24.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 8, 2022

Tambwe kuikosa Azam FC Jumapili

amissi-tambweNa THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga, Amissi Tambwe, ataukosa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC utakaochezwa Jumapili Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Tambwe analazimika kukaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki mbili hadi tatu kutokana na majeraha aliyopata katika mchezo wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar juzi uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mshambuliaji huyo raia wa Burundi alipata majeraha ya kuchanika kichwani baada ya kugongana na nahodha wa Mtibwa Sugar, Shaban Nditi.

Tambwe mwenye mabao manne msimu huu alikimbizwa katika zahanati iliyopo karibu na uwanja baada ya kuumia na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa ya daktari wa timu hiyo, Edward Bavu, Tambwe ameshonwa nyuzi tano kutokana na jeraha alilopata kichwani huku akiendelea kutumia dawa za kukausha kidonda.

Hii ni mara ya pili kwa Tambwe kupata majeraha sehemu ya kichwani, kwani aliwahi kuumia sehemu hiyo na kushonwa nyuzi tatu wakati Yanga ilipokwenda kuweka kambi nchini Uturuki kujiandaa na michuano ya kimataifa.

“Tambwe atalazimika kuwa nje ya uwanja kwa muda ili aweze kupona haraka, lakini baadaye ataanza kufanya mazoezi mepesi kujiweka fiti ili asipoteze uwezo wake,” alisema Bavu.

Kitendo cha kuumia kwa Tambwe ni pigo kwa kikosi cha Yanga ambacho kinapambana kutetea ubingwa wake msimu huu, kutokana na umuhimu wa mchezo wa Jumapili.

Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, mara nyingi amekuwa akimpanga Tambwe kuanza kikosi cha kwanza kutokana na umahiri wake wa kupachika mabao, lakini sasa atalazimika kutafuta straika mbadala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,235FollowersFollow
549,000SubscribersSubscribe

Latest Articles