TAASISI YA ‘UCHUNGAJI’ YADAIWA KUTAPELI MIL. 120/-

0
655

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA

TAASISI ya Uchungaji ya Tanzania Pastors Saccos Limited ya  Dar es Salaam inatuhumiwa kuwatapeli wananchi zaidi ya 50 wa mkoani Arusha   Sh milioni 120.

Fedha hizo zilidaiwa kutolewa na watu hao kama amana, kabla ya hawajanufaika na mikopo kupitia Taasisi hiyo ya Kuweka na Kukopa (SACCOS) iliyoingia mkoani hapa kushawishi wananchi kujiunga kupitia uaminifu wa Pastors Saccos.

Akizungumza mjini hapa jana kwa niaba ya wenzake kuhusu utapeli huo, Mchungaji Peter Kitilla alisema  wamemuandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Arusha wakimuomba msaada wa kurejeshewa fedha zao.

Mchungaji Kitilla alisema  kupitia barua yao ya Juni 6, mwaka huu,  walalamikaji  zaidi ya 50 wameomba mkuu wa mkoa awasaidie kuwabana watuhumiwa baada ya juhudi walizofanya wao kushindikana.

“Tumejaribu kufanya kila njia lakini tumekwama kurejeshewa fedha zetu mpaka hivi sasa.  Kwa sababu  tumefuatilia mpaka kwa waliokuwa viongozi wa taasisi hiyo vikiwamo vyombo vya dola,” alisema Mchungaji Kitilla.

Akielezea mahali taasisi hiyo ilikoanzia shughuli zake mkoani hapa, alisema ilianzia katika maeneo ya Kata ya Unga Limited,  Mianzini  Arusha kisha ikafungua matawi meneo ya Tengeru na Kikatiti wilayani Arumeru.

Alisema katika maeneo hayo viongozi wa Pastors Sacco’s waliokuwa wakiwachangisha fedha wananchi wanachama wapya kwa kuwatoza fedha za kiingilio, akiba ikiwamo kununua hisa.

“Tuliojiunga tuliamini na kusadiki SACCOs hii imeundwa na watumishi wa Mungu kutokana na jina wanalotumia. Lakini pia malengo ya kuweka akiba, kutoa mikopo na kuweka utaratibu wa urejeshaji,” alisema Kitilla.

Mchungaji Kitilla alimtaja mwakilishi wa Pastors Saccos anayedaiwa kutapeli kuwa ni Paulo Daniel ambaye baada ya kujikusanyia   Sh milioni 120 kutoka kwa wanachama wapya aliondoka mjini Arusha bila taarifa yeyote.

Mwananchi mwingine aliyetapeliwa Lucas Kitomary, alisema viongozi wa Pastors Saccos walioko Dar es Salaam baada ya kupatikana walifika mjini Arusha na kuahidi kulipa fedha hizo Februari mwaka huu.

Kitomary alidai mpaka wanaandika barua yao kwenda kwa mkuu wa mkoa bado viongozi hao walikuwa hawajatimiza ahadi yao ya kuwarudishia fedha walizotapeliwa.

Naye Mtendaji Mkuu wa Tanzania Pastors Saccos Limited, Nathaniel Mwaluko akijibu madai ya wananchi hao, alidai  taasisi yake imekuwa ikiendesha shughuli zake kwa weledi mkubwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here