24 C
Dar es Salaam
Saturday, May 4, 2024

Contact us: [email protected]

TANZANIA INA UHABA WA MADAKTARI BINGWA 2,000

 

 NA VERONICA ROMWALD- DAR ES SALAAM


TANZANIA inakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa kwa asilimia 82, imebainishwa.

Kutokana na hali hiyo ili kuweza kukidhi mahitaji hayo inahitaji kuwa na madaktari bingwa 2,453 wa fani mbalimbali ambapo kwa sasa waliopo ni 451 tu ambao wanahudumia nchi nzima.

Taarifa hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Obadia Nyogole  mbele ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan katika kongamano la 49 la Afya Kitaifa na Mkutano Mkuu wa mwaka wa chama hicho.

“Tuna upungufu wa madaktari bingwa kwa kiwango cha asilimia 82. Hali hii si nzuri, tunaamini katika weledi na uadilifu lakini bila kuendeleza wataalamu hatuwezi kufika mbali,” alisema.

Dk. Nyogole aliishauri Serikali kuwapatia ufadhili madaktari pindi wanapohitaji kujiendeleza ili kuweza kukabiliana na hali hiyo.

“Hivi tunavyozungumza, kuna takriban madaktari 127 ambao wameomba na kukubaliwa katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwenda kujiendeleza katika taaluma za kibingwa lakini wameshindwa na hawana uhakika wa kwenda masomoni kwa kukosa udhamini.

“Hivyo, tunaiomba serikali iendelee kusomesha wataalamu kama ambavyo imeahidi katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015, tunashauri itenge fungu maalumu (fedha) kwa ajili kusaidia pale ambapo madaktari wanahitaji kujiendeleza,” alisema Dk. Nyongole

Mwenyekiti huyo wa MAT ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Mfumo wa Mkojo (Urolojia), aliiomba serikali pia kuangalia upya masilahi ya wataalamu wa afya ili kila mmoja apewe malipo kulingana na taaluma aliyosoma.

“Tunashauri kila Mtanzania awe na bima ya afya na bima hizo zilipe kwa wakati ili vile vituo vinavyohudumia viweze kutoa huduma kwa ufasaha, Serikali pia ianzishe mfuko maalumu na upate mapato kutoka kwenye tozo mbalimbali mfano madini, mafuta kulingana na wataalamu wa uchumi watakavyoshauri basi fedha hizo zisaidie yale makundi maalumu,” alishauri.

Alisema MAT inaunga mkono hatua ya Serikali kupeleka muswada wa sheria ya madaktari kwani  imelenga kusaidia kulinda weledi wa  taaluma hiyo ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma bora.

“Tunaamini Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu itakapofika wakati wa kutunga kanuni, atatushirikisha ili tutoe maoni yetu yatakayosaidia kuboresha zaidi ili sheria hiyo iwe na manufaa kwa wote,” alisema.

 

MAKAMU WA RAIS

Akizungumza  katika mkutano huo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema Serikali itaendelea kufadhili na kuwezesha wataalamu wa afya kujiendeleza kitaaluma.

Alisema pia itashughulikia suala la kuwa na mtihani mmoja kwa watahiniwa wa vyuo vyote vya afya nchini.

“Hili limezingatiwa katika Sheria ya Madaktari, iliyopitishwa Septemba, mwaka huu, tutaendelea kusomesha wahadhiri na wataalamu wa fani zenye uhitaji mkubwa wa kitaaluma ambazo hazijawahi kufundishwa nchini hasa masomo ya ‘Geriatricks’, physiotherapia na mengineyo,” alibainisha.

Aliongeza “Tumekwisha kuchukua hatua, kuhakikisha walimu wanaoajiliwa kama wahadhiri katika vyuo vikuu ni lazima wawe na ufaulu wa GPA kuanzia 3.8, na tunafikiria (bado tunajadili ndani) kuanza kutoa ‘scholaship’ kwa wale ambao wanafanya mafunzo ya ubobezi.

Alisema katika kuboresha masilahi ya wataalamu wa afya hasa madaktari, serikali imeongeza viwango anavyolipwa daktari mmoja kwa kumuona mgonjwa ambaye ni mwanachama wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

“Kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa Daktari Bingwa alikuwa akilipwa Shilingi 2,000 na sasa analipwa 15,000, daktari wa kawaida alikuwa akilipwa Shilingi  2,000 sasa analipwa 7,000.

“Kwa upande wa hospitali za wilaya, daktari wa kawaida alikuwa akilipwa Sh 1,000 sasa analipwa Shilingi 7,000, tumechukua hatua hii ili kuwavutia madaktari nchini kufanya katika hospitali za mikoa na Wilaya,” alisema.

Alisema ili kukabiliana na upungufu wa wataalamu wa afya nchini Serikali imetoa vibali vya ajira mpya vipatavyo 3,410.

“Katika awamu ya kwanza vibali vya madaktari 258 vilitolewa na awamu ya pili vibali 3,150 kwa wataalamu wa kada mbalimbali za afya vimetolewa na taratibu za ajira zimekamilika hatua inayofanyika sasa ni uhakiki wa vyeti katika Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA),” alibainisha

Alisema ili kukabiliana pia na ongezeko la gharama za matibabu kwa wananchi tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kuandaa mswada wa bima ya afya kwa wote, ambao utamlazimu kila Mtanzania kuwa mwanachama wa bima ya afya.

Alisema hatua hiyo itasaidia kumuondolea mwananchi usumbufu wa kutokupata matibabu pindi unapokuwa anazihitaji.

“Tunaendelea kuchukua hatua za makusudi za kuwatambua wazee wasiojiweza wenye umri wa miaka 60 na zaidi katika halmashauri zote nchini ili wapatiwe vitambulisho vitakavyowawezesha kupatiwa huduma za afya bila malipo.

“Kwa mujibu wa sera pia, tunayo makundi maalumu mfano watoto chini ya miaka mitano na wajawazito ambao nao wanahitaji kupata huduma bila malipo. Serikali imeendelea kuimarisha hali ya  upatikanaji dawa nchini kutoka asilimia 45 hadi kufikia asilimia 86.3 Julai, mwaka huu,” alisema

Alisema kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuboresha na kuanzisha huduma za kibingwa zilizokuwa hazipatikani nchini idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya  nchi kutibiwa imepungua kutoka 423 mwaka 2015/16 hadi 203 mwaka 2016 /17 sawa na asilimia 47.9.

Awali, Waziri Ummy alikemea tabia ya viongozi mbalimbali wa serikali ambao wamekuwa wakichukua hatua bila kufuata utaratibu uliopo dhidi ya wataalamu wa afya.

“Kuliibuka tabia ya wakuu wa mikoa, wilaya kuwaweka ndani madaktari kwa makosa ya kitaalamu, hili nimelisema na narudia unakuta mkuu wa wilaya, mkoa wanawaweka ndani.

“Juzi nimepigiwa simu eti mama amefariki, kwanini msiwapeleke kwenye baraza la madaktari au la wakunga huko ndipo itajulikana ni kosa la kitaalamu au laa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles