23.6 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Kampeni kuelimisha, kupima TB Pemba yafanikiwa

Khamis Sharif -Pemba

WATU 20 wamegundulika kuugua ugonjwa wa kifua kikuu (TB) kati ya 375 waliochunguza afya mara baada ya mikutano ya kuelimisha jamii juu ya ugonjwa huo kwisha.

Akizungumza na MTANZANIA mwishoni mwa wiki kisiwani Pemba, Mratibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC), Kombo Khamis, alisema kwa kipindi hicho tayari wameshatoa elimu ya TB kwa watu 6,467.

Alisema wakati wanaendelea kutoa elimu na kuwapima, waligundua watu 20 wakiwa na ugonjwa huo kati ya 375 waliochunguzwa.

 “Tunaendelea kutoa elimu kwa jamii na tunapomaliza mkutano tu watu wanakuja kupima, wengine wanatufuata ofisini kwa siku nyingine,” alisema.

 Alisema tayari wameshazifikia shehia 13 kisiwani Pemba, visiwa vinne, madago mawili, masoko matatu, dahalia tano, nyumba ya kurekebisha tabia (Sober House) moja na mochuari moja (sehemu zinapopikwa pombe).

Akizungumzia kuhusu mabadiliko kwa shehia na sehemu wanazotoa elimu ya TB, alisema kuwa yapo makubwa, kwani kwa sasa watu wamehamasika na kushawishika kwenda kupima afya zao kwa wingi.

“Zamani wakati tunapita kwenye mashehia kutoa elimu ya TB, watu walikuwa hawataki kupima, lakini kwa sasa tunashukuru wanakuja na wanatoa ushirikiano mkubwa,” alifafanua.

Mgeni aliishauri jamii kuwa tayari kuchunguza afya zao, ili kupata tiba mapema kwa yule ambaye atagundulika, kwani TB ipo na inaambukiza.

“Jamii ni muhimu kuchunguza afya zenu, ili kuitokomeza TB, matibabu yapo na dawa zipo zinatolewa bure mahospitalini na kwenye vituo vya afya,” alisema.

Aidha, aliwashauri waandishi wa habari watoe elimu ya TB kupitia vyombo vyao, kwani ni jukumu lao kuielimisha jamii, jambo ambalo litasaidia kuwafikia wanajamii wengi kwa muda mfupi.

Wakati PPC ilipowafikia wananchi wa Shehia ya Bopwe Wete, walisema elimu hiyo imewasaidia kutoka hatua moja kwenda nyingine na kusema watawafikishia ujumbe wengine, ili na wao waweze kufaidika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,070FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles