30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

Simu yako ni jasusi unayetembea naye mfukoni

*Wadukuzi wanaweza kuwasha kipaza sauti, kamera na kufanya chochote watakacho

LONDON, UINGEREZA

KWA watu wengi duniani simu za kisasa za smartphone ni fursa ya kufikia dunia, lakini maswali yameibuliwa ikiwa fursa hiyo inatoa mwanya wa kufikiwa kwa maisha yao binafsi.

Hebu tafakari ikiwa wadukuzi watakuwa na uwezo wa kufikia simu yako na kuchukua kila kitu kilicho ndani, ikiwa ni pamoja na ujumbe mfupi (SMS) na kudhibiti kinasa sauti na kamera yake.

Ukweli ni kwamba haya ni mambo yanayofanyika katika dunia ya sasa japo huenda usiamini kama hilo linawezekana.

Lakini ni nani anayefanya hivyo na kwanini?

Mtaalamu wa usalama wa kimtandao katika Kampuni ya Lookout mjini San Francisco, California inayosaidia Serikali, biashara na watu binafsi kuhakikisha taarifa zao binafsi ziko salama, Mike Murray, anaelezea jinsi programu za udukuzi zinavyobuniwa na vile zinavyofanya kazi.

Anasema programu hiyo imeorodheshwa kuwa silaha ya kiwango cha juu ambayo inauzwa kwa udhibiti mkubwa.

“Wataalamu wa programu za ujasusi wanaweza kukufikia kupitia mfumo wa GPS.

“Wanaweza kuwasha kipaza sauti na kamera wakati wowote na kurekodi kila kitu kinachofanyika katika mazingira yake.

“Inaiba nambari ya siri ya kufikia app ya mitandao ya kijamii uliyonayo, kuiba picha, nambari za watu ulizonazo katika simu yako, taarifa zako za siri, barua pepe zako, na stakabadhi nyingine muhimu ulizonazo.

“Yaani inageuza simu yako kuwa kifaa cha wizi ambacho wanaweza kukisikiliza wakati wowowte wanapotaka kukufuatilia na kuiba kila kitu kilichopo ndani yake,” anasema Murray.

Programu za ujasusi zimekuwepo kwa miaka kadhaa, lakini hizi za sasa zimefikia kiwango cha juu zaidi.

Hii ya sasa haifikii data ambayo imefichwa katika simu yako kupitia mfumo unaoziba mawasiliano maandishi kati ya watu wawili, lakini imekuwa ikishindana na mfumo huo kupitia teknolojia ya kisasa ambayo inaendelea kuimarishwa kila uchao.

ILISAIDIA CHAPO KUKAMATWA

Mlanguzi sugu wa dawa za kulevya nchini Mexico, Joaquín Guzmán maarufu kama El Chapo, alikuwa akimiliki himaya ya thamani ya mabilioni ya madola.

Baada ya kutoroka jela, alienda mafichoni kwa miezi sita, kwa usaidizi wa mtandao wake wa wahalifu na alikuwa akiwasiliana kupitia simu ambayo ilikuwa vigumu kudukuliwa na majasusi.

Lakini mamlaka ya Mexico iliponunua programu mpya ya ujasusi, ilisaidia kufikia simu ya El Chapo na washirika wake waliokuwa mafichoni.

Kukamatwa kwa El Chapo kunaashiria jinsi programu hiyo inavyoweza kutumiwa kama silaha ya kukabiliana na ugaidi na wahalifu sugu kwa kushirikiana na kampuni za simu.

SIMU YA MTU ANAYEKOSEA SERIKALI

Mwanablogu Rori Donaghy anayeendesha shughuli zake za kimtandao Mashariki ya Kati, alikuwa akiripoti visa vya ukiukwaji wa haki za kibinadamu vinavyotekelezwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kuanzia jinsi wafanyakazi wahamiaji na watalii wanaokiuka sheria za nchi hizo walivyokuwa wakidhulumiwa.

Alipata wasomaji wengi waliokuwa wakifuatilia taarifa zake mitandaoni. Lakini haikuchukua muda mrefu alianza kupata barua pepe kutoka kwa watu asiowafahamu.

Donaghy aliwasilisha moja ya barua pepe hizo kwa kundi la utafiti linalofahamika kama Citizen Lab, lenye makao yake katika Chuo Kikuu cha Toronto, Canada ambalo linachunguza jinsi ujasusi wa kidijitali unavyotumiwa kuwalenga waandishi wa habari na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu.

Walithibitisha ‘link’ zilizoambatanishwa katika barua pepe alizokuwa akitumiwa zilikuwa zitumiwe kudukua mitambo yake na pia kuwafahamisha wadukuzi hao ulinzi anaotumia kulinda vifaa vyake vya kazi.

Watu waliokuwa wakimtumia Donaghy barua pepe hizo, waligunduliwa kuwa majasusi wanaofanya kazi kwa niaba ya Serikali ya UAE mjini Abu Dhabi.

Serikali ilikuwa na hofu huenda mtandao unaoendeshwa na Donaghy unashirikiana na makundi yenye itikadi kali ambayo huenda yakawa tishio kwa usalama wa taifa.

Mwanaharakati maarufu ambaye pia alishinda tuzo kwa kutetea haki za kibinadamu, Ahmed Mansoor, amekuwa akilengwa na shirika la kijasusi la UAE kwa miaka mingi.

Mwaka 2016 alipata ujumbe wa kutilia shaka, ambao pia aliusambaza kwa The Citizen Lab.

Kwa kutumia simu aina ya iPhone ambayo haina programu yoyote, timu ya utafiti ilibofya link, na kile walichokiona kiliwashangaza.

Ilikuwa ni simu ya smartphone inayoonesha data, licha ya kwamba haina programu yoyote.

Simu aina ya iPhone imetengenezwa kwa kuzingatia usalama, lakini programu moja ya kisasa zaidi iligundua shimo lililotokana na mdudu katika mfumo wa simu ya Apple.

Kampuni ya Apple ililazimika kumfahamisha kila mmoja duniani.

Bado haijafahamika ni taarifa gani zilizopatikana kwa simu ya Mansoor, lakini alitiwa mbaroni na kufungwa kifungo cha miaka 10 gerezani.

Kwa sasa amezuiliwa katika eneo ambalo hawezi kuchanganyika na wengine.

Balozi wa Falme za Kiarabu jijini London, ameiambia BBC kwamba taasisi zao za usalama zinatimiza viwango vya kimataifa na sheria za ndani ya nchi, lakini kama nchi nyingine, haiwezi kuzungumzia chochote kuhusu masuala ya kiusalama.

Oktoba mwaka 2018, mwanahabari Jamal Khashoggi aliingia katika Ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul nchini Uturuki, na hakuwahi kuonekana tena, baada ya madai kuibuka kuwa aliuawa na mawakala wa utawala wa nchi hiyo.

Rafiki wa mwanahabari huyo, Omar Abdulaziz, alidai kuwa simu yake ilidukuliwa na watu aliosema ni maofisa wa Serikali ya Saudi Arabia.

Abdulaziz anaamini kuwa udukuzi huo ulichangia mauaji ya mwanahabari huyo maarufu ambaye alikuwa akilengwa na Serikali.

Anasema walikuwa wakiwasiliana sana na katika mazungumzo yao waliangazia siasa za taifa lao na miradi ya maendeleo waliyokuwa wakishirikiana kufanya.

Kwa muda mrefu Serikali ya Saudi Arabia ilikuwa ikifikia mawasiliano hayo na hata nyaraka walizokuwa wakitumiana kupitia simu zao.

Serikali ya Saudi Arabia katika tamko lake kuhusu madai hayo, ilisema japo kuna programu zinazotumika kudukua simu za watu kisiri, hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa ilihusika na madai yanayotolewa dhidi yake.

Mei mwaka huu, kulikuwa na udukuzi wa hali ya juu wa mtandao wa kijamii wa WhatsApp, ambayo watu wengi hutumia kuzungumza na marafiki na familia karibu kila siku.

Kama ulidhani udukuzi huo ulimaanisha tu kuwa mtu anaweza kusikiliza mawasiliano ya simu kupitia WhatsApp, basi itabidi utafakari upya.

Udukuzi wa mtandao huo ulikuwa na uwezo wa kuvuruga programu nzima ya simu, punde ukishafunguliwa, mdukuzi ana uwezo wa kupakua programu ya kuweza kufuatilia kila kitu katika simu ya muathiriwa.

Aliyeathirika na udukuzi hakuhitaji hata kubofya kiunganishi chochote, simu yake iliweza kudukuliwa kwa yeye tu kupiga simu na kisha kuikata.

Hii inajulikana kama teknolojia ya pasi kubonyeza. WhatsApp ilichukua hatua za dharura kuwalinda watumiaji wake bilioni 1.5, lakini hakuna ajuaye nani alihusika na udukuzi huo.

WhatsApp ililengwa kipindi hiki, lakini swali ni je, ni App ipi itakayolengwa katika siku zijazo?

Watengenezaji wa programu kama hii ya ujasusi, huhitaji leseni maalumu ya kuiuza katika mataifa ya ng’ambo, sawia na ilivyo na kandarasi za kijeshi.

Programu hiyo inauzwa kwa minajili ya kuwazuia wahalifu. Lakini mahabara ya Citizen Lab, wamegundua kile wanachoamini kuwa ni utumizi mbaya wa programu hiyo na Serikali zilizoinunua.

Je, waundaji wa programu hii wanapaswa kuwajibishwa kuhusiana na matumizi mabaya?

Tofauti na silaha nyingine kama bunduki, mfumbuzi wake amesalia katika sekta ya huduma na pia kutoa muongozo na ufundi baada ya kuuza programu hiyo.

Lakini je, wao watahusika ikiwa programu hiyo itatumika vibaya baada ya kuiuza?

Kampuni inayoongoza katika sekta ya udukuzi halali na unaoruhusiwa ni NSO Group ya Israel.

Kampuni hiyo imekuwepo kwa takriban muongo mmoja na hupata mamilioni ya dola kila mwaka.

Wakili mmoja ameishtaki kampuni hiyo mahakamani kwa madai ya kudukua simu ya mteja wake.

Ni wakati muhimu sana na itasaidia kubainisha majukumu ya kampuni za kutengeneza programu za udukuzi baada ya programu zao kuuzwa.

Kampuni ya NSO imekataa kutoa tamko lolote, lakini katika taarifa yake imesema teknolojia inazipa taasisi za Serikali zilizopewa leseni vifaa wanavyohitaji kuzuia na kuchunguza uhalifu, na kuwa teknolojia yao imeokoa maisha ya watu wengi.

Wakili huyo sasa amedai kuwa ameanza kupokea simu kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp kutoka kwa watu wasiojulikana.

Habari kwa hisani ya BBC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,195FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles