27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

TUKIMALIZANA NA MASHOGA TURUDI KWENYE HUDUMA ZA AFYA

NIMEONA mahali andiko la Naibu Waziri wa Afya, Dk. Hamis Kigwangalla kuwa akimaliza ziara yake jimboni atarudi kuja kutaja orodha ya watu wanaojihusisha na biashara ya ushoga mtandaoni.

Hili sijui hata nilizungumze vipi? Kama watatajwa ila sidhani kama watu wanataka kusikia orodha yao maana tukishawajua tutapata nini? Tuyaache hayo labda kuita vyombo vya habari na kutaja majina ya watu na kuitana ‘Central’ ndio mtindo wa kisasa.

Pamoja na kuwa suala la ushoga limekuwa sehemu ya tatizo kwenye jamii yetu lakini si tatizo kubwa kama suala la utoaji wa huduma za afya hasa kwenye hospitali za Serikali kiukweli hauridhishi.

Juma lililopita nilishikwa na malaria nikaenda kupata huduma kwenye hospitali moja ya serikali, wahudumu walikuwa wachache ambao waliwaacha wagonjwa wakihangaika bila kupata msaada.

Upatikanaji wa dawa pia ni wa shida, hospitali hazina dawa hali inayolazimu tutoke nje ya hospitali kwenye Dispensary kupata hayo madawa tunayopata kwa bei juu yaani hali si nzuri kwa kweli.

Nilifika hospitali nikiwa mahututi hali iliyonihitaji niwekewe drip ambayo ilinichukua karibu nusu saa nzima, manesi walikuwa wakizunguka tu huyu anaenda huku huyu anaenda kule, mara hakuna gloves yaani ilimradi tabu na ndio nikaelewa ni kwa nini kuna watu hufia mapokezi.

Unaonana na daktari anakuelekeza uende maabara ukacheki, unaenda mabaara unarudi na majibu unakuta daktari hayupo kwenye chumba chake kwa zaidi ya dakika 20 huku kuna wagonjwa chungu nzima wakisubiri wamuone.

Nikajiuliza mimi mwenye malaria na nimeenda hospitali na mtu nachelewa kupata msaada vipi kwa wale wanaofika bila ndugu zao wakihitaji msaada wa haraka huwa inakuwaje?

Suala la afya ni nyeti sana, nafahamu kuwa hospitali zetu zinahudumia watu wengi lakini hiyo haiwi sababu ya kwanini tusihudumie watu kwa viwango vizuri, ni lazima tujitahidi kuhudumia watu kulingana na namba iliyokuwepo, magonjwa yamekuwa mengi na watu nao ni wengi hivyo ni lazima namba ya wahudumu iongezeke.

Nitafurahi nikisikia kuna nguvu itakayoelekezwa kwenye utoaji wa huduma za afya baada ya hili la kuhangaika na mashoga, afya za Watanzania ni suala muhimu kwenye ujenzi wa Taifa.

Maana ili nchi iendelee inahitaji watu, sasa kama watu afya zetu zinapopata hitilafu hatupati huduma stahiki basi tutakuwa na taifa lenye watu magoigoi ambao hawataweza kushiriki vyema kwenye shughuli za uzalishaji.

Siku hizi serikali imejitahidi sana kwenye suala la ukusanyaji wa mapato kwenye hizi hospitali hivyo natarajia kuwa hata huduma zitaboreshwa na mazingira ya ufanyaji kazi kwa wahudumu yatakuwa ni yenye kuvutia pia.

Naomba nieleweke vyema si kwamba siungi mkono hatua zinazotaka kuchukuliwa dhidi ya mashoga la hasha nakubaliana nazo lakini nilikuwa nawakumbusha tu kuwa kuna tatizo kubwa hivyo tusilifumbie macho kisa tu kuna jambo fulani litakalopoteza mazingatio kwenye jambo kubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles