Na HERIETH FAUSTINE
TIKITI maji ni tunda ambalo kisayansi huitwa Citrullus lanatus. Tunda hili hutokana na mmea unaotoa maua ambayo humea kwa kutambaa.
Mmea huo hutoa matunda makubwa yaliyo na umbo la tufe au yai na asili yake ni kusini mwa Afrika.
Watu wengi huamini kuwa tikiti maji ni tunda lililo na maji na sukari pekee, lakini ukweli ni kwamba lina virutubisho vingi. Tikiti maji lina vitamini, madini na viondoa sumu (antioxidants).
Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa ulaji wa vyakula vitokanavyo na mimea kama tikitiki maji na mbogamboga, hupunguza hatari ya kupata magonjwa, pia huboresha maisha na kuongeza umri wa kuishi.
Tafiti za awali zimeonyesha kuwa watu wanaokula matunda ya aina hii – yenye lycopene kwa wingi wanaweza kuwa na nafasi ndogo ya kupata maradhi ya saratani hususani ya tezi dume.
Utafiti uliochapishwa mwaka 2013 nchini Marekani, ulibainisha kuwa ulaji wa tikiti maji kwa watu wazima walio na uzito mkubwa uliweza kupunguza shinikizo la damu la aota (aortic BP).
Pia tunda hili limejipatia umaarufu kutoka kwa watu walio katika ndoa, kwa kuwa na nitric oxide amabyo huongeza mzunguko wa damu katika viungo vya uzazi.
Kwa wana michezo, ulaji wa tunda hili au juisi yake ni wa faida kubwa kwani husaidia kupunguza maumivu ya misuli na kuondokana na uchovu kwa haraka.
Tikiti maji ni tunda muhimu katika kurekebisha mmeng’enyo, hii ni kwa sababu limetengenezwa na kiasi kikubwa cha maji na fiber ambayo husaidia kuondoa matatizo ya kukosa choo (constipation).
Kwa wagonjwa walio na upungufu wa maji mwilini, tunda hili ni muhimu kwao kutokana na kuwa na asilimia 92 ya maji na madini.
Pia husaidia afya ya ngozi kwa kuwa lina vitamini A na C. Vitamini A husaidia ukuaji wa tishu za mwili, ikiwamo ngozi na nywele, wakati Vitamini C husaidia katika utengenezaji wa kolageni mwilini. Pia huponya haraka tishu zilizo na majeraha ikiwamo ngozi.
Kwa upande wa mbegu za tikitiki maji, zina faida kubwa kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha protini.
Pia mbegu hizo zina vitamin B ambayo ni muhimu mwilini kwani husaidia kubadili chakula kuwa katika mfumo wa nishati.
Vilevile mbegu hizo zina uwezo mzuri wa kusaidia mmeng’enyo wa chakula pamoja na mfumo wa fahamu, huku zikisaidia pia kuimarisha afya ya ngozi kwa mtumiaji.