31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

Muhongo ateta na Balozi wa Canada

picmuhongoNa TERESIA MHAGAMA

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amekutana na Balozi mpya wa Canada nchini, Ian Myles na kuzungumzia masuala mbalimbali ya uendelezaji wa sekta za nishati na madini nchini.

Kikao hicho kilifanyika jana ofisi za wizara hiyo jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara ya kwanza kwa balozi huyo kufika wizarani tangu alipowasili nchini, Agosti mwaka huu.

Wakati wa mazungumzo hayo, Balozi Myles alimweleza Profesa Muhongo, kuwa nchi hiyo imeshiriki katika shughuli mbalimbali za uendelezaji wa sekta za nishati na madini nchini na kutoa mfano ushiriki wao kupitia Shirika la Maendeleo la Canada (CIDA) ambapo walikuwa wakitoa fedha kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) kuanzia mwaka wa fedha wa 2012/2013  hadi 2015/2016.

“Katika Mpango wa Uhamasishaji Uwazi katika Mapato ya Madini, Gesi Asilia na Mafuta (TEITI), Canada ilisaidia mchakato wa maandalizi ya kupata sheria ya kuongoza sekta hiyo.

“Pia, tunawajengea uwezo wataalam ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi,” alisema Myles.

Pia, balozi huyo alisema Tanzania ni moja ya nchi zinazopewa kipaumbele na Serikali ya Canada katika masuala  mbalimbali ikiwamo utoaji wa misaada ya kifedha.

Kwa upande wake, Waziri Muhongo alisema kuwa, uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulianza tangu miaka ya 1960 na kwamba nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali ikiwamo kilimo na elimu.

“Katika sekta ya madini, kampuni kubwa zinazofanya shughuli za uchimbaji wa madini nchini, nyingi zinatoka Canada na mfano halisi ni kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia.

Kuhusu uendelezaji wa Chuo cha Madini Dodoma (MRI), Profesa Muhongo alimwambia Balozi Myles, kuwa mazungumzo kati ya wizara yake na ubalozi wa Canada kuhusu kukiendeleza chuo hicho yalishaanza.

“Tunataka chuo hicho kiwe cha kimataifa,  kisiwe kinatambulika hapa nchini tu na pia kiwe kinabadilishana wataalam na vyuo vingine vya nje ili kuboresha elimu inayotolewa katika taasisi hiyo,” alisema.

Pia alizitaka kampuni kutoka Canada kuja kuwekeza nchini kwa kuwa Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles