22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

SUMATRA CCC: WANAOKATISHA RUTI WANAWATESA ABIRIA

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


SERIKALI ipo katika mkakati wa kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara na reli ili iwe ya kisasa ambayo itasaidia kuleta maendeleo kwa kasi.
Mabadiliko hayo japokuwa yana maumivu kwa wananchi ambao wamekumbwa na bomoabomoa, yatasaidia kuchochea uchumi wa nchi.


Mkakati huo wa Serikali ndio uliolisukuma Baraza la Ushauri kwa Watumiaji Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra Ccc), kuona umuhimu wa kuzunguka katika baadhi ya mikoa mbalimbali nchini kuelimisha wananchi ili kuweza kukabiliana na mabadiliko.
Sumatra Ccc ilianzishwa kwa mujibu wa sheria namba 9 ya mwaka 2001 ambayo pia ndiyo iliyoanzisha Mamlaka ya Udhibiti ya Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).


Sheria hiyo inaanzisha taasisi mbili, kila moja ikiwa huru na inayojitegemea kimuundo, kimajukumu, kimalengo, kimaamuzi na kiutendaji.


Sumatra Ccc iko chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambapo lengo kuu la baraza ni kuwa kiungo baina ya watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na Sumatra, watoa huduma, Sumatra yenyewe na Serikali.


Majukumu ya Sumatra Ccc ni pamoja na kuwasilisha maslahi ya watumiaji kwa kuwasilisha maoni na taarifa mbalimbali, kushauriana na Sumatra, Waziri mwenye dhamana ya kusimamia uchukuzi na mawaziri wa sekta nyinginezo.
Pia kupokea na kusambaza taarifa na maoni mbalimbali kuhusu masuala yanayowagusa watumiaji huduma zinazodhibitiwa na Sumatra na mengineyo.


Ofisa Habari kwa Umma wa Sumatra Ccc, Nicholous Kinyariri anasema baraza hilo limeangalia umuhimu wa majukumu yake kwa jamii na kuona haja ya kutoa elimu ya mabadiliko ya miundombinu ya barabara na reli.
Anasema jamii ni vyema ikapewa elimu ya kutosha kuhusu mabadiliko ya miundombinu ili kupunguza ajali pamoja na kuhamasisha wasafiri kubadilika na kwenda na muda.


Hapo awali abiria walijenga mazoea ya kuchelewa vituoni lakini kwa sasa ni vyema wajiandae kubadilika kwa kuwahi vituoni kama ambavyo usafiri wa treni ulivyo au mabasi yaendayo kasi ambayo hayana muda wa kupoteza vituoni," anasema Kinyariri.
Anasema wameamua kutoa elimu ya haki za watumiaji huduma za usafiri katika ulimwengu wa kidigitali.
Pia anasema wamefanya kampeni ya kuelimisha wananchi 940 ili waone umuhimu wa mabadiliko hayo.


Anasema kwa upande wa Mkoa wa Dodoma wameelimisha vijana jinsi ya kufahamu haki na wajibu pindi wanapokuwa safarini.
Anaongeza kuwa kwa upande wa Mkoa wa Tabora, wameelimisha watu 40 wenye mahitaji maalumu.
Kinyariri anasema wamebaini changamoto wanayokabiliana nazo wenye mahitaji maalum ndani ya vyombo vya usafiri binafsi ikiwamo kuchajiwa baiskeli zao.


"Katika mazungumzo na kundi hili wamelalamikia kutozwa fedha pindi wanapopanda magari huku wakilazimishwa kuzishusha baiskeli zao endapo ikitokea hawana fedha,” anasema Kinyariri.


Anasema kitendo hicho ni sawa na kukatwa miguu yao au kuchajiwa fedha kwani na wao ni kiungo muhimu wanachokitegemea.
Kinyariri anasema pia wameelimisha wenyeviti wa serikali za mitaa 113 ili kulinda haki za abiria pamoja na tabia ya ukatishaji ruti ambayo imeenea katika maeneo mbalimbali nchini.


“Tabia ya ukatishaji ruti imekuwa ikichangia wananchi kuteseka na kutumia fedha nyingi kwenye usafiri jambo ambalo si sahihi, inatakiwa kila mtu alipigie kelele jambo hili,” anasema Kinyariri.


Anasema mkoani Arusha wamewajengea uwezo vijana wawe watoa taarifa pindi panapotokea tukio.
Kinyariri anasema Mkoa wa Mbeya wametoa elimu kwa vijana katika stendi kuu ili waweze kuachana na tabia ya kusumbua wapiga debe na kuwanyang’anya mali zao.


“Suala la wapiga debe katika stendi Kuu ya Mbeya ni kero abiria wengi wanalalamika hulazimika kupanda magari wasiyoyapenda kwa sababu ya kulazimishwa na wapiga debe,”anasema Kinyariri.
Anasema pia wametoa elimu kwa vijana wa sekondari 300 katika Mkoa wa Dar es Salaam ili waweze kupaza sauti ili nchi iwe na usafiri wa uhakika.


Anaongeza kuwa, Sumatra CCC imeona haja ya kutumia mbinu za kuelimisha jamii ili kujenga uelewa utakaoibua hoja ambazo serikali itazisikia na kuzitatua.
“Tunaomba jamii isikae kimya ijitahidi kuibua hoja na kupaza sauti ziwafikie viongozi ambao wanaweza kuchukua hatua,” anasema Kinyariri. 
mwishooo

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles