28.4 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

TBPL yaingia mkataba na kampuni ya JJ Agricultural kusambaza viuatulifu hai

Na Gustafu Haule, Mtanzania Digital

KIWANDA cha Kibaiolojia cha Tanzania Biotech Product Limited (TBPL) kilichopo Kibaha mkoani Pwani kimeingia rasmi mkataba wa miaka mitatu na kampuni ya JJ Agricultural Ltd kwa ajili ya kusambaza dawa mpya za viuatilifu hai vitakavyotumika katika kupambana na wadudu waharibifu wa mazao.

Kiwanda cha Tanzania Biotech Products Limited kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Kiwanda hicho ambacho kinamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100, mbali na kutengeneza viuatilifu ya kuua mazalia ya mbu lakini pia kinatengeneza dawa za kuua viuadudu wanaoshambulia mazao ikiwemo  pamba, mahindi, matunda na mbogamboga.

Mkataba huo umesainiwa leo katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya kiwanda cha TBPL Kibaha ambapo kwa upande wa kampuni ya TBPL imewakilishwa na meneja mkuu wa kiwanda hicho, Rafael Rodriquez wakati kwa upande wa JJ Agricultural Ltd imewakilishwa na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mhandisi James Kilaba.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kutiliana saini mkataba huo Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Rafael Rodriquez ameeleza kufurahishwa na makubaliano waliyofikia na kampuni ya JJ Agricultural Limited ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo ni mafanikio makubwa katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata fursa ya kufikiwa na bidhaa hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tunatambua changamoto inayowakabili wakulima ya uwepo wa wadudu waharibifu  katika mazao yao lakini makubaliano haya yanakwenda kuwasaidia wakulima katika kupatikana kwa dawa hii hali itakayowafanya wakulima kuongeza tija na uzalishaji katika mazao yao” amesema Rodriquez.

Muonekano wa dawa za viuadudu waharibifu wa mazao iliyohifadhiwa katika madumu mbalimbali kiwandani hapo.

Rodriquez ametumia fursa hiyo kubainisha sifa za kipekee za dawa hizo za viuatilifu kuwa ni tofauti na dawa zingine zinazopatikana sokoni kwa kuwa zenyewe zimetengenezwa kwa namna ya viuatilifu hai ikilinganishwa na dawa zingine zisizo za kibaolojia zinazopelekea madhara kwa watumiaji kama vile magonjwa ya kansa pamoja na kuharibu mazingira.

Rodriguez amesema kuwa wameamua kuingia mkataba na kampuni hiyo ili kuhakikisha wakulima wote nchini wanafikiwa na dawa hiyo kwa haraka na hivyo kuwaondolea changamoto ya kuharibiwa mazao yao huku akiwaomba  mawakala wengine kujitokeza kwa wingi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya JJ Agricultural Ltd, Mhandisi James Kilaba ameishukuru TBPL kwa kufikia makubaliano ya kusaini mkataba huo huku akiomba kupewa ushirikiano katika kipindi chote cha utekelezaji wake.

Kilaba amesema kuwa miongoni mwa kazi zitakazofanywa na kampuni hiyo ni pamoja na kuhakikisha wanaandaa mashamba darasa katika maeneo mbalimbali hapa nchini ambayo yatatumika katika kutoa elimu kwa wakulima juu ya namna bora ya kutumia dawa hizo katika kupambana na wadudu waharibifu katika mazao yao.

Kilaba amesema kwa kuanzia dawa hizo zinatarajia kupatikana katika mikoa ya Dar es salaam Pwani, Morogoro, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Iringa, Dodoma Singida, Katavi pamoja na Tanga na utahusisha pia utoaji wa mafunzo ya namna bora ya kutumia dawa hizo ambao utakuwa unafanywa na wataalam kutoka katika kiwanda cha TBPL.

Hatahivyo,kiwanda cha Kibaolojia cha TBPL ni kiwanda pekee kilichopo nchini na Barani Afrika ambacho kinamilikiwa na serikali na kinazalisha dawa za kibaolojia ikiwemo Viuadudu vya kupambana na Malaria (biolarvicides)  na dawa za viuatilifu hai vya kilimo (biopesticides).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles