27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TRA WATOA MAFUNZO WAFANYABIASHARA WA KICHINA  KARIAKOO

Na KOKU DAVID


KATIKA mwendelezo wa kutoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara mbalimbali na wadau wa kodi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hivi karibuni imekutana na wafanyabiashara wa China wanaofanyabiashara zao katika mkoa wa Kodi Kariakoo wilayani Ilala.

TRA kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sofia Mjema, waliendesha semina ya siku moja kwa wafanyabiashara hao ili kuwawezesha kujua masuala mbalimbali ya kodi.

Katika semina hiyo,  zaidi ya wafanyabiashara 100 ambao ni raia wa China walishiriki na kwamba huo ni muendelezo wa mikakati ya TRA kuhakikisha inatoa elimu ya kodi kwa wadau na wafanyabiashara nchini.

Sambamba na elimu ya kodi, wafanyabiashara hao walipata nafasi ya kuuliza maswali pamoja na kueleza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo pindi wanapokuwa katika maeneo yao ya biashara.

Lengo kuu la semina hiyo kuwaelimisha wafanyabiashara hao wa kigeni ambao hawazijui sheria na taratibu za kodi.

Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Diana Masalla anasema kuwa kabla ya kumchukulia hatua mlipakodi, TRA imejiwekea utaratibu wa kumuelimisha kuhusiana na sheria mbalimbali za kodi na baada ya hapo itachukua hatua iwapo atakiuka.

Anasema katika semina hiyo waliwahusisha wafanyabiashara raia wa China ambao wanafanya biashara zao katika mkoa wa kodi wa Kariakoo uliopo  katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Anasema walitoa elimu ya kodi katika nyanja mbalimbali kutokana na kuwa baadhi ya wafanyabiashara hao wametoa ajira lakini hawalipi kodi ya mapato inayotokana na ajira waliyoitoa kwa kile wanachodai kutojua sheria za kodi zinawataka kufanya hivyo. Lakini kutojua sheria sio jawabu zuri kwa kutokulipa kodi kwani  kuielewa sheria ya Kodi ni jukumu la kila mlipa kodi.

Anaongeza kuwa kwa wafanyabiashara ambao wameajiri wafanyakazi zaidi ya wanne wanatakiwa kulipa kodi ya uendelezaji ufundi stadi kwa ajili ya kuichangia serikali kuendeleza vyuo vya ufundi.

Anasema, pia wakiwa kama wafanyabiashara wanatakiwa kulipa kodi kulingana  na biashara wanazofanya kama ambavyo sheria inawataka.

Diana anasema hivi sasa wafanyabiashara wengi kutoka China wamekuwa wakitumia kigezo cha kutokuzijua Sheria na kwamba kama Mamlaka wameweka mikakati ya kuhakikisha inatoa elimu kwa kila mfanyabiashara.

Anasema katika semina hiyo, TRA imekutana na wafanyabiashara hao wa China ambao wanafanyabiashara zao Kariakoo kwa mara ya kwanza na kwamba itaweka  utaratibu wa kuwa inakutana nao mara mbili kwa mwaka ili kuwaelimisha sheria mbalimbali za kodi ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya sheria hizo ambayo hujitokeza.

Anasema mafunzo yaliyotolewa katika semina hiyo ni elimu ya kodi ya mapato inayotokana na biashara, uwekezaji, ajira pamoja na upande wa ushuru wa forodha ambako wamefundisha kuhusu taratibu za kuondosha mizigo bandarini.

Anaongeza kuwa katika ushuru wa forodha wametoa mafunzo yatakayowawezesha kujua ushuru wa forodha watakaotakiwa kulipa ikiwa ni pamoja na kodi ambazo atatakiwa kulipa pamoja na kujua aina za misamaha iliyopo katika kodi.

Utaratibu wa kutoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara wanaotokea China utakuwa endelevu kutokana na kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa wakija nchini  kwa uwingi kwaajili ya biashara karibu kila siku.

Sambamba na kutoa elimu ya kodi, TRA kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji itakuwa ikifuatilia kujua idadi ya wafanyabiashara wa kigeni waliofika nchini kwaajili ya biashara ili kuisaidia kujua kodi wanayoweza kupata kutoka kwa wafanyabiashara hao ikiwa ni pamoja na kupanga mipango yake ya maendeleo kwa jamii.

Diana anasema TRA inawataka wafanyabiashara wote wa kigeni anatakiwa kujua taratibu za nchi pamoja na sheria za kodi zinamtaka kufanya nini ikiwa ni pamoja na kuzifuata ili kuepuka adhabu.

Pamoja na kufuata sheria za kodi, kila mfanyabiashara anatakiwa kuhakikisha anatoa risiti kwa kila huduma anayotoa kwa mteja wake kama sheria inavyowataka kufanya ili kuepuka faini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles