27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Tshishimbi auanza unahodha kibabe

Mohamed Kassara -Dae es salaam

NAHODHA mpya wa Yanga, Papy Tshishimbi ameanza kwa kishindo majukumu yake hayo mapya,  baada ya kufunga bao kwenye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Friends Ranger,  katika mchezo wa kirafiki uliochezwa jana mjini Morogoro.

Bao jingine la Wanajangwani hao, likiwekwa kimiani na mshambuliaji mpya wa timu kutoka Namibia, Sadney Urikhob dakika ya 38.

Tshishimbi amechaguliwa kuwa nahodha mkuu wa timu hiyo, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na kiungo, Ibrahim Ajib aliyetimkia Simba.

Kiungo huyo wa kimataifa wa  Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC), alijiunga na Yanga miaka miwili iliyopita akitokea Mbambane Swallows ya Eswatini(zamani  Swaziland), mkataba ambao ulimalizika mwishoni mwa msimu uliopita kabla ya kuongeza mwingine wa miaka miwili,  baada ya benchi la ufundi la klabu hiyo, kuridhika na kiwango chake tangu alipotua Jangwani.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Salehe alithibitisha Tshishimbi kuteuliwa kupewa wadhifa huo, baada ya kuteuliwa na Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera.

“Ni kweli Tshishimbi ni nahodha mpya wa kikosi cha Yanga, lakini wasaidizi wake bado hawateuliwa kwakua Juma Abdul ndiye anashikilia nafasi hiyo yupo Dar es Salaam, lakini kila kitu kitajulikana hapo badae,”alisema Hafidh ambaye kabla ya kukabidhiwa cheo cha sasa alikuwa meneja wa timu hiyo.

Hata hivyo, taarifa kutoka katika kambi ya timu hiyo inaeleza kuwa  kiungo mkongwe wa timu hiyo, Mrisho Ngasa anapigiwa chapuo kuwa msaidizi wa Tshishimbi, kutokana na kuwa miongoni mwa wachezaji wa muda mrefu wa kikosi hicho lakini pia akisifika kwa uzalendo wake.

Wakati huo huo, Yanga imeendeleza makali yake, baada ya kushinda michezo mitano mfululizo katika muendelezo wa mechi zao za kirafiki, ambapo ilianza kwa kuichapa Tanzanite mabao 10-1, ikashinda mabao 2-0 dhidi ya Moro Kids, ikaishushia mvua kwa kuichapa mabao 7-0 timu ya ATN, kabla ya kuinyuka Mawenzi Market bao 1-0.

Mbali na kuvuna ushindi mfululizo, kinachonogesha zaidi kambi hiyo ni kitendo cha timu hiyo kufunga mabao mengi, huku wachezaji wapya waliojiunga na timu hiyo, wakionekana kufunga karibu kila mchezo, kitu kinachotatafsiriwa kama ishara njema kwa kikosi hicho kuelekea msimu ujao.

Wababe hao wa Jagwani, wamefunga hesabu katika michezo ya kirafiki, ambapo sasa wanatarajia kurejea Dar es Salaam, kwa ajili ya mchezo wa kuhitimisha  siku ya tamasha lao walilolipa jina Wiki ya Mwananchi kwa kuumana na Kariobangi Sharks ya Ligi Kuu Kenya, utakaochezwa Jumapili  Uwanja wa Taifa.

Baada ya mchezo huo, Yanga itaendelea na maandalizi ya kuumana na Township Rollers ya Botswana, katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambao utachezwa kati ya Agosti 8 na 11, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku mchezo wa marudiano ukipangwa kupigwa kati ya Agosti 23 na 25, jijini Gaborone.

Kama Yanga itafanikiwa kuruka kiunzi hicho,  itakutana na mshindi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia, katika raundi ya kwanza, ambapo mbabe wa jumla atatinga hatua ya makundi.

Yanga imeweka kambi kwenye hoteli ya Highland Park mjini Morogoro, ikijifua Uwanja wa Chuo cha Biblia uliopo Bigwa, kwa ajili ya kujiandaa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wanajagwani hao wanarejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuikosa kwa miaka miwili.

Katika kuhakikisha inafanya vizuri kwenye michuano hiyo, Yanga imefanya usajili wa nguvu wa wachezaji wa kigeni pamoja na wazawa.

Wachezaji wa kimataifa waliojiunga na Yanga ni Issa Bigirimana (Burundi)
, Patrick Sibomana (Rwanda), Mustapha Suleiman (Burundi), Sadney Ukhrob (Namibia), Lamine Moro (Ghana), Maybin Kalengo (Zambia) na Juma Balinya (Uganda).

Wazawa ni  Ally Mtoni ‘Sonso’ (Lipuli FC), Abdulaziz Makame (Mafunzo),  Ally Ally (KMC), Mapinduzi Balama (Alliance), Metacha Mnata (Mbao FC) na Muharami Issa( Malindi).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,404FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles