29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

TFF IWE MACHO UPANGAJI WA MATOKEO DARAJA LA KWANZA

MASHINDANO ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara iliyoanza Septemba 16, mwaka huu, yanazidi kushika kasi katika viwanja mbalimbali, tukitarajia kuona msimu ujao timu sita zikipanda kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Rais wake, Wallece Karia, imetangaza kuwa timu sita za Ligi Daraja la Kwanza zitapanda kucheza Ligi Kuu msimu ujao na hivyo kuwa na timu 20.

Hii inashiria kuwa Ligi Daraja la Kwanza msimu huu itakuwa na ushindani wa aina yake kutokana na kupanda timu sita, lakini pia timu mbili zikishuka daraja kutoka ligi kuu, hali hii inaweza kuleta udanganyifu na hata upangaji wa matokeo.

Ikumbukwe kuwa mara nyingi baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza zimekuwa na tabia ya udanganyifu na hata upangaji wa matokeo, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za soka duniani.

Sisi MTANZANIA kwa kuliona hilo, tunaiomba TFF ianze mikakati mapema ya kuzuia udanganyifu na upangaji wa matokeo ili kuleta ushindani wa kweli katika Ligi Daraja la Kwanza, lakini pia kuipa haki timu ambayo inastahili kupanda ligi kuu kwa uwezo wake na si kubebwa.

Suala la upangaji halikubaliki na linapaswa kukemewa kwa nguvu zote, ndio maana zimewekwa sheria kali kwa timu itakayobainika kufanya hivyo ili iwe fundisho, lakini pia kunahitajika umakini ili kubaini viashiria vya upangaji wa matokeo katika mchezo.

Katika msimu uliopita, kuliibuka upangaji wa matokeo katika Ligi Daraja la Kwanza na timu za JKT Kanembwa, Geita Gold SC, Polisi Tabora na JKT Oljoro zilishushwa daraja kutokana na kubainika kupanga matokeo.

Adhabu ya kushushwa daraja kwa timu hizo liwe fundisho kwa timu nyingine zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza msimu huu.

Sisi kama wadau wa soka hatutarajii kuona mambo kama haya yanatokea tena katika msimu huu, kwani hayawezi kuendeleza soka letu na badala yake yatafifisha maendeleo.

MTANZANIA tunaona kuwa jambo hili lianze kutupiwa macho mapema kabla ya hata mambo hayajafikia ukingoni mwa ligi hiyo, kwani yawezekana zikatafutwa mbinu mbadala za mapema ili zisibainike katika upangaji huo wa matokeo.

Ni jambo la msingi kwa TFF kuhakikisha kuwa wanafuatilia ligi hii kwa karibu ili kuangalia aina yoyote ya upangaji wa matokeo, kwa vile kila timu itakuwa ikihitaji kupata nafasi ya kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya nafasi hizo sita.

TFF isimamie kanuni zake ipasavyo na iwapo msimu huu kutatokea tena upangaji wa matokeo, isisite kuwachukulia hatua viongozi, waamuzi, wachezaji na hata timu zilizohusika katika vitendo hivyo viovu vinavyozorotesha mchezo huo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles