HUENDA nia ya nyota wa timu ya Atletico Madrid, Antoine Griezmann na Saul Niguez kutua ligi pendwa ya England ikafanikiwa iwapo kocha wao, Diego Simeone, atashindwa kuongeza mkataba wa kuifundisha timu hiyo baada ya kumalizika mwaka 2018.
Simeone amepunguza mkataba wa kuifundisha timu hiyo hadi mwaka 2018 na kuna kila dalili ya kuihama ingawa bado suala hilo halijawa wazi.
Klabu ya Chelsea kwa muda mrefu wamekuwa wakimfuatilia kwa karibu Griezmann wakati Manchester United mara kadhaa wameonekana kuhitaji huduma ya Saul.
Nyota hao hawana mpango wa kuondoka katika usajili wa msimu ujao kwa sababu timu ya Atletico Madrid wamefungiwa kusajili hadi mwaka 2018 hivyo hakuna atakayetoka.
Lakini kama Simeone ataondoka wakati wa usajili msimu wa 2018, itakuwa vigumu kuwazuia nyota hao ambao wanasakwa na klabu kubwa Ulaya.
Kitendo hicho huenda kikabadili kila kitu katika klabu hiyo kitu ambacho kitafanya kuporomoka kwa klabu hiyo.
Ni jambo ambalo linaweza kuathiri timu hiyo msimu ujao ingawa haitakuwa kwa nafasi kubwa kutokana na Simeone atakuwa akionekana akirandaranda uwanjani.
Wakati akiondoka itachukua muda kwa timu hiyo kufanya maajabu aliyokuwa ikiyafanya enzi zake.
“Mashabiki watakuwa shwari kama kocha wao ataendelea kuifundisha timu hii,” yalikuwa maneno ya Rais wa klabu hiyo, Enrique Cerezo, msimu uliopita akielezea umuhimu wa kocha huyo.
Mbadala wa kocha huyo shupavu na hodari inaonekana kuwa kaa la moto hasa baada ya kufanikiwa kujenga umoja na ari ya kujiamini kwa mashabiki wa klabu hiyo.
Kabla ya ujio wake, uongozi wa klabu hiyo umedaiwa kubadili zaidi ya makocha 52 katika miaka 25.
“Tunazungumza kama klabu na kila siku ndio sera yetu tangu tuwe hapa kwa kuwa tunafanya uamuzi sahihi kila wakati.
“Mimi ni Mtendaji Mkuu wa klabu hii, tumefanya uamuzi huu na tutamwongezea mkataba pindi utakapoisha,” alisema Cerezo.
Simeone akiwa mbele ya mashabiki wa timu hiyo Ijumaa iliyopita, aliwataka mashabiki hao kutokuwa na wasiwasi kuhusu kuifundisha timu hiyo.
Lakini kocha huyo huenda akatimkia Ulaya ambapo klabu kubwa zimekuwa zikifukuzia saini yake kwa muda mrefu.
“Hakuna sababu ya kuwa na shaka kwa kuwa nikiwa hapa natamani kuendelea kuwapo.
“Mashabiki wananiamini kwani nimekuwa mwaminifu kwao, hata hivyo naongozwa na mapenzi yangu kuhusu klabu hii,” anasema Simeone.
Kocha huyo anasema kwamba, mkataba ni jambo la siri ingawa limebadili kila kitu ndani ya klabu hiyo na kuonekana kuwa la kila mtu.
Kwa sasa kocha huyo ni miongoni mwa makocha wanaolipwa vizuri katika Ligi ya Hispania baada ya kupokea kitita cha pauni milioni sita kwa mwaka.
Hata hivyo, fedha hizo hazina faida kwa klabu hiyo kwani licha ya kumlipa zaidi huenda wakampoteza wakiwa bado wanamhitaji.
Lakini klabu hiyo inaonekana kujiandaa kumpa mkataba wa miaka miwili zaidi baada ya kumaliza wa sasa.
Klabu hiyo itakuwa vitani kuzipiku klabu zinazotaka saini ya kocha huyo ikiwamo PSG inayofundishwa na Unai Emery na Inter Milan, Frank de Boer.
“Ni kocha mzuri kwa klabu yetu hakuna aliyewahi kuwa kama yeye katika historia ya klabu yetu,” alisema Cerezo.
Klabu hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika Ligi Kuu Hispania, La Liga tangu mwaka 2000.
Kwa sasa Atletico Madrid si timu ya ndogo licha ya kupoteza michezo miwili ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Timu hiyo ilikuwa kati ya timu tatu bora duniani katika miaka mitatu iliyopita ikiwa chini ya Simeone.