31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

CHADEMA: HALI YA UCHUMI TETE

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, hali ya uchumi imezidi kuwa tete.

Kutokana na hali hiyo, mauzo na manunuzi ya nje, mikopo sekta binafsi yameporomoka, huku deni la taifa likipaa kuliko kipindi chochote.

Pia amesema Serikali imeshindwa kusimamia mfumko wa bei ya chakula kwa sababu haitambui umuhimu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Kutokana na hilo, amewataka wachumi kufanya uchunguzi wa kina na kuacha kuingia kwenye mkumbo wa kupika takwimu za uchumi ili kupata umashuhuri wa kisiasa.

Mbowe alitoa kauli hiyo jana, wakati akitoa maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho kuhusu kuporomoka kwa uchumi wa taifa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, iliyokutana kwa siku mbili, Dar es Salaam juzi.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema hivi sasa biashara zinafungwa kuliko kipindi chochote, lakini bado Serikali imekuwa ikisema uchumi unakua.

Alisema kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu mwenendo wa uchumi kwa kipindi cha Mei, 2015 kiasi cha akiba ya chakula kwenye ghala la taifa kilifikia tani 406,846 ikilinganishwa na tani 74,826 Mei, mwaka huu.

“Bei za jumla kwa vyakula muhimu kama mahindi, Mei mwaka 2015 ilikuwa Sh 47,163 kwa gunia, wakati mwaka huu ni Sh 90,149.9 sawa na asilimia 92, bei ya mchele kwa gunia ilikuwa Sh 162,701 wakati mwaka huu, ni Sh 176,330.

“Mazao mengine yote ya chakula, ikiwamo maharage, viazi na sukari nayo yamepanda bei kwa wastani wa asilimia kati ya 40 na 60.

“Sekta ya kilimo imekua kwa asilimia 1.7 mwaka 2016/17, kiwango ambacho ni cha chini kupata kutokea zaidi ya miongo mitatu.

“Wakati mataifa yote duniani yanasaidia wakulima kuongeza tija katika kilimo kwa kuwasaidia ruzuku ya mbolea, Tanzania ambayo asilimia 75 wanategemea kilimo, mwaka 2015 ilikuwa Sh bilioni 78, wakati 2016/17 ruzuku ilikuwa Sh bilioni 10.

“Tume ya Maji iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria mwaka 2015 kwa lengo la kuhakikisha tunaongeza kilimo cha umwagiliaji katika bajeti ya mwaka 2016/17, ilipata sifuri katika bajeti ya maendeleo,” alisema.

 HALI YA UKATA

Alisema wakati bei za bidhaa zikiwa juu sasa kuliko mwaka 2015, hali ya ujazo wa fedha, imekuwa kinyume chake na hivyo kuathiri biashara, uzalishaji na thamani ya mali.

“Mzunguko wa fedha kwa maana ya kiasi cha fedha katika matumizi kwa mwaka, inaonyesha Mei 2015, kiliongezeka kwa asilimia 15.2, wakati Mei 2017 kilikuwa na ongezeko la hasi kwa asilimia 3. Hiki ni kielelezo cha usimamizi hafifu wa uchumi na ndio msingi wa ukata unaoendelea,” alisema Mbowe.

Alisema kwa sababu ya mdodoro wa biashara, wafanyabiashara wanashindwa kulipa mikopo na hivyo kuongeza presha kwenye kasi ya mikopo isiyolipika.

Mbowe alisema ukata umesababisha kushuka kwa thamani kama ya ardhi, nyumba na kwamba viwanja ambavyo viliuzwa Sh milioni 100, hivi sasa ni Sh milioni 50.

“Gari au mashine ambayo mwaka 2015 ungeuza Sh milioni 50, leo huwezi kupata nusu yake,” alisema.

MIKOPO KUPUNGUA

Alisema sekta binafsi kama injini ya uchumi, inategemea zaidi mikopo kugharamia uwekezaji, hata hivyo takwimu za BoT kuhusu mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi kwa ulinganisho wa mwaka 2015 na 2017, ni kielelezo uchumi umevurugwa.

“Ndani ya miaka miwili kiwango cha mikopo isiyolipika kilivuka wastani wa asilimia 5 na kufikia 8. Benki kadhaa zilifungwa kutokana na tatizo la mikopo isiyolipika na zilizobaki kuyumba vibaya kutokana na mdodoro wa biashara uliosababisha ongezeko la mikopo isiyolipika,” alisema.

 MANUNUZI NJE

Alisema manunuzi ya bidhaa nje ya nchi yalifikia Dola za Marekani milioni 13.305.2 mwisho wa Mei, 2015, ikilinganishwa na manunuzi ya Dola milioni 9738.8 Mei, mwaka huu.

 MAUZO YA BIDHAA NJE

Mbowe alisema jumla ya bidhaa na huduma nje ni kigezo muhimu katika kupima uchumi unaokua au kusinyaa.

“Kipindi cha Mei 2017, mauzo ya jumla yalikuwa Dola milioni 8,774.9, ikilinganishwa na mauzo ya Dola milioni 9,454.5 kipindi kama hicho mwaka 2015.

“Hivyo biashara ya nje kwa ujumla imeanguka kwa takribani Sh trilioni 10,” alisema.

 DENI LA NDANI

Alisema pamoja na kwamba deni la taifa, limeongezeka kwa zaidi ya Sh trilioni 11.5, lakini Serikali imeendelea kudai kuwa deni ni himilivu, badala ya kuelekeza nguvu na mikakati mikubwa kwenye uwekezaji.

Kutokana na hilo, alisema Serikali imekuwa ikipambana na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na kwamba hivi sasa uhusiano baina ya sekta binafsi uko shakani zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

“‘Investors confidence’ inaondoka kwa kasi, ni vigumu sana hata kwa wawekezaji wa ndani kuchukua ‘risk’ kuwekeza katika nchi isiyoheshimu demokrasia, Katiba utawala wa sheria, kanuni, mikataba na hata utu. Tunakimbiwa na tutakimbiwa zaidi huku tukipongeza kuwa nchi inanyooshwa,” alisema.

Alisema bila kuongeza uzalishaji, deni hilo litaielemea Serikali kama hadi sasa halijaielemea.

“Kwa sasa tunatumia asilimia 80 ya makusanyo yote ya kodi kulipa mishahara na deni la taifa tu. Tunabakia na asilimia kama 20 ya makusanyo kuendesha Serikali na kutekeleza miradi ya maendeleo. Hali hii haikubaliki na ni muujiza kutoka kwenye umasikini,” alisema Mbowe.

 MAKINIKIA 

Mbowe alisema Rais Dk. John Magufuli aliunda kamati mbili na kwamba taarifa za kamati hizo zilizua sintofahamu kubwa ya uchumi na uwekezaji katika taifa.

Alisema kwa lengo jema la kuwa wawazi katika sakala hilo, ni vyema Serikali ikaweka wazi taarifa hizo kwa ujumla wake na si vipande vipande.

“Ni jambo jema kulinda rasilimali za nchi, hata hivyo ulindaji huo hauhitaji kuwa wa pupa na papara. Unahitaji kufanywa kwa umakini na tahadhari kubwa ili faida yake kwa nchi iweze kuwa na uhakika.

“Ripoti hizi zimeweka rekodi za kidunia za uzalishaji madini, hususani dhahabu na hasa baada ya TRA kuiandikia Acacia madai ya kodi yanayofikia kiwango cha Sh trilioni 425.

“Taarifa hizi zimesambazwa katika vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa sambamba na mitandao kadhaa ya kimataifa, yakiwemo majarida na magazeti makubwa duniani.

“Kutangazwa huku ni kwa misingi ya kejeli zaidi, ikihoji kuna uwezekano gani wa kampuni kudaiwa kodi ambayo ni zaidi ya mara 10 ya bajeti ya taifa husika.

“Serikali isikae kimya, kukaa kimya ni kukubali kebehi hizi. Kama ilivyokuwa na ujasiri wa kutangazia taifa ripoti zilipotoka, iwe tayari kuitangazia hata dunia kwa kuweka hadharani hiyo siri yenye sifa ya kuingia kwenye ‘Guinness Book of Records’.

“Unaweza kufikiria unarekebisha kumbe unaharibu, haya mambo yanahitaji umakini, uvumilivu na haihitaji papara kwa sababu kilichofanywa na rais ni papara, wabunge wake papara na wananchi wake wakalishwa papara.

“Jambo hili lifanywe lisiathiri misingi ya uchumi ila litajenga uchumi wa taifa na kumkataa mwizi ni heshima ya taifa, ila kumuua mwizi bila kuonyesha umemuua kwa sababu zipi ni tatizo,” alisema mbunge huyo wa Hai.

 AMKOSOA JPM 

Mbowe, alisema Serikali haiwezi kujenga viwanda peke yake bila kuihuisha sekta binafsi ambayo ndiyo mdau mkuu katika uwekezaji.

Alipinga kusudio la Rais Magufuli kuwanyang’anya wawekezaji viwanda walivyobinafsishwa kwa madai, Serikali ilitakiwa kutafuta chanzo cha kufungwa kwa viwanda hivyo kabla ya kufikia uamuzi wake.

Alitaja sababu zilizofanya viwanda hivyo kushindwa kufanya kazi, kuwa ni pamoja na kutopatiwa ruzuku na Serikali, teknolojia ya zamani ya viwanda hivyo na wakati vinajengwa kulikuwa na mfumo hodhi wa soko.

Alisema sekta binafsi ndiyo inayotegemewa kukuza taifa, lakini rais amekuwa akiichukia.

“Hakuna mfanyabiashara duniani ambaye atapewa kitega uchumi kinachozalisha halafu akakifunga, hayupo. Rais Magufuli hana mapenzi na sekta binasi kwa kuwa anaamini kila mtu kwenye sekta hii ni dili,”alisema.

Alimtaka Rais Magufuli kuelewa yeye ni kiongozi mmoja ambaye anawaongoza Watanzania milioni 40, hivyo uamuzi wake unawakwaza wengi na kutesa Watanzania.

“Hatuchukii au hatupingi mapambano ya kutafuta haki na rasilimali zetu, mambo haya yanahitaji kutumia busara na umakini, anakotupeleka siko. Kwa sasa si mwekezaji wa nje tu, hata ndani huwezi kutoa Sh bilioni 5 ukawekeza halafu ukaja ukasema bomoa, utakuwa chizi.

“Tukiendelea kuficha ugonjwa kifo kitatuumbua. Hali yetu ni mbaya. Huhitaji uprofesa wa chuo kikuu kujua,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Uwasilishaji uliofanywa na Mh. Mbowe juu ya taarifa baada ya kikao cha CHADEMA una maswali mengi kuliko majibu.
    1. Chakula kuwa na bei ya juu, kama bidhaa zozote zile, hutegemea kiwango cha mahitaji na kiwango cha ugavi. Mahitaji yakiwa makubwa kuliko ugavi, bila shaka bei itapanda.
    Aidha ukosefu wa chakula ni suala mtambuka. Ama wazalishaji hawakufanya walichopaswa kufanya (walizalisha kidogo au walizalsha wakauza chote) au mazingira (hali ya hewa /wadudu / majanga)yaliwaathiri au watu hawataki kufanya kazi za kilimo, nk, nk.
    Pamoja na hayo, bei inapopanda,naamini mkulima hunufaika na mfanya biashara hunufaika ingawa mlaji huathirika!
    2.Kuhusu ukata, wote tu mashahidi kwamba pesa iliyokuwa kwenye mzunguko ilikuwa na makandokando mengi. Zilikuwa sio pesa zenye kufuata kanuni za kiuchumi. Zilikuwa pesa za kutakatisha. Kwa mkutadha huo, ujazo wake huwezi kuuchukulia kuwa ni mzunguko wa kiuchumi!
    3 Kuhusu mabenki kushindwa kutoa mikopo ni kutokana na athari ya kushindwa kufuata kanuni za mikopo. Kama wangefuata kanuni za mikopo, bila shaka dhamana ya mikopo hiyo ingeweza kusaidia kurejesha mikopo chechefu na hivyo mabenki kuhimili mikikimikiki iliyopo.
    4. Kuhusu makinikia, ni kweli yanaweza yakawa na athari lakini ili kurejesha heshima ya taifa kuhusu raslimali zake zinazopotea, lazima kufanya maamuzi magumu.
    5. Kuhusu viwanda vilivyobinafsishwa, ni jukumu la wahusika kutoa maelezo kitambo juu ya ni kwa nini hawakuviendeleza kiasi cha baadhi yao kuhamisha mashine kwenda nje ya nchi au kubadilisha makusudio yake.
    Juu ya hayo naamini, kama waziri wa biashara na viwanda alivyowahi kusema, serikali kazi yake ni kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje na sio kujenga viwanda.
    Tujitafakari!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles