24.8 C
Dar es Salaam
Thursday, September 21, 2023

Contact us: [email protected]

SHERIA MPYA MADINI YAANZA KAZI KWA KISHINDO

Mgodi wa dhahabu Geita

Na SHERMARX NGAHEMERA,

SHERIA ya Madini ya mwaka 2010 imefanyiwa mabadiliko makubwa, hivyo kuanzia sasa mambo ya utoaji wa Leseni za Madini umesimamishwa hadi itakapoundwa Tume au Kamisheni ya Madini kama sheria inavyotaka.

Sheria ya Madini imefanyiwa mabadiliko makubwa na mabadiliko ya Sheria  2017 (Sheria Iliyoandikishwa  na Mengineyo ya Mwaka 2017 ( Written Law Miscellaneous Ammenfments  2017), iliyopitishwa na kikao cha Bajeti na imesheheni makatazo ya mambo mengi ili kubana utoroshaji wa mapato ya Serikali.

Sheria hiyo imefuta Wakala wa Madini iliyojulikana kama Tanzania Minerals Audit Agency (TMAA) na ofisi nane za kushughulikia madini nchini.

Kwa maelezo ya Profesa James Mdoe, Katibu Mkuu Wizara ya  Nishati na Madini, amewaambia waandishi wa habari kuwa wale wanaotaka kupeleka madini nje wanatakiwa kulipa ‘Clearing Fee’ ya  kiwango cha asilimia moja ya thamani ya madini hayo, ambayo yamefanyiwa ukaguzi na kuthaminishwa  na Ofisi ya Kamishina wa Madini kwa muda huo wa mpito hadi Kamisheni ya Madini itakapoanza kazi rasmi baada ya kuundwa.

Aliainisha kuwa, hayo ni pamoja na majukumu yote ya kazi iliyokuwa inafanywa na TMAA kwa muda itafanywa  na ofisi hiyo, ikiwamo makusanyo ya mrabaha kwa madini ya ujenzi na ya viwanda, uthibitishaji wa  vocha za malipo  na usalama wa madini migodini.

Majukumu mengine yaliyoathirika ni usimamizi wa migodi kwa kupitia mahitaji ya wazalishaji wote wa madini  na miradi yao, ukaguzi katika sehemu za kutokea na kusafirisha mizigo, ikiwamo viwanja vya ndege na mipaka  ya nchi pamoja na bandari kuzuia upoteaji madini kwenda nje.

Profesa Mdoe alisema kuwa, mrabaha kuhusu madini mbalimbali umeongezeka, ambapo madini ya metali kama dhahabu, shaba  na fedha yameongezeka kutoka kiwango cha awali cha asilimia 4 hadi asilimia 6. Wakati huohuo madini ya vito na ya thamani kama almasi, yakuti, ganeti na tanzanite  yameongezeka mrabaha kuwa wa asilimia 6 kutoka za awali asilimia 5.

Wachimbaji wadogo kulipa kodi

Alisema sheria mpya inataka kila mtu au taasisi katika mnyororo wa thamani atailipa serikali kwa mapato na huduma mbalimbali ambapo tozo ya asilimia 5 kwa mara ya kwanza itakusanywa na madalali  na wafanyabiashara wakubwa (dealers) kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo kama kodi ya makusanyo (withholding tax)  na kuwasilishwa kwa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA)

Amewataka wadau wote kushirikiana na wafanyakazi waliopo, kwani wanafanya majukumu yao kama ilivyoainishwa na Wizara na katika misingi ya sheria kwa mafanikio makubwa kukusanya maduhuli yote ya serikali katika wakati huu wa mpito.

Aliwahakikishia wafanyakazi ambao hawakuhusika na mtafaruku wa biashara ya madini kuwa wataendelea na kazi kama kawaida na kupata stahiki zao za malipo kwa mpangilio mpya hadi hapo mabadiliko yatakapofanyika kikamilifu kwa sheria mpya.

Wafanyakazi hao wameambiwa  wataendelea kutoa mwendelezo wa leseni za wachimbaji wadogo wadogo, kwa vile maofisa wote wa TMAA na wale wa ofisi za kanda wako chini ya kanda, wakati utambulisho na vifaa vya kazi vyote vitatolewa na Kamishina wa Madini, vikiwamo  mihuri, lakiri na risiti, vikionesha ofisi hiyo ya Kamishina wa Madini.

Mabadiliko haya ni matokeo ya ripoti mbili  zilizoanzishwa na Rais John Magufuli  kuchunguza kuhusu mwenendo wa biashara ya madini  na makinikia, ambayo ilifichua uozo na wizi wa kutisha na udanganyifu uliokithiri wa rasilimali za taifa za madini  zenye thamani ya mamia ya shilingi trilioni na hivyo Bunge kubadilisha sheria mbalimbali  zilizoleta mabadiliko makubwa  ambayo yamelenga uboreshaji  huduma na ukusanyaji mapato ya taifa.

Matokeo yake kwa undani ni kupata sheria tatu ambazo zina  mtazamo wa kuboresha Uchumi wa nchi, zikiwamo (Written Laws Miscellaneous  Act , 2017, Natural Wealth and Resources (Permanent  Sovereignty) Act 2017 na Natural Wealth and Contracts Review and Renegotiation of Unconscionable Terms Act  2017.

Sheria hizo wanadai wengi ni sawa na tangazo la vita kwa ubeberu,  mtazamo ambao Rais  Magufuli ameuona na Waziri wake wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi  kuukubali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles