25.3 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA, YANGA PRESHA JUU

 

ADAM MKWEPU Na JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM

HOMA ya pambano la watani wa jadi katika soka la Tanzania, Simba na Yanga, inazidi kupanda huku kila timu ikijinadi kwa upande wake kuelekea katika mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Timu hizo tayari zimeanza maandalizi ya kuelekea kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kubeba hisia za mashabiki wengi wa soka nchini, ambapo Simba wako visiwani  Zanzibar wakati Yanga imejichimbia Morogoro.

Kocha wa Yanga, George Lwandamina,  atakiongoza kikosi chake akiwa na kumbukumbu ya kushindwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii Agosti 23, mwaka huu walipokabiliana na Simba na kufungwa kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Kocha huyo ameshindwa kutamba katika michezo yote aliyokutana na kocha wa Simba, Joseph Omog, ukiwemo wa ligi kuu msimu uliopita Simba ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Omog aliiongoza tena Simba kuifunga Yanga kwa penalti 4-2 kwenye Kombe la Mapinduzi mwaka huu, kabla ya kuibuka tena na ushindi wa penalti 4-3 kwenye Ngao ya Jamii.

Timu hizo zote zimekusanya pointi 15 baada ya kucheza michezo saba ya ligi hiyo, huku Simba ikiongoza msimamo   kutokana na kufunga mabao mengi, ambapo imezifumania nyavu mara 19, huku Yanga wakiwa na mabao 10.

Akizungumza na MTANZANIA jana,  Omog alisema Yanga ni timu nzuri lakini kikosi chake ni bora zaidi ya mabingwa hao watetezi ambao wanalifukuzia taji la nne mfululizo la ligi hiyo.

“Nimeifunga Yanga mara mbili na kutoka sare mara  moja katika mechi sita nilizocheza nao nikiwa kocha wa Simba, kwa hiyo najivunia rekodi hiyo ambayo naamini itanibeba na kupata matokeo mazuri katika mechi ya Jumamosi na hata mechi nyingine za ligi na michuano mengine,” alisema Omog.

Kocha huyo alisema kambi yao ya Zanzibar itakuwa ni maalumu kwa ajili ya kuwaweka sawa wachezaji wake na kuwakumbusha mambo muhimu yatakaowasaidia kupata ushindi na kujilinda ili wasipoteze mchezo.

Omog alisema anawajua Yanga lakini si timu tishio kwake kutokana na ubora wa safu ya ushambuliaji na ulinzi imara aliyoandaa dhidi ya mshambuliaji, Ibrahim Ajibu,anayeonekana kuwa moto wa kuotea mbali kutokana na aina ya mabao aliyofunga katika mechi zilizopita.

Mkuu wa Kitengo cha Habari wa klabu Yanga, Dismas Ten, alisema hawana hofu wala presha kuelekea kwenye mechi hiyo kwa sababu wanashiriki ligi ili kusaka ubingwa.

“Simba wakienda kuweka kambi Zanzibar hayo ni mapendekezo yao, si lazima tuwafuate huko ingawa mara nyingi imekuwa hivyo, sisi tunapambana kupata matokeo mazuri yatakayotuwezesha kutetea taji letu.

“Hatushiriki ligi sababu ya Simba, kwani nao ni moja ya timu 16 zinazoshiriki ligi kuu, ndio maana kila kikosi kinapambana kwa hali na mali kufanya vizuri,” alisema Ten.

Ten alieleza wanachokitegemea wao ni kupata matokeo ya kuridhisha, kupitia kwa wachezaji wao ambao wamepewa jukumu la kuhakikisha kikosi chao kinatoka uwanjani na ushindi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles