24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TUMBAKU MKOMBOZI VIWANDA MOROGORO

Na Mwandishi Wetu,

MANISPAA ya Morogoro imepanuka kieneo na idadi ya watu kutokana na mji huo kukaa kimkakati kwa usafiri na mwenendo wake wa kiuchumi na kuwa mwenyeji wa vyuo vikuu  vya maana visivyopungua vinne.

Kile kinachoonekana kuwa  ni bahati ya mtende  ni kiwanda kikubwa cha tumbaku na sigara kinajengwa katika Manispaa hiyo na kuajiri wafanyakazi zaidi ya 2,500, ambao watakuwa rasilimali kubwa kwa uchumi wa hapo na taifa kwa kulipa kodi na kuongeza thamani ya zao la tumbaku.

Kiwanda hicho ni neema kiuchumi, lakini kiafya ni kibaya, lakini kama methali isemavyo Baniani mbaya kiatu chake dawa.

Kiwanda kipya cha kutengeneza sigara cha Philip Morris Tanzania (PMT), Kampuni tanzu ya Phillip Morris International (PMI) ya Marekani, ambacho kitakuwa kikubwa kuliko vyote katika Afrika Mashariki, kinajengwa Mkambalani, katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Shanif Mansoor Hiran, alisema kwenye shughuli ya Mbio za Mwenge wa Uhuru na kiongozi wa Mbio hizo, Amour Hamad Amour, aliweka “jiwe la msingi” la ujenzi wa kiwanda hicho.

Hiran alisema PMI inazalisha na kuuza bidhaa za tumbaku na hasa sigara aina ya Marlboro na Camel na chapa nyingine bora 15 duniani kote na uwekezaji huo wa mkoani Morogoro unategemea kugharimu Sh bilioni 60. Miongoni mwa chapa hizo bora, sita ni za PMI na zimekuwa zikiuzwa katika nchi zaidi ya 180 duniani.

Miezi  mitatu iliyopita Mohamed Dewji, mfanyabiashara maarufu nchini, alifichua ujaji  wa uwekezaji huo mkubwa ambao kampuni yake ina hisa na kutegemea kujenga kingine cha sabuni ambacho kitakuwa kikubwa Afrika Mashariki.

“Sababu za msingi na maamuzi haya ni kutokana na mazingira mazuri ya kibiashara, amani na utulivu, kiwango cha ukuaji wa uchumi na sera ya viwanda hapa nchini,” alisema Dewji, kauli ambayo imerudiwa na Hiran.

Kimsingi ujenzi wa kiwanda hicho upo katika hatua za mwisho na matarajio yake ni kuanza uzalishaji wa sigara mwezi ujao. Wadadisi wa mambo wanasema Morogoro imepata bahati kubwa kupata uwekezaji huo, wakati duniani uzalishaji wa tumbaku unapigwa vita kwa madai ya afya za watumiaji kuwa hatarini kwa magonjwa kutokana na matumizi ya nicotine, iliyomo kwenye tumbaku, ni vita ya zaidi ya karne 2 bila ushindi.

Hiran anasisitiza umuhimu wa kiuchumi wa kiwanda hicho kwa kusema kampuni yao imeamua kuunga mkono serikali ambapo mbali na kukuza uchumi wa nchi utokanao na viwanda, pia kiwanda hiki kitatoa fursa ya ajira 2,500 kwa vijana, wengi wakiwa wakazi wa Morogoro.

Aliongezea kusema kuwa, ujenzi wa kiwanda hicho ni moja ya juhudi za kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli na kwamba sigara zitakazotengenezwa zitakuwa na ubora wa kimataifa.

Hiran anasema kiwanda hicho kitaongeza mapato yatokanayo na kodi kwa serikali kupitia kodi mbalimbali, maongezo ya thamani kwa zao la tumbaku; pia kitatoa ajira ya moja kwa moka katika nyanja za uzalishaji na usambazaji wa bidhaa zitakazozalishwa na kuchangia huduma za kijamii kwenye miradi ya maendeleo, elimu, afya na maji hali ambayo itachochea wakulima wa zao la tumbaku kuongeza uzalishaji, hususan wa Mkoa wa Tabora na Ruvuma inakolimwa kwa wingi.

Kiongozi wa Mwenge alisema kiwanda hicho kitatoa ajira kwa vijana wengi na pia kukuza uchumi kutokana na mapato yatakayotokana na kodi, itakayochangia kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Alitaka kilindwe dhidi ya hujuma yoyote.

Wananchi wa Mkoa wa Morogoro walihakikishiwa upendeleo wa ajira  pale ujenzi utakapokamilika kwa kupewa kipaumbele na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa kiwanda hicho, Evans Mrema.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Stephen Kebwe, anawaonya wasioendeleza viwanda Morogoro wafanye juhudi kuvifufua viwanda hivyo au wavirejeshe serikalini kama inavyotakiwa kama wameshindwa kuviendesha.

Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wawekezaji katika viwanda walioshindwa kuviendeleza, kuanza kazi mara moja, vinginevyo serikali itavichukua na kuwapa wenye uwezo.

Dk. Kebwe alisema serikali iliwakabidhi viwanda hivyo kutokana na wao kusema watamudu kuviendeleza kwa lengo lililokusudiwa ili kuongeza ajira kwa wananchi, mapato ya serikali na wenye viwanda kupata faida na uchumi wa nchi kukua.

Alisema hayo akiwa katika kiwanda cha Moproco cha mafuta ya kula, ambapo Mkuu huyo wa Mkoa alikuta shughuli za ukarabati wa mitambo na mashine ya kiwanda hicho ikiendelea kufanyika kwa ajili ya kuanza uzalishaji wa kukamua mafuta ya kula ya alizeti.

Naye Mkurugenzi wa kiwanda hicho na makampuni ya Abood, Talal Abood, alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa uzalishaji wa hatua ya awali umepangwa kuanza mwishoni mwa Agosti, mwaka huu, itakayotoa ajira wa watu kati ya 80 hadi 100.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles