24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

TIMU YA TANZANIA MAKINIKIA SIRI NZITO

Waziri wa Sheria na Katiba, profesa Palamagamba kabudi (aliyenyoosha mkono), akiwa na ujumbe wa maofisa wa Kampuni ya Barrick baada ya kuwasili Dar es Salaam jana kwa ajili ya mazungumzo na Kamati maalumu ya Tanzania iliyoudwa na Rais Dk. John Magufuli.

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

KAMATI Maalumu ya majadiliano iliyoundwa na Rais Dk. John Magufuli na wawakilishi kutoka Kampuni ya Barrick Gold Corporation wameanza majadiliano rasmi jijini Dar es Salaam.

Kuanza kwa majadiliano hayo kunatokana na biashara ya madini yanayochimbwa na migodi ya kampuni hiyo hapa nchini.

Taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa kamati hiyo kwa upande wa Tanzania inaongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, huku upande wa Barrick Gold Corporation inaongozwa na Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa kampuni hiyo, Richard Williams.

Bila kuwekwa wazi majina ya Watanzania waliomo katika kamati hiyo, tayari wameanza mazungumzo rasmi yaliyotanguliwa na yale ya awali ambayo hayakuwa rasmi.

Taarifa iliyotumwa na Msigwa, imeeleza kuwa pande zote mbili zimeahidi matokeo chanya kwa Tanzania na wafanyabiashara hao.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa majadiliano hayo Mwenyekiti wa upande wa Tanzania, Profesa Kabudi alisema kamati yake imejipanga vizuri kujadiliana na Barrick Gold Corporation juu ya madai ya Tanzania katika biashara ya madini ya kampuni hiyo hapa nchini na itahakikisha inasimamia masilahi ya Tanzania ipasavyo.

“Leo (jana) tunaanza mazungumzo rasmi maana mazungumzo yasiyokuwa rasmi yalikwisha anza kwa Rais Dk. John Magufuli kukutana na kukubaliana kuanza kwa mazungumzo.

“Baada ya hapo utekelezaji wa agizo hilo la Mheshimiwa Rais ulianza na watu ni lazima wafahamu kwamba majadiliano sio tukio, ni mchakato wa muda. Hii si mara yangu wa kwanza kukutana naye. Kwani tulishakutana hapa Dar es Salaam, ni wazi kabisa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi huru na inasimamia rasilimali zake, hasa madini ambayo yanatakiwa kunufaisha Watanzania wote.

“Ninawaomba Watanzania wote kuyatakia heri mazungumzo haya, maadamu ndugu zetu wamekuja ni vema mazungumzo haya tukayapa nafasi na wakati ukifika tutajua nini kimeamuliwa kwa pande zote mbili,” alisema Prof. Kabudi.

Kwa upande wake, kiongozi wa Barrick, Williams, ameshukuru kuwapo kwa majadiliano hayo na alisema Kampuni ya Barrick imeyapokea madai ya Tanzania kwa mtazamo chanya na ipo tayari kujadiliana na kufikia makubaliano yenye masilahi kwa pande zote mbili.

Licha ya timu ya wajumbe kutoka Barrick ikiwekwa hadharani kwa upande wa Tanzania, bado kumekuwa na giza nene, kwamba hadi sasa wajumbe wake katika jipo hilo hawajulikani.

Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA ilimtafuta Msigwa, ambaye alisema kwa sasa timu hiyo itaongozwa na Prof. Kabudi kama ilivyoelezwa, ambaye ataongoza timu ya wajumbe kutoka upande wa Tanzania kwenye mazungumzo hayo.

“Watanzania wasiwe na hofu na tunaomba waiamini Serikali katika hili chini ya Profesa Kabudi, hakuna kitakachoharibika na hata wanaotaka wajumbe wa kamati hiyo wawafahamu wavute subira na wajenge imani kwa Serikali yao,” alisema Msigwa.

KUUNDWA KWA KAMATI

Rais Magufuli aliunda kamati mbili kuchunguza mchanga wa madini, moja chini ya Mwenyekiti wake Profesa Abdulkarim Mruma.

Kamati hiyo ilikuwa na kazi ya kuchunguza aina na kiwango cha madini yaliyopo ndani ya mchanga wa madini unaosafirishwa nje.

Pia ilielezwa kuwa chimbuko la utafiti huo ni kutojulikana kwa kiwango cha makinikia na mikataba yake, kufanya uchunguzi wa makinikia kwenye bandari ya Dar es Salaam, migodini, kufanya uchunguzi wa kimaabara ili kujua thamani na aina ya madini yaliyopo kwenye makinikia, kuchunguza uwezo wa scanner zilizopo bandarini na kuchunguza uwezo wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) katika kusimamia makinikia hayo.

Matokeo ya uchunguzi, kamati ilibaini uwapo wa dhahabu kwa kiasi kikubwa cha dhahabu kwenye makinikia, katika makontena 277 yaliyozuiliwa kulikuwa na tani saba za dhahabu.

Makontena hayo yalikuwa na dhahabu yenye thamani zaidi ya Sh trilioni 1.47 sambamba na kubaini uwapo wa madini ya shaba, silver, surpher na chuma.

Kamati ilipendekeza baadhi ya watendaji wa Serikali kuchukuliwa hatua kutokana na uzembe huo na Rais Magufuli alifanya hivyo ikiwa ni pamoja na watendaji wakiwamo wa TMAA kutumbuliwa.

 JINSI BARRICK WALIVYOTUA

Baada ya Rais Magufuli kupokea ripoti hizo mbili, Juni 14 mwaka huu, Mwenyekiti wa mgodi wa Barrik Gold Corporation ambaye ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited, Profesa John Thornton alitua nchini kwa ndege binafsi.

Katika mazungumzo hayo, pia alihudhuria Balozi wa Canada  hapa nchini, Ian Myles na Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Kabudi.

Katika mazungumzo hayo Profesa Thornton alisema wapo tayari kufanya mazungumzo yenye masilahi kwa pande zote mbili, huku Rais Magufuli akiwakaribisha.

Hata hivyo, mazungumzo hayo yalionekana kuchelewa ambapo hivi karibuni akiwa mkoani Singida kwenye ziara ya kikazi, Rais Magufuli alisisitiza kuwa kampuni hiyo ifanye haraka kufanya mazungumzo na kama wakishindwa Serikali itakuwa tayari kuwapa Watanzania wazawa ili wachimbe na kuyauza madini hayo hapa nchini.

“Ninawaambia tena kama wakichelewa (Barrick), ni bora kuwapa Watanzania ambao watakuwa na uwezo wachimbe madini na kuyauza ambapo watalipa kodi kwa Serikali na hela itapatikana.

“Na badala ya madini haya kuuzwa nje, tutajenga kiwanda hapa hapa na kuyauza. Kama watachelewa kwa ajili ya mazungumzo nasema tutawapa Watanzania kwani tumeibiwa sana katika madini yetu,” alisema Rais Magufuli.

Hatua ya Serikali kuzuia uchimbaji wa madini na usafirishaji nje ya nchi, imeonekana kuitikisa kampuni hiyo na kulazimika kupunguza wafanyakazi katika migodi yake ya hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles