22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

UHUSIANO WA KIMAPENZI UNAVYOWEZA KUANZISHWA BILA KUTARAJIWA 

Na CHRISTIAN BWAYA


WIKI iliyopita tuliona ni jinsi gani uhusiano wa kimapenzi unavyoweza kuanzishwa bila kutarajiwa na wahusika wakajikuta wakiangukia kwenye penzi zito.
Tunaendelea na makala hii ambapo leo tutazungumzia mambo kadhaa yanayoweza kuendeleza uhusiano mpya. 

Mambo yanayoendeleza uhusiano mpya

Wataalamu wa masuala ya uhusiano wanasema, baada ya mtu kuvutiwa na mtu fulani, ni kawaida kufanya juhudi za kumvutia kwa kujaribu kujenga taswira chanya ili mlengwa naye avutiwe. Kanuni nne kubwa zinazosaidia kuwafanya watu wawili waanze kuwa karibu kihisia na bila kukwaruzana ni:
•    Kwa kawaida, watu hujenga uhusiano na wale wanaowafanya wajisikie vizuri. Na kadri mtu anavyojisikia vizuri, ndivyo anavyovutiwa nawe. Kinyume chake, ni kujisikia mzigo na hivyo kuongeza uwezekano wa uhusiano kusonga mbele. Kwa mfano; mwanamke hujisikia vizuri anapokuwa na mwanamume anayemfanya ajisikie kuwa mzuri na wa maana. 
•    Watu wana kawaida ya kukupa kile unachowapa, hivyo mtu anayeonesha kuvutiwa na wewe, hukufanya ujisikie kuvutiwa naye na kutamani kutumia muda mwingi kwake. Hujisikia kuchoka pale unapompenda asiyeonesha kukupenda. Kwa hiyo, mtu humpenda zaidi yule anayempenda.
•    Watu unaofanana nao imani, mitazamo na misimamo hupendana zaidi kuliko wale wanaotofautiana kiimani, mitazamo na misimamo. Kufanana kunakoambatana na mvuto wa kimwili, huchochea mvuto. Mvuto huo huchochea kufanana. Hata hivyo, watafiti wanasema; zipo tofauti za kihaiba ambazo kwa kawaida huchochea kuvutiana. Mfano mtu mzungumzaji hujisikia kuvutiwa na mtu anayeweza kumsikiliza na si yule anayetaka kuzungumza kama yeye.
•    Kumwamini unayevutiwa naye, humfanya avutike kwako. Hii hutegemea kiwango cha usalama wa kihisia unachokuwa nacho wewe na kiwango hicho hicho cha usalama anachokuwa nacho yeye. Kutokuwa salama kihisia kunamaanisha ama kutokujiamini, kutokuamini wengine au vyote viwili, ambavyo huathiri kwa kiasi kikubwa uhusiano.
Je, unaweza kuhusiana na mtu yeyote?

Jibu ni ndio. Tafiti zinathibitisha kuwa inawezekana kuhusiana na mtu yeyote anayeweza kukufanya ukajisikia kupata mahitaji yako ya kihisia na kukusababisha na wewe uweze kutambua na kujibu mahitaji yake ya  kihisia. Kwa muhtasari tu, tunazungumzia namna gani mwanaume anamfanya mwanamke ajisikie kupendwa na hivyo kumhamasisha mwanamke huyo kumpa mamlaka anayostahili.

Kama tulivyoona awali, ukaribu na mtu hata asiyekuvutia unaweza kuamsha hisia za kuvutiwa kadri unavyoonana naye na namna mtu huyo anavyoweza kuonekana kuelewa na kujibu mahitaji yako ya kihisia. Tunaambiwa, sura unayoweza kuiita mbaya, inapoambatana na jitihada za kutambua na kuelewa mahitaji yako ya kihisia, mitazamo na imani inayofanana na ya kwako, inayokufanya ujisikie vizuri, basi, hatua kwa hatua ubaya wa sura hiyo uliouona awali, hupotea na kugeuka kuwa uzuri.

Vile vile, namna gani uhusiano unakupa kipimo kinachofanana na kile ulichowekeza kwenye uhusiano na hivyo kujenga hali fulani ya usawa, ndivyo uhusiano huo unavyoimarika na kudumu. Watu hawapendi kuonekana wanagharimika zaidi kwenye uhusiano kuliko huyo wanayehusiana naye. Inawafanya wajisikie kubeba mzigo. 


Kwa mfano, mwanaume asiye na elimu, anapoanzisha uhusiano na mwanamke anayemzidi kielimu, huweza kujikuta katika mazingira ya kutokujiamini. Ili ajisikie vizuri, yaani ajiamini, kwa kujua au kutokujua, mwanamume huwa na kingine kinachofidia tofauti hiyo ya elimu ili kudumisha uhusiano huo. Inaweza kuwa uwezo wa kifedha, umaarufu na kadhalika. 

Kwa hiyo, inawezekana kuhusiana na mtu yeyote. Na kwa hakika, si kweli kwamba uhusiano bora huwezekana unapokutana na watu sahihi. Kama tulivyoona uhusiano wowote huanza kwa njia ya nasibu, kutegemeana na uliko na unayeonana naye. Kinachowaunganisha watu wawili kimapenzi ni namna wanavyoweza kuelewa na kuitikia ipasavyo mahitaji yao ya kihisia.
Kwamba, mtu sahihi ni matokeo ya mtazamo, imani na matarajio yako. Mtu sahihi kwenye uhusiano ni wewe na si huyo unayeonana naye. 

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles