TAZARA YATUPA KARATA UTALII WA AFRIKA KUSINI

0
691

Na Mwandishi Wetu


WADAU wanaitaka Tazara kulitazama suala la utalii kwa nguvu na umakini mkubwa, ili kulinusuru shirika hilo linalochechemea lifanye vizuri katika shughuli zake.

Wanasema inawezekana kabisa shughuli ya utalii ikawezesha kupatikana mapato ya haja na kukuza mwingiliano wa watu katika eneo la SADC, ambako Tanzania ni mwanachama wa uhakika.

Kwa miaka mingi kumekuwa na safari za majaribio na za upande mmoja kutoka Afrika Kusini kuja Tanzania na si kwenda Afrika Kusini na hivyo, kufanya safari hizo za kitalii kuwa ghali kwani likiegesha treni hapo stesheni hakuna shughuli nyingine hadi wakati wake wa kurudi na mara nyingi halichukui abiria hapa kwenda Afrika Kusini ingawa nchi imeshapata wenye fedha wa kutosha ambao wangependa kutalii kwa treni kwenda Afrika Kusini.

Wadau wanasema shida kubwa iliyopo nchini ni mwenendo wa ‘gendaweka’ (stand alone), ulioshamiri ambapo kila kampuni au shirika hupenda kufanya mambo yake bila kushirikisha wengine na hivyo kukosa ushikiano na huduma ya kimtandao yenye uzalendo ndani yake.

Hivi basi taarifa ya kuwa Tanzania Tourist Board (TTB) na Tanzania Zambia Railway Authority (Tazara) kushirikiana kwa kuweka pamoja rasilimali zao ili kuweza kuwavutia wasafiri na watalii matajiri kutoka Afrika Kusini kutembelea nchi hii ni hatua nzuri ya kusifiwa.

Hayo ni matokeo ya majadiliano ya pamoja kati ya TTB na Tazara katika kuhudumia watalii wanotumia Rovos Rail kutembelea Tanzania na kuainishwa katika kauli ya pamoja jijini wiki iliyopita.

Rovos Rail ni kampuni ya Reli ya Afrika  Kusini ambayo inaelezwa kuwa ni ya fahari na starehe kubwa duniani inayofanya kazi nchini humo kwenye Stesheni ya Capital Park, mjini Pretoria makao makuu ya Serikali ya Afrika Kusini.

Hiyo treni kama hoteli, inaendeshwa kwa umakini mkubwa kwa njia mbalimbali Kusini mwa Afrika yote kwenda Namibia na Tanzania.

Ni starehe tupu kwenye treni hizo ambapo zipo behewa mbili za mapumziko na za burudani, migahawa miwili, maeneo ya malazi binafsi (private) zenye sehemu ya kulala na maeneo ya kubarizi na kukaa na wageni wa mhusika.

Akielezea ujio wa watalii hao 60 na ubia wa Tazara na mwenendo wa Rovos Train Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Devotha Mdachi, alisema ushirikiano huo ambao umeanza kwa mara ya kwanza kushughulikiwa kwa pamoja inabidi uendelezwe kwa manufaa ya nchi na kukuza utalii.

Kabla ya kufika Tanzania watalii hao walipita Botswana, Zimbabwe na Zambia kabla ya kutinga Tanzania katika treni ya starehe ya Rovos inayoongoza kwa ubora wa starehe duniani.

Anasema kuwa treni hizo za matajiri ni muhimu kufanya vivutio vya utalii vya Tanzania vijulikane duniani kote na hivyo kuleta faida nyingi kwa nchi.

“Watalala katika hoteli zetu, watanunua sanaa zetu za kiasili na hivyo kueneza uzuri wa nchi yetu na ukarimu wa watu wake na hivyo wahudumiwe vilivyo,” alisema Devotha kwa hisia kubwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here