24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wafuasi Chadema wafanya maombi kwa ajili ya Mbowe

Na Clara Matimo, Mwanza

Baadhi ya wafuasi wa Chama cha CHADEMA jijini Mwanza wamekusanyika katika ofisi za chama hicho Kanda ya Viktoria na kufanya maombi kwa ajili ya Mwenyekiti, Freeman Mbowe.

Maombi hayo yameongozwa na Askofu wa Kanisa la Evangelical Pentecostal Restoration(EPRC) ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo Mkoa wa Mwanza, Amos Hulilo.

Akizungumza  kabla ya kuanza maombi, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Mbutusyo Mwakihaba, amesema wamekusanyika kwa ajili ya maombi na si kuvunja amani maana  wanaamini Mwenyekiti wao hana hatia kwa  shauri linalomkabili  ambalo ndani yake kuna shitaka la ugaidi hivyo wanamuomba Mungu akatamalaki katika kesi hiyo.

“Lengo la maombi ni kumuomba Mwenyezi Mungu awakumbushe kutenda haki na   weledi waliosomea  viongozi wote wanaofanya kazi ndani ya vyombo vyote  vya ulinzi na usalama,  sheria na  watu wote  wanao toa  haki, watende haki si tu kwa wanachama wa chadema bali kwa wananchi wenye tuhuma mbalimbali mtu akifikishwa mahakamani afikishwe kwa tuhuma za kweli,” amesema Mwakihaba.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Baraza la Wanawake Chadema  (Bawacha) Jimbo la Nyamagana, Hyasinta Wanchelele, amesema wanaamini  mamlaka zote zinatoka kwa Mungu ndiyo maana wamefanya maombi hayo wakimsihi Mungu  awakumbushe watawala kutumika kwa haki ili kuepuka mipasuko miongoni mwa watanzania.

Amesema watanzania waliishi  kama ndugu hawakutengenezeana visasi  kutokana na misingi imara ya upendo, umoja na mshikamano aliyoijenga Baba wa Taifa  Mwalimu Nyerere  na Biblia Takatifu kitabu cha  Yeremia 1:7  Mungu anasema  kabla sijakuumba nalikujua kabla sijakutoa tumboni mwa mama yako nalikutakasa ili ukawe nabii na mfalme wa mataifa.

 “Kwa hiyo kama Mungu alimuumba Mbowe akampa mamlaka aje kuwatumikia watanzania kupitia Chadema  tumeona tuje tumuombe  asimuache mwenye haki aendelee kuteseka,  tunamlilia yeye aliyehakimu wa haki ashuke ahukumu kwa haki kutokana na tuhuma zinazomkabili  Mwenyekiti wetu pamoja na viongozi wengine wapenda haki ndani ya taifa hili.

“Sisi sote ni watanzania hakuna aliyemkimbizi ndani ya taifa hili kila mtu anayo nafasi ya  kuongoza kadri Mungu alivyomkusudia,  tunapozuia makusudi ya Mungu juu ya wanadamu aliyowaumba tunakuwa tumemkosea  inamaana tunamkosoa, tusifike mahali tukaingilia nafasi ya Mungu tumpe  nafasi afanye kazi kama alivyokusudia juu ya watu wake,”amesema Hyasinta.

 Akizungumza na wafuasi hao kabla ya kuanza maombi, Askofu  Hulilo amesema ili nchi idumu katika amani na utulivu ni wajibu wa kila mtanzania kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan, Mungu ampe hekima na washauri wema ambao watamshauri vizuri.

“Nafasi aliyonayo rais ni kubwa anaongoza wanaompenda na wasiompenda, wanachama wa vyama vyote vya siasa vilivyopo nchini na watanzania wenye dini mbalimbali, tuliombee pia taifa letu ili liwe na amani matukio ya kuuwana, kukamatana na kuchukiana yanasababisha mgawanyiko miongoni mwa watanzania.

“Ukisoma Biblia Takatifu kitabu cha Mithali 14:34 inasema haki huinua taifa dhambi ni aibu ya watu wote. Kwa hiyo tuombe bila kuchoka ili viongozi wetu wa taifa hili watende haki Mungu aliinue taifa letu,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles