambo ambayo yanasababisha homa hiyo kupamba moto duniani.

  1. Kufutwa Bima ya Afya

Mwanzoni mwa mwezi huu kabla ya kuapishwa, Trump aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook akisema: “Kama kuna Obamacare basi mimi ninayo Trump Don’t Care”.

Ilikuwa kauli ya dhihaka lakini ndiyo uwasilishaji wake aliokuja kuutekeleza baada ya kukabidhiwa madaraka. Obamacare ni mpango wa Bima ya Afya ambao uliwasaidia takribani wananchi milioni 20 nchini humo.

Hata hivyo, unalalamikiwa kuwa wa gharama kubwa kiuendeshaji. Huduma hiyo ilipitishwa na Bunge la nchi hiyo ikiwa ni moja ya sera za Rais Mstaafu Barack Obama, kuwasaidia watu masikini kupata huduma za afya.

Chini ya utawala wa Obama alikutana na upinzani mkali kutoka chama cha Republican kilijaribu mara tatu kupiga kura ya kufutwa mpango huo bila mafanikio kwa kuwa hawakuwa na mbadala.

  1. Kuwafuta kazi mabalozi wote

Rais huyo mpya ameendelea kufanya mabadiliko ya kiuongozi baada ya kuwatangazia wananchi kwamba mabalozi wa nchi yao walioko kwenye mataifa mbalimbali na mashirika ya kimataifa wanatakiwa kurejea nyumbani haraka.

  1. Vita dhidi ya vyombo vya habari

Tangu kuingia madarakani Januari 20, mwaka huu, Trump amelumbana na vyombo vya habari kwa namna mbili. Mosi; amelumbana navyo yeye moja kwa moja katika moja ya mkutano wake na vyombo hivyo ambapo aliwaita waandishi feki.

Pili; kwa sasa anawatumia wasaidizi wake ambao wameonyesha msimamo mkali wa kiongozi huyo katika malumbano hayo. Uhusiano wa vyombo vya habari na Trump ulikuwa mbaya tangu alipoanza mchakato wa kuwania urais ndani ya chama chake.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari, Sean Spicer, vyombo vya habari vinaandika habari mbaya dhidi ya Trump hususani juu ya idadi ndogo ya watu waliojitokeza siku ya kuapishwa kwake.

Naye mshauri wa Ikulu, Kellyanne Conway, ameunga mkono hatua hiyo na kudai Spicer alizungumza ukweli. Wawili hao wanadai Trump hatendewi haki na vyombo vya habari.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi, Reince Priebus pamoja na Rudy Giulliani, wamevishutumu vyombo vya habari kuwa vinakosea kulinganisha idadi ndogo ya watu waliohudhuria wakati wa kuapishwa Trump na kipindi cha kuapishwa Obama mwaka 2009, wakidai kuwa wingi au uchache wa watu si jambo lenye umuhimu.

  1. Mkataba mpya wa NAFTA

Serikali ya Trump imetangaza kuwa itasaini upya mkataba wa kibiashara kwa nchi za Amerika Kaskazini. Mkataba wa NAFTA (North America Free Trade Agreement), unazihusisha pia nchi za Canada na Mexico, Trump amebainisha kuwa anazingatia zaidi masuala mawili pekee kati ya mengi; suala la uhamiaji na ulinzi mipakani.

Anataka mkataba huo uwe na manufaa kwa Marekani badala ya kubeba mzigo wa wengine: Tutakutana na Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau na vile vile Rais wa Mexico, Pena Enrique Nieto. Tutasaini mkataba katika masuala hayo,” ilisema taarifa ya Trump.

  1. Kuhamisha ubalozi Israel

Uhusiano wa Marekani na Israel una historia ndefu. Rais mpya ameonekana kuwa na mtazamo mpya na tayari kuna madai ya kuhamisha ubalozi wa Marekani nchini Israel kutoka mjini Tel Aviv kwenda mji wa Jerusalem.

Suala hilo ni miongoni mwa mambo yaliyozua mjadala mkali miongoni mwa mataifa ya bara la Asia yakipinga wazi mpango huo.

Kiongozi wa Mamlaka ya Palestina, Mahmood Abbas na Mfalme wa Jordan, Abdullah II wanapinga mpango huo. Wanasema unaweza kusababisha machafuko mapya katika eneo la Mashariki ya Kati.

  1. Ziara ya kwanza CIA

Tangu kuingia madarakani amefanya ziara ya kwanza katika Ofisi za Makao Makuu ya Shirika la Kijasusi nchini Marekani, CIA. Pamoja na mambo mengine, Trump ametangaza kumteua Mike Pompeo kuwa Mkurugenzi wa CIA. Kabla ya uteuzi huo, Pompeo alikuwa mbunge wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Kansas tangu mwaka 2011 hadi 2017.

  1. Kufuta sheria ya utoaji mimba na misaada

Trump ametangaza kufuta mpango wa kutoa misaada kwa asasi zinazojihusisha na harakati za kuunga mkono utoaji mimba. Trump amefuata nyayo za Ronald Reagan kupiga marufuku utoaji mimba uliopo chini ya sheria ya ‘Gag rule’ kama sehemu ya sera ya MCP (The Mexico City Policy) iliyokuwa ikipiga marufuku kufadhili utoaji mimba duniani mwaka 1984.

 Ilianza kutumika katika utawala wa Reagan mwaka 1984 na baadaye George W. Bush ambao walisababisha kiwango cha utoaji mimba kuwa kikubwa nchini Marekani. Tangu mwaka 1973 chini ya Sheria ya Helms Amendment, ni makosa kutumia fedha za Serikali kushughulikia masuala ya utoaji mimba popote duniani. Hatua hiyo inatajwa kuziathiri asasi mbalimbali na kusababisha ukata mkubwa miongoni mwake.

  1. Baraza la mawaziri ni dogo

Serikali ya Trump inaundwa na baraza la mawaziri dogo mno wapo 21 tu. Uteuzi wa mawaziri ulikamilika Januari 12, mwaka huu.

  1. Wateule kubanwa bungeni

Licha ya kuteua zaidi ya maofisa 4,000 katika nafasi mbalimbali, Trump anakabiliwa na mtihani wa kukubaliwa wateule wake 1,100 wanaotakiwa kuidhinishwa na Bunge la Seneti. Kati ya wateule wake 450 wanatajwa kutokuwa na sifa zinazotakiwa na Bunge la Seneti.

  1. Kufutwa haki za mashoga

Katika utawala wa Rais Mstaafu Barack Obama, alifanikiwa kupitisha sheria ya kuwatambua na kuwapa haki watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja maarufu kama mashoga na wasagaji.

  1. Kujitoa mkataba wa TPP

Nilimsikiliza Rais wa Mexico, Pena Nieto, alipozungumza na Televisheni ya Africa News Jumanne wiki hii kuhusu mkataba wa TPP (Trans-Pacific Partnership).

Nieto alikuwa akizungumza huku amekunja sura na kuonyesha ishara kuwa rais huyo ameumizwa na uamuzi wa Serikali ya Trump kujitoa kwenye mkataba wa kibiashara wa kanda ya Pasifiki unaojumuisha nchi 12 za Mexico, Canada, Peru, Vietnam, Malaysia, Brunei, Japan, New Zealand, Singapore. Licha ya uamuzi huo, mataifa mengine yamesema yatasonga mbele.

  1. Aipa shavu Misri

Trump amezungumza na Rais wa Misri, Abdel Fattah Al-Sisi kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili ikiwamo kupambana na ugaidi. Al Sisi ni kiongozi pekee kutoka Afrika ambaye amepewa nafasi ya kwanza kuzungumza na Trump. Haijulikani itakuwaje kwa wengine.

  1. Kufuta ajira serikalini

Kiongozi huyo ametoa mwongozo wa kufutwa ajira zote serikalini isipokuwa kwa upande wa ajira za jeshini pekee.

  1. Netanyahu kumtembelea Trump

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ndiye kiongozi wa kwanza kualikwa na Trump tangu alipoingia madarakani rasmi Januari 20.

Kwa mujibu wa taarifa ya Televisheni ya Africa News, Israel na Marekani ni washirika wa muda mrefu, inatarajiwa watazungumzia suala la nyuklia ya Iran hali ambayo inasubiriwa kwa hamu kujua hatima ya mkataba wa nyuklia. Trump wakati akiwa kwenye kampeni, alikosoa mkataba huo na kudai angeufuta mara moja.

  1. Afuta visa

Jumatano wiki hii, Trump alisaini hati ya kusitisha visa siku 30 kwa nchi za Sudan, Iran, Iraq, Libya, Somalia, Syria na Yemen. Hatua hiyo inatajwa kutekeleza sera zake za kuwapiga marufuku Waislamu kuingia nchini Marekani pamoja na kuanzisha daftari maalumu la kuwasajili.

  1. Malumbano ya Rais Nieto na Trump

Suala la ujenzi wa ukuta mpakani mwa Mexico na Marekani limechukua sura mpya. Rais wa Mexico anapingana na mpango wa Trump na kudai anaingilia haki za taifa lake.

Akizungumzia ujenzi wa ukuta kwenye mahojiano na Televisheni ya ABC nchini Marekani, Trump alisema: “Ujenzi unatarajiwa kuanza hivi karibuni haraka iwezekanavyo,… utajengwa tu. Naweza kusema kwa mwezi mmoja, … ndiyo! Ndani ya mwezi mmoja. Mipango inaanza karibuni. Yote yatafanyika kutokana na kile kitakachotokea Mexico. Tutaanza kwa makubaliano muhimu karibuni na yatafanyika kwa taratibu maalumu. Mexico watalipia gharama za ujenzi. Zitakuwa taratibu ngumu kidogo.”

Kwa upande wake, Rais Nieto alijibu mapigo ya kauli hiyo kwa kusema: “Mexico haiamini katika ujenzi wa ukuta. Mara nyingi nimesema hayo, narudia tena, Mexico haitalipa gharama zozote za ujenzi wa ukuta. Tunaomba kuheshimiwa kama taifa huru. Mexico imekuwa rafiki wa watu wa Marekani na ina matumaini kutakuwa na makubaliano kati ya Serikali hizi. Makubaliano ambayo yatainufaisha Mexico na wananchi wake.”

Hadi sasa marais hao wamefuta mkutano wao waliopanga kuufanya wiki ijayo. Taarifa ya kufutwa ilianza kutolewa na Rais Nieto ambaye alibainisha kuwa kutokana na uamuzi wa kujenga ukuta huo haoni sababu za kutembelea Washington. Naye Trump alijibu mapigo ya taarifa hiyo kwa kubainisha hakuna sababu za kukutana kwao tena.

  1. Maofisa wa Ikulu kuachia ngazi

Saa chache tangu Bunge la Kongresi kuidhinisha jina la mteule wa Rais Trump katika wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson, ameshuhudia maofisa kadhaa wa Ikulu wakiachia ngazi hali ambayo inatajwa kuathiri mwelekeo wa sera za nje huku waziri huyo akikosa msaidizi.

Waliojiuzulu ni Patrick Kennedy (aliyedumu kwa miaka tisa kama msaidizi wa waziri), Joyce Anne Barr (aliyekuwa ofisa utawala wa wizara hiyo), Michael Bond (mshauri wa mambo ya nje wa wizara), Balozi Gentry O. Smith (mkurugenzi wa wizara katika mipango ya nje).

Makala haya yametayarishwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles