JPM KUFUNGUA MAONYESHO YA SABASABA

0
727

Na CHRISTINA  GAULUHANGA – DAR ES SALAAM

RAIS Dk.John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonyesho ya 41 ya Biashara Kimataifa ya Sabasaba ambayo yanatarajiwa kuanza leo.

Akizungumza   Dar es Salaam jana, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema Rais Magufuli atafungua maonyesho hayo Julai Mosi mwaka huu.

Alisema suala la ulinzi na usalama limeimarishwa katika viwanja hivyo.

“Tumejipanga kuhakikisha maonyesho haya yanakuwa ya aina ambayo kamera zimeongezwa pamoja na vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama ambavyo vitaongoza kamera hizo,”  alisema Mwijage.

Alisema kaulimbiu ya maonyesho hayo   mwaka huu ni ‘ukuzaji biashara kwa maendeleo ya viwanda’.

“Ukiwa na viwanda bidhaa unazozalisha  zisiweze kuuzwa biashara itakufa,” alisema Mwijage.

Mbali na hilo  Julai 6 mwaka huu itakuwa siku maalumu ya wafanyabiashara wa nchi za Afrika Mashariki.

Alisema katika maonyesho ya mwaka huu   nchi 30 zitashiriki   na   kutakuwa na mabanda maalumu yatakayoonyesha bidhaa za Afrika   na kuwapo mabanda maalum likiwamo la asali  na ngozi.

Alizitaja baadhi ya nchi zitakazoshiriki kuwa ni pamoja na Burundi  China, DRC, Ujerumani, India, Japan na Malawi, Rwanda, Afrika Kusini, Uturuki, Marekani, Uingereza na Vietnam.

Alisema viingilio  vya mwaka huu katika maonyesho hayo ni Sh1,000 kwa watoto  na wakubwa  ni Sh 3,000 na siku ya kilele Julai 7 kwa wakubwa kiingilio kitakuwa Sh 4,000.

Hata hivyo alisisitiza washiriki wa maonyesho hayo kuhakikisha wanakua na risiti za bidhaa wanazouza.

Aliwasihi  wananchi watakaonunua bidhaa katika maonyesho hayo kudai risiti   kuondokana.na.usumbufu unaoweza kujitokeza kutoka kwa walinzi na wakaguzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), watakaokuwapo milangoni katika viwanja hivyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here