24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 4, 2024

Contact us: [email protected]

TANESCO YAJIPANGA KUELEKEA UCHUMI WA KATI, VIWANDA

*Waja na maboresho kabambe kwa jiji la Dar es Salaam

Na MWANDISHI WETU


KAMA inavyofahamika, Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwa kujenga uchumi wa viwanda, kumekuwa na ukuaji wa kasi wa miji mikuu ya mikoa pamoja na miji mashuhuri ya  kibiashara kama inavyoonekana katika miaka ya hivi karibuni, katika jiji la Dar es Salaam.

Jiji la  Dar es Salaam limekuwa likikua kwa kasi, ikiwamo ujengwaji wa majengo makubwa yanayohitaji umeme mkubwa kuweza kuhimili uendeshwaji wa mitambo mbalimbali itumikayo katika majengo hayo, pia kumekuwa na ongezeko kubwa la uanzishwaji wa viwanda katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na miji mingine.

Takwimu za hivi karibuni kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara inaonesha katika jiji la Dar es Salaam pekee, idadi ya viwanda vilivyoanzishwa katika mwaka 2009 pekee ni 378, kati ya viwanda 733 vilivyoanzishwa katika miji mbalimbali  nchini na ukuaji huu wa kasi umepelekea jiji la Dar es Salaam  kuwa na mahitaji makubwa zaidi ya umeme, pengine kuliko miji yote katika nchi yetu.

Kwa kuzingatia ukuaji huu wa kasi wa Jiji la Dar es Salaam, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanya mabadiliko makubwa sana katika uboreshaji wa miundombinu katika jiji, hii ni kutokana na ukweli kwamba, mahitaji ya umeme katika jiji la Dar es Salaam yameongezeka zaidi hadi kufikia Megawatt 474, ambayo ilifikiwa mwaka 2016, ikilinganishwa na Megawatt 358.8 ambazo zilitumika mwaka 2009.

Kutokana na ongezeko hilo la mahitaji ya umeme, Tanesco imefanya maboresho katika maeneo mbalimbali katika miundombinu ya umeme, miongoni mwa miradi mikubwa iliyokamilika ni ule wa Uboreshwaji wa Miundombinu ya umeme ya Jiji la Dar es Salaam.

Huu ni mradi mpya kabisa ambao umebadilisha njia ya usambazaji umeme katika Jiji la Dar es Salaam kutoka mfumo wa zamani wa usafirishaji umeme kupitia juu ya ardhi (overhead distribution lines) kwenda katika mfumo wa usambazaji umeme kupitia chini ya ardhi, underground distribution lines, njia hii ni salama zaidi,  inawezesha matumizi mazuri zaidi ya mazingira, kwani hakuna tena hitaji la kupitisha nyaya kwa kutumia nguzo.

Mfano mzuri ni ujenzi wa laini ya Msongo wa Kilovolti 132 kutoka katika Kituo cha  kupozea umeme cha katikati ya Jiji hadi kituo cha kupozea umeme cha Makumbusho, njia hii ya umeme imejengwa chini ya ardhi, ikiambaa katika kingo za Barabara ya Ali Hassan Mwinyi hadi kilipo Kituo cha Makumbusho.

Pia katika mradi huu kimejengwa kituo cha kupozea umeme chenye uwezo wa kupokea Megawatt 150, hali ambayo imeboresha zaidi upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo ya katikati ya jiji la Dar es Salaam, sambamba na mradi huu kimejengwa kituo cha kisasa kabisa cha kudhibiti mifumo ya umeme katika jiji la Dar es Salaam, kituo hiki kimejengwa eneo la Mikocheni.

Katika Mkoa wa Kitanesco wa Kinondoni Kaskazini, kuwapo kwa kituo hiki kumerahisisha zaidi kazi za mafundi wa Tanesco kuweza kubaini maeneo ambayo  yana hitilafu, hivyo kuwezesha kuyafikia maeneo hayo na kutatua tatizo lililosababisha umeme kukatika.

Tanesco haikuishia hapo, imejenga na kukarabati vituo vya kupozea umeme pamoja kuviongezea uwezo vituo hivyo ili kukabiliana na changamoto ya usambazaji umeme katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam.

Miongoni mwa vituo vilivyoboreshwa ni Kituo cha Kupozea Umeme cha Kariakoo, ambacho kimeongezewa uwezo kwa kuwekewa transfoma kubwa zenye uwezo wa 30MVA kutoka zile za zamani zilizokuwa na uwezo wa 15MVA, hii imeongeza ubora wa upatikanaji wa umeme katika eneo la biashara la Kariakoo. Kituo cha Sokoine ambacho kipo karibu  na eneo la Chuo cha IFM pia kimeboreshwa na kuongezewa uwezo kufikia uwezo wa 50MVA kutoka 15MVA za awali, hivyo kuboresha upatikanaji wa umeme katika maeneo ya katikati ya Jiji.

Pia kwa ufadhili wa Serikali ya Japan, Tanesco inaendelea na upanuzi na ukarabati wa kituo kikubwa cha kupozea umeme cha Ilala, kilichopo eneo la Karume. Kituo hiki kikubwa na cha kisasa kabisa kitaongeza uwezo Manispaa ya Ilala, hususan katika uwekezaji wa viwanda, kwa kuwezesha kusambaza umeme wa uhakika katika eneo la viwanda la Ilala.

Kwa upande wa maeneo ya Kurasini hadi Kigamboni, hususan maeneo ya viwanda ya Kurasini, pia kumejengwa kituo kipya cha kupozea umeme na kuwekwa transifoma kubwa yenye uwezo wa 50MVA, kituo hiki kinapokea umeme wa Msongo wa Kilovolti 132/33/11, ili kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo ya viwanda yaliyo Kurasini hadi maeneo yote ya Wilaya Mpya ya Kigamboni.

Mbagala pia kumejengwa kituo kipya kabisa cha kupozea umeme cha Msongo wa Kilovolti 132/33/11, hii ni kutokana na ongezeko la mahitaji ya umeme ya maeneo  ya viwanda kuanzia Temeke, Mbagala hadi Mkuranga.

Jitihada zote hizi ambazo Serikali ya Awamu ya Tano, imekuwa ikizifanya kupitia Wizara ya Nishati na Madini ni  ushahidi tosha kuwa Serikali hii imedhamiria kwa dhati kufanya mapinduzi ya viwanda katika nchi yetu na kwa mifano tunaona jiji la Dar es Salaam linavyokua na kuimarika kiuchumi.

Mwisho

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles