23.2 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

TRC yawapa elimu ya fidia wananchi mradi wa SGR

Na Clara Matimo, Mwanza

Shirika  la Reli Tanzania (TRC), limezindua kampeni  ya uelewa kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza   juu ya uandikaji wa madai ya fidia katika maeneo yanayopitiwa na  Ujenzi wa Reli ya Kisasa(SGR).

Walengwa wa kampeni  hiyo ni wenye nyumba zilizo pembezoni mwa reli,   majengo, makaburi, viwanja na mashamba ambayo yatachukuliwa  na maeneo mengine yataondolewa ili kupisha utekelezaji wa mradi huo kwenye kipande cha Mwanza -Isaka.

  Kampeni hiyo imezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, katika Kata ya Nyamagana ambapo amewataka wataalamu watakaoshiriki zoezi la uthamini wawe waadilifu  waepuke vitendo vya rushwa watende haki kwa kupima    sawasawa na vigezo vilivyoainishwa ili kila mwananchi alipwe kulingana na anavyostahili.

“Kwenye ardhi kuna dhuluma sana, mara nyingi  haki haitendeki, yoyote atakayevuruga mradi huu kwa kutaka kufanya figisu ili ajinufaishe tukipata taarifa ataondoka, viongozi wa mitaa  na watendaji simamieni zoezi la  uhakiki  ili lifanyike  kihalali,  lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanaodai fidia hawadhurumiwi maana Serikali inania nzuri nao lakini baadhi ya watendaji wasiowaaminifu wanaweza kutumia mwanya huo kujinufaisha.

“Natoa onyo kwa wataalamu,  wananchi wasionewe na nyie wananchi   asije mtaalamu  wa uthamini akakwambia eneo lako linathamani ya Sh milioni tano  lakini nakuandikia milioni 10 utanigawia milioni moja huyo ni mwizi usikubali kwa sababu halali yako ni hiyo milioni 10 ikitokea hivyo njoni ofisini kwangu tutamshughulikia,”amesema Mhandisi Gabriel.

Afisa Mwandamizi Kitengo cha Ardhi kutoka TRC, Fredrick Kusekwa,  amewasisitiza walengwa kama wana migogoro ya maeneo yao waimalize mapema kabla  zoezi la uthamini halijaanza   kwa kuwa huwa inachelewesha fidia kwa wahusika.

“Kama mna migogoro ndani ya familia, mipaka, uwakilishi kwenye masuala ya mirathi, uwakilishi kwenye zoezi la uhamishaji wa makaburi, itatueni mapema ili kurahisisha zoezi la uthamini na malipo ya fidia yaweze kwenda kwa haraka migogoro huwa inachelewesha fidia kwa wahusika pia wamiliki washiriki katika zoezi la uthamini na hatua zote za uthamini wakiwa na nyaraka rasmi za kuwatambulisha,”amesema Kusekwa.

  Diwani wa Kata ya Nyamagana, Bhiku Kotecha,  amewataka wananchi watoe ushirikiano  kwa Serikali  wakati wa ujenzi kwa kulinda miundo mbinu na mali ambazo zitatumika kwenye mradi.

 Baadhi ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo ambayo yatapitiwa na mradi huo akiwemo Sausi Nyamhanga, wameitaka Serikali kutoweka hujuma  kila mtu alipwe kwa jinsi anavyostahili bila kutoa rushwa.

NayeThereza Magambo mmoja wa wafanyabiashara, eneo ambalo litapitiwa na ujenzi huo, ameiomba Serikali kuwatengea eneo lingine la kufanyia shughuli zao ili waendelee kujikimu kupitia kipato wanachopata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,250FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles