25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Rushwa ya ngono Chuo Kikuu SAUT yaundiwa kitengo

BENJAMIN MASESE NA CLARA MATIMO -MWANZA

CHUO Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) jijini hapa, kimeanzisha kitengo maalumu ambacho kitakuwa kikipokea malalamiko ya wahadhiri wanaotumia nafasi zao kuomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Costa Mahalu, alisema hayo jana alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano wa uzinduzi wa kuelekea jubilee ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa SAUT.

Jubilee hiyo itafanyika Julai 2, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Profesa Mahalu alisema chuo hicho kilianzishwa kwa lengo la kiroho na kielimu na suala la mahusiano ya kimapenzi ni siri ya watu wawili na uthibitisho wake umekuwa mgumu.

Hata hivyo, alisema kutokana na uwepo wa malalamiko hayo katika vyuo mbalimbali, SAUT imeamua kuanzisha kitendo maalumu ambacho kitakuwa kinafanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua kwa mhusika.

Alisema kitengo hicho kitakuwa kinapokea malalamiko kwa njia ya maandishi au ana kwa ana, kwamba mlalamikaji atalazimika kutaja jina lake na mhadhiri anayemtaka kimapenzi kisha uchunguzi utafanyika na atakayebainika ni chanzo atachukuliwa hatua.

“Hili suala napata ugumu kusema lipo hapa au halipo, lakini malalamiko yapo ila ushahidi unakuwa mgumu sana, mahusiano ni ya watu wawili, lakini mmojawapo anaposhindwa kuelewana na mwenzake huibuka hadharani, kama SAUT tunasema  tunavichukulia kama vitendo viovu na hawa ndio wanachafua jina letu.

“Hapa SAUT tuna kitengo cha ‘Social Ethics’ (maadili ya jamii) ambapo wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanapofika tu tunawapa elimu ya namna ya kuishi chuoni na maadili yake, maana wapo baadhi ya wanavyuo wanapopata uhuru wa kujiamulia, hasa wale ambao hawajalelewa katika maadili mema, hufanya mambo ya ovyo, pia tumewaelekeza  watawa wetu na mapadre wetu kuwajaza elimu ya maadili.

“Hayo ni matukio machache tu ambayo yanachafua vyuo, lakini hapa SAUT kama mnavyoshuhudia, tuna wanafunzi zaidi ya 13,000. Idadi hii ni kubwa na inatokana na ubora wa elimu tunayoitoa hapa.

“Nia yetu ni kuona malengo tuliyojiwekea yanatimia ikiwa ni kuwa chuo cha mfano Afrika, ambacho kinatoa wabobezi wa kada mbalimbali wanaohimili ushindani katika soko la ajira duniani,” alisema.

Akizungumzia ujio wa Rais Mkapa katika sherehe hiyo, Profesa Mahalu alisema ndiye mwasisi wa elimu ya juu katika vyuo binafsi nchini akisaidia mambo mbalimbali ndani ya SAUT, ikiwamo kuwaongezea eneo la chuo, kujenga barabara ya lami kuelekea chuoni na kutoa misaada ya fedha katika kutekeleza miradi inayoanzishwa.

Profesa Mahalu alisema mafanikio yaliyopatikana tangu chuo hicho kuanzishwa mwaka 1998, ni pamoja na kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 204 hadi 11,400 kwa mwaka wa masomo 2018/2019, kuongeza matawi mapya 13, kuanzisha kituo cha haki za binadamu, kuongeza vitivo vinne kutoka kimoja cha sayansi ya jamii na maswasiliano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles