24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Simba yavamia Brazil

Na MOHAMED KASSARA 

-DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba imeendelea kujiimarisha, kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa ,  baada ya jana kutangaza kumsajili kwa mkataba wa miaka miwili, mshambuliaji Mbrazil, Wilker Henrique da Silva.

Silva mwenye umri wa miaka 23, amejiunga na mabingwa hao wa soka Tanzania, akitokea katika klabu Bragantino inayoshiriki Ligi Daraja la Nne nchini Brazil.

Mchezaji huyo, anakuwa mchezaji mpya wa nne kusajiliwa na Simba msimu huu, baada ya kipa Beno Kakolanya kutoka Yanga, beki wa kati, Kennedy Wilson Juma kutoka Singida United na kiungo wa kimataifa wa Sudan, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman.

Simba pia imewaongezea mikataba wachezaji wake wanne ambao ni , John Bocco, Jonas Mkude, Aishi Manula na Erasto Nyoni.

Silva amekuwa mchezaji wa Bragantino tangu mwaka 2015 alipojiunga nayo akitokea Ponte Preta.

Mwaka jana, Silva alikwenda kuichezea kwa mkopo Uniao Barbarense iliyokuwa Daraja la tatu.

Mbrazil huyo ataungana na wakali wengine kama ,John Bocco, Meddy Kagere kuimarisha safu ya ushambulizi ya mabingwa hao.

Hata hivyo,  kuna taarifa kuwa Simba inaendelea kufanya mazungumzo na Mbrazil mwingine, Gerson Fraga Vieira aliyemaliza mkataba na klabu ya ATK ya India.

Vieira ni beki wa kati  ambaye kama usajili wake utafanikiwa anatarajia kuziba pengo la Pascal Wawa ambaye mkataba wake wa kuichezea Simba umemalizika na kuna uwezekano akapewa mkono wa kwaheri.

Katika hatua nyingine, Azam FC imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji, Emmanuel Mvuyekure kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea KMC.
Mvuyekure anayemudu nafasi zote za ushambuliaji, anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na Azam, baada ya idd Selemani ‘Nado’ kusaini miaka miwili akitokea Mbeya City.

Mrundi huyo alimaliza msimu uliopita kwa kupachika mabao 10 na kuisadia timu hiyo kumaliza nafasi ya nne, hivyo kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Mvuyekure ambaye antajwa kuwa ni kipenzi cha kocha mpya wa Azam, Etienne Ndayiragije,kwani walianza kufanya kazi pamoja katika kikosi cha Mbao FC kabla kuhamia wote, KMC msimu uliopita.

Timu hiyo pia imemuongezea mktaba wa mwaka mmoja mshambuliaji wake, Obrey Chirwa ili kuendelea kuitumikia kubaki katika viunga vya Chamazi.

Hivi karibuni, Azam ilitangaza kuachana na Mzambia huyo aliyefunga bao muhimu lililoipa timu hiyo ubingwa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Lipuli FC na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles