SIJAMWELEWA MWIGULU NCHEMBA

0
633

NA LEAH MWAINYEKULE,

WENGI tulimsikia Rais Dk. John Magufuli akizungumzia suala la wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito.  Wengi tulimsikia akisema kwamba atakayepata ujauzito hataruhusiwa kurudi shule baada ya kujifungua.

Wengi tulimsikia akiwashangaa watu na NGOs zinazotetea wanafunzi hao wa kike kurudi shule, huku akisema kwamba wanaweza kutafutiwa masomo mengine, kama vile kupelekwa kwenye masomo ya ufundi.

Tangu kauli hiyo ya Rais itoke, mijadala imekuwa mingi.  Wengi wakipingana naye kabisa na wachache wakimuunga mkono kwa sababu wanazozijua wenyewe.  Kiujumla, mjadala umekuwa mkubwa kama ilivyotarajiwa na hakuna la kushangaza kabisa kutokana na hilo.

Kilichoshangaza, hata hivyo ni kauli aliyoitoa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, akionya taasisi zinazojadili kauli ya Rais.

Mwigulu amenukuliwa akisema kwamba taasisi zisizo za Serikali zinazohamasisha kudai haki ya mtoto anayepata mimba kurejeshwa shuleni kuacha mara moja na zikiendelea atazifutia usajili.

Hivi, tangu lini Katiba ya nchi yetu ilitoa maelekezo kwamba kauli ya Rais haitakiwi kujadiliwa?  Wapi na lini ilitungwa sheria ya kueleza kwamba yeyote atakayejadili na kupingana na kauli ya Rais anatakiwa kupewa onyo kali?

Pengine nijitolee kumkumbusha Mwigulu kwamba Katiba ya nchi yetu inatoa uhuru wa maoni.  Watu wana haki ya kuzungumza na kutoa maoni yao kupitia njia yoyote pasipo kuvunja sheria na hakuna sheria yoyote inayokuwa imevunjwa kwa kujadili kauli ya Rais.

Actually, kauli yoyote ya Rais inatakiwa kujadiliwa na mtu yeyote yule, iwe mtu binafsi ama taasisi, kwani chochote kinachotamkwa na Rais kinaathiri nchi nzima.

Labda tu nimkumbushe Mwigulu sababu ya watu kujadili kauli ya Rais…na akumbuke kwamba si taasisi zisizo za Serikali tu zinazojadili suala hili, bali idadi kubwa ya watu, wengi wao wakiwa wazazi wenye watoto wa kiume na watoto wa kike.

Watu wanajadili kauli ya Rais kutokana na ukweli kwamba kibaolojia na kitamaduni, tayari mtoto wa kike anakuwa anabanwa na mambo mengi sana yanayosababisha asipate ‘mteremko’ katika elimu yake na maisha kiujumla…huenda kutokana na yeye kuwa mtoto wa kiume, basi Mwigulu anaweza asilielewe hilo, japo wapo wanaume wengi sana, tena wasio katia taasisi zisizo za Serikali, wanaoelewa hilo.

Wapo wanaoelewa kwamba suala la mtoto wa kike kupata ujauzito akiwa shule ni kubwa na haliwezi kuisha kwa kupiga tu marufuku binti huyo kurejea shule baada ya kujifungua.

Wapo wanaotambua kwamba wapo mabinti wanaojihusisha na ngono kwa kupenda, kutokana na mabadiliko ya mwili yanayosababisha tamaa na wapo pia wanaopata kwa kutopenda.

Wapo wanaotambua kwamba kuna mabinti wanaoishi katika mazingira hatarishi sana.  wanaondoka nyumbani bila kula, wanatembea umbali mrefu au wanakuwa hawana hata nauli, wanarubuniwa na kujikuta wakishindwa kuepuka hivyo vishawishi.  Wanaingia kwenye mahusiano wakidhani wanapendwa, kumbe wanadanganywa.

Wapo pia wanaotambua kwamba kuna wanaume wengine, tena watu wazima wenye maisha yao, wanaopenda kurubuni mabinti wa shule.  Wanaweza kujaribu kuwarubuni na ama kufanikiwa au kutofanikiwa na wanaweza hata kuamua kuwabaka.  Yametokea na yanaendelea kutokea.

Sina hakika kama Mwigulu anayaelewa haya yote au kama ameamua tu kuzungumza hadharani kutokana na ukweli kwamba yeye ni Waziri na analazimika kukubaliana na chochote kinachotamkwa na Rais wake.  Kama kweli anayaamini aliyoyasema na atayatekeleza aliyoyatishia, basi kama nchi tuna kazi kubwa sana.

Tuna kazi kubwa sana kwa sababu Waziri wa Mambo ya Ndani anapoamua kupeleka nguvu zake katika kuwadhibiti wanaoipinga kauli ya Rais, badala ya kupeleka nguvu hizo katika kuwakamata wahalifu wanaowarubuni watoto hawa na kutaka kuwaharibia maisha yao, basi kweli bado safari ya kumkomboa mtoto wa kike ni ndefu sana.

Kama Waziri wa Mambo ya Ndani anadhani mtu ama taasisi inayotetea mtoto wa kike kupata elimu anavunja sheria, basi naishiwa kabisa maneno ya kusema.

Tangu lini kutetea binti kupata elimu ikawa ni uhalifu? Na kufikiria hili linatoka kwa Waziri…sijamwelewa kabisa Mwigulu!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here