24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, May 28, 2022

Dhana Yanga, Simba kuua vipaji kutoweka

yngNa SAMUEL SAMUEL

WIMBO maarufu wa ‘kuua vipaji’ uliokuwa ukivuma sana kwenye ngome za Simba na Yanga, sasa unaanza kutoweka kwa kile wanachokifanya klabu maarufu Mitaa ya Kariakoo kwenye usajili wao.

Klabu hizo kwa miaka mingi zimekuwa zikilaumiwa kuua vipaji vya vijana chipukizi au wachezaji wanaowika na timu nyingine lakini pale wanapowasajili hupotea katika soka kabisa.

Lawama zikitupiwa katika suala la kushindwa kuwapa nafasi ya kucheza ili kuendeleza vipaji vyao, ila kwa namna moja au nyingine lawama hizo zilikuwa na mashiko pale usajili ulipokuwa unafanyika bila kuzingatia mahitaji ya benchi la ufundi, huku sehemu kubwa ya usajili ikifanywa na viongozi wasio na taaluma ya ukocha ilimradi kusajili kwa mitazamo mbalimbali.

Usajili ulikuwa ukifanyika pale vigogo hao wa soka nchini walipokuwa wakikimbizana kuwania saini ya mchezaji mmoja kwa dhima nzima ya kubaniana, wakati mwingine ulikuwa ukifanyika kwa wale wachezaji walioweza kuwasumbua sana katika msimu wa ligi, hata kama aina ya mchezaji huyo yupo ndani ya timu husika.

Mtazamo wa mwisho katika usajili huo wa kimagumashi, ulikuwa ukifanyika pale viongozi waroho walipokuwa wakisajili wachezaji wasio na uwezo mkubwa ilimradi tu waweze kupata asilimia kumi (ten percent) ya mauzo kutoka kwa wadhamini kukidhi haja za matumbo yao, hii hufanyika kwa wachezaji wanaotoka nje ya nchi.

Tukitembea na mifano halisi katika usajili wa aina hii ni pale Yanga walipomsajili golikipa wa Kagera Sugar, Benedicto Tinoco, ambaye kwa msimu mzima hakuweza kuichezea timu hiyo, msimu wa 2015/16.

Kwa upande wa Simba ni pale ilipomchukua kwa mkopo, Joseph Kimwaga, kwa makubaliano ya kuendeleza kipaji chake, lakini kinda huyo alijikuta akisugua kwenye benchi na kupotea kabisa kwenye ramani ya soka.

Ipo mifano mingi lukuki inayonogesha wimbo wa Simba na Yanga kuua vipaji vya wachezaji, lakini kuanzia msimu wa 2015/16 hususani msimu huu mpya ulioanza rasmi Agosti 20, klabu hizo pendwa zaidi nchini zimeonesha kuamka katika usingizi huo mzito na kuachana na wimbo huo.

Msimu wa 2015/16, Yanga ilifanya usajili makini na wenye malengo na matunda yake yameonekana, pia Simba imetoa ishara nzuri kwa kukata mzizi huo wenye uozo wa dhambi ya kuua vipaji kwa usajili wapo makini msimu huu mpya wa ligi 2016/17.

Msimu wa 2015/16, Yanga walizinasa saini za wachezaji wazawa kama Deusi Kaseke na Malimi Busungu ukiachilia mbali wale wa kimataifa kama Donald Ngoma na Thabani Kamusoko.

Usajili wa Kaseke na Busungu, ulihesabika kama mwendelezo wa kuwaleta Kariakoo na kuwapotezea mustakabali wao kisoka.

Wachezaji hao walikuwa tegemeo sana kwenye timu zao, lakini Kaseke kwasasa amegeuka lulu kwenye kikosi cha Wanajangwani hao na yeye kutanua wigo wake kisoka nchini, hii ni tofauti na chipukizi wa miaka ya nyuma waliopotea kwenye benchi la timu hiyo, licha ya kuwika na klabu zao za awali.

Yanga msimu huu chini ya kocha Hans Van Pluijm, pia imesajili wazawa chipukizi na tayari benchi la ufundi limeonesha thamani yao kimbinu na kiufundi, hii ikionesha usajili umefanyika kwa kuzingatia mahitaji.

Pacha ya Nadir Haroub na Kelvin Yondani tayari imeanza kuonesha mkono wa buriani kutokana na umri wao, ila ujio wa Vicent Andrew ‘Dante’ na uwepo wa Mtogo, Vicent Bossou, kumeonesha weledi mkubwa katika usajili wa mzawa huyo Dante toka Mtibwa Sugar. Ameonesha uwezo mkubwa Kombe la CAF na pia mechi tatu za awali ligi kuu.

Simba wamezinasa saini za wazawa mbalimbali kama Muzamir Yassin, Shiza Kichuya toka Mtibwa Sugar na Jamal Mnyate toka Mwadui FC.

Kichuya tayari amefunguliwa milango kwenye kikosi cha kwanza cha Wekundu hao wa Msimbazi kutokana na uhodari wake mkubwa kiuchezaji kama kiungo mshambuliaji wa pembeni, lakini pia ni kiungo mchezeshaji mwenye uwezo mkubwa kuwachezesha washambuliaji wa Simba na kupata ushindi.

Justice Majabvi alipoonesha hana nia tena ya kuichezea timu hiyo, Simba ilizichanga vyema karata zake kwa kumnyakua Muzamir toka Mtibwa Sugar, lakini unadhani kaja kuua kipaji chake Simba baada ya kuwika vyema na Mtibwa Sugar? Ondoa mawazo hayo.

Kuondoka kwa Majabvi kuliwafanya Simba kubakiwa na kiungo mkabaji mmoja ambaye ni nahodha Jonas Mkude, ambaye ndiye kiungo mkabaji aliyekamilika mzawa nchini na ndani ya Simba.

Kimbinu na kiufundi kubaki na mchezaji mmoja tu katika nafasi hiyo ambayo ndiyo moyo wa timu ni hatari, Muzamir ana uwezo mkubwa kucheza nafasi hiyo pia kiungo mshambuliaji, hivyo ni usajili wenye tija kimbinu, ni jukumu la mwalimu kuona anawatumiaje wote.

Kwa mtazamo huu, ni dhahiri shahiri sasa klabu hizi zimeanza kuzingatia usajili kimbinu na kiufundi na kuua dhana ya kusajili vijana chipukizi na kuua vipaji vyao, huku wakikumbatia wakongwe ‘mafaza’.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,577FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles