24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

TFDA yatoa neno mayai yenye viini viwili yaliyozua hofu

 Grace Shitundu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) imewatoa hofu wananchi juu uwepo wa mayai yenye viini viwili na kusema kwamba hayana madhara yoyote.

Wakati TFDA wakisema hayo tovuti inayofuatilia usalama wa mayai ya ‘Egg Safety Center’ inaeleza kuwa viini viwili katika yai moja si jambo la kawaida sana ‘unsual’ na kutokea kwa viini viwili kunaweza kuhusishwa na usalama wa chakula.

Kauli hiyo ya TFDA imekuja baada ya kusambaa video ya dakika 1:19 inayonyesha kijana anayeuza mayai ya kuchemsha yenye viini viwili na hivyo kuzua hofu kwa walaji.

Katika video hiyo kijana muuza mayai anaonekana akiwa na vijana wengine wawili ambao walionyesha kuingiwa hofu baada ya kumenya yai moja walilonunua na kukuta lina viini viwili. Kijana huyo muuza mayai alisema mayai hayo yote yana viini viwili na kumenya jingine ambalo nalo lilikuwa hivyo hivyo.

Alidai mayai hayo wanachukua kutoka kampuni ya Interchic ingawa wao hajui hasa chanzo cha kuku wanaotoa mayai hayo.

“Haya tunachukua Interchic lakini sijui yanapotoka ila ni lazima yawe na viini viwili na yanatoka kwa kuku chotara” aliwaeleza wateja wake kijana huyo muuza mayai.

Katika kutaka kudhibitisha kama jambo hilo ni kweli kijana mteja alitaka limenywe yai jingine ili kuhakikisha endapo nalo lina viini viwili ambapo baada ya kumenya na kukata vilionekana.

“Haki ya Mungu haya ndio mayai ya kutengeneza, kwa kweli mtatuua uwii’, alisikika kijana mnunuzi akisema.

Baada ya video hiyo kusambaa na kuzua mjadala kwenye mitandao mbalimbali ya jamii hasa katika makundi ya whatsapp, Mtanzania Jumapili liliwatafuta TFDA kupata ufafanuzi juu ya hofu hiyo.

Ofisa Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza alisema mayai yenye viini viwili hayana shida yoyote.

“Ukifuatilia hiyo ‘clip’ na ukienda kufatili kule yanakotoka wanaweza kukueleza kwanini mayai yote yametoka hivyo.

“Wao wanajihusisha na utotoleshaji vifaranga, wanapototolesha wanapoona mayai yana viini viwili, hayafai kutotolesha vifaranga hivyo wanaweka pembeni yanauzwa kwa hiyo hamna ‘ishu’ hapo” alisema Gaudesia .

MTANZANIA Jumapili liliwawatafuta Interchic kwa njia ya simu ambayo ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Bakita Kiongosi aliyesema kampuni hiyo haiuzi mayai bali inajihusisha na kuuza kuku, nyama, vifaranga na chakula cha kuku.

“Sisi hatuuzi mayai kwa mteja yoyote, sisi tunazalisha mayai ya kuku na kutotolesha vifaranga, hatuuzi mayai sehemu yoyote kwa mteja yoyote,” alisema Bakita.

MTANZANIA Jumapili pia liliwatafuta wazalishaji wengine wa vifaranga nchini ambao ni kampuni ya AKM Glitters Limited na kuzungumza na meneja masoko wake, Michael Joseph ambaye alisema mayai kuwa na viini viwili hilo jambo lipo na aina ya kuku ambaye anaweza kutoa mayai hayo ni aina ya Kroiler.

Hata hivyo Michael aliomba atumiwe kipande hicho cha video ili akione na alipokiona alirudi kwa mwandishi na kuendelea kueleza juu ya hali hiyo kuwa;

“Huyo kijana anasema anachukua kutoka kampuni ya Interchic sasa sijajua hayo mayai anayatoa kwa kuku wa aina gani maana kuna kuku aina nyingi, kuna kroiler, sasso, na kuku wa malawi

Akielezea kwa upande wao alisema kuwa wao wanahusika na hao kuku wa Kroiler na ndio kampuni pekee inayohusika na kuku aina hiyo nchini, lakini hawauzi mayai bali wanauza vifaranga.

Michael alisema huenda ni wateja ambao wanauziwa kuku hao ndio wanaozalisha mayai hayo. “Sisi hatuuzi mayai, bali tunauza vifaranga sasa wakianza kuwakuza na kufikia hatua ya kutaga ndio wanaweza kutaga mayai ya aina hiyo” alisema.

“Hata hivyo hiyo hutokea ‘by chance’ yaani ni sawa na kama mtu kupata watoto mapacha, yaani kuku anaweza kwa wiki akataga mayai matano na moja au mawili kati yao yakawa na viini viwili ndani” alisema

Alisema hiyo inawezekana mfugaji akawa anayakusanya na yanapofikia trei anayauza lakini si kwamba kuku kwa wiki nzima anaweza akawa anataga mayai hayo ya viini viwili.

Kuhusu kuwa na madhara, Michael alisema hayana madhara yoyote, ila kwa hayo ambayo yameonekana kwenye kipande hicho cha video hawezi kujua kwa kuwa hajui chanzo chake.

Aidha tovuti ya ‘Egg Safety Center’ imeeleza kwamba ni kawaida yai kuwa na kiini kimoja lakini kuna nyakati za nadra hutokea kuwa na viini viwili.

“Yai kuwa ni viini viwili ni jambo la nadra sana, kwa kawaida mayai yenye viini viwili hutagwa na kuku wadogo ambao mifumo yao ya uzazi haijawa kamilifu pia yanaweza kutagwa na kuku wakubwa wanaokaribia kufika ukomo wa kutaga mayai” unaeleza mtandao huo.

Mtandao huo unaeleza kwamba viini viwili katika yai moja si jambo la kawaida sana ‘unsual’ kutoka katika yai, na kutokea kwa viini viwili kunaweza kuhusishwa na usalama wa chakula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles