23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

CHENGA, MIZENGWE NA SARAKASI UBUNGE AFRIKA MASHARIKI

Na DEUS KIBAMBA,

NIMEFUATILIA michakato ya uchaguzi wa Wabunge kwenda katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa hisia mchanganyiko. Kama wasemavyo mtaani, nimetakafakari sana kuhusu yanayoendelea katika nchi zote wanachama wa Afrika Mashariki kiasi cha kujiuliza demokrasia hiyo inakuwaje?

Mbona hakuna mfumo mmoja wa kuwapata wabunge tisa ambako kila nchi inapasa kuwachagua ili kutimiza idadi ya Wabunge 54 wanaounda Bunge la mtangamano wa Afrika Mashariki.

Mbona Uganda wanafanya kivyao, Tanzania kivyao, Kenya kivyao, Sudan Kusini na Burundi na Rwanda kivyao? Hatuwezi kuwa na utaratibu wa usimamizi, uratibu na uangalizi ili kuhakikisha kuwa utaratibu unaotumika kuwapata wajumbe wa EALA ni mmoja ili kupunguza mivutano isiyo ya lazima pamoja na mizengwe, mivutano, ghilba, chenga na sarakasi katika kuwapata wabunge hao mithili ya kinachoendelea hivi sasa katika ukanda huu?

Wakati Bunge la Tatu la Afrika Mashariki likiwa limemaliza muda wake wa miaka mitano, Bunge la Nne limeshindwa kuanza rasmi kutokana na upungufu mkubwa katika utaratibu wa kuwapata wabunge wake kutoka nchi za Kenya na Sudan ya Kusini kiasi cha kutuhumiana na kushitakiana.

Ikiwa ni mara ya kwanza kuleta wabunge wake katika EALA, Sudan ya Kusini ambayo mji mkuu wake ni Juba ndiye imeongoza kwa kukosea utaratibu wa uchaguzi wa wabunge wake.

Badala ya kuandaa utaratibu wa Bunge la Sudan Kusini kuwachagua wabunge wake kutoka nje ya Bunge kama ilivyo matakwa ya ibara ya 50 ya mkataba unaoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir aliamua kwenda kinyume na kuchukua mkato wa kuteua wabunge wote tisa (9) watakaowakilisha Sudan ya Kusini katika Bunge hilo.

Kutokana na hilo, makada wafuatao wa chama tawala cha SPLM walipata nafasi hiyo: Dk. Anne Itto, Dk. Gabriel Garang Aher, Gai Deng Nhial, Ukel Ubango, Isaac Aziz Justin, Gabriel Alaak, Adil Elais Sandrai, Thomes Dut Gatkek na Gideon Gatpan Thoar.

Baada ya hapo, Bunge la mpito la nchi hiyo liliwathibitisha wabunge hao Machi mwaka huu, kuiwakilisha nchi hiyo changa kuliko zote duniani katika Bunge la  EALA.

Endapo wangekubalika, wabunge hao wangetumikia Bunge la  EALA kwa kipindi chote cha miaka mitano huku wakiwa na haki ya kuomba tena ridhaa ya kuiwakilisha nchi yao kwa miaka mingine isiyozidi mitano.

Swali moja la kujiuliza ni Je, hakuna aliyepata kusoma na kufahamu kanuni na taratibu za uchaguzi wa wabunge hao?

Mbali na kukiukwa kwa utaratibu wa wabunge wa EALA kuchaguliwa na Bunge la nchi husika, uteuzi wa Rais Kiir umekiuka msingi mwingine muhimu wa uwiano wa kijinsia.

Kwa mujibu wa taratibu za EALA, uchaguzi wa wabunge wa EALA lazima ufuate utaratibu ambapo angalau theluthi moja ya wabunge wanaochaguliwa watakuwa ni wanawake.

Hii inamaanisha kuwa katika wabunge tisa, angalau asilimia 33 yao lazima wawe wanawake. Kwa ukokotozi wangu wa haraka, nchi lazima ihakikishe kuwa angalau wabunge wanne katika tisa ni wanawake.

Sasa iweje Sudan ya Kusini imepeleka Arusha wabunge wanawake wawili pekee huku wote saba waliosalia wakiwa wanaume? Hivi washauri wa Rais  wa Sudan Kusini hawakumshauri chochote kuhusu msingi huu wa uwiano wa kijinsia?

Aidha, msingi mwingine wa kuhakikisha uwakilishi mpana wa vyama vya siasa vilivyoko katika Bunge la Taifa husika sambamba na uwakilishi wa makundi mahususi na maalumu kama vile watu wenye ulemavu, Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, vijana, makundi ya wazalishaji wadogo wadogo umezingatiwa?

Nionavyo, hilo nalo limekiukwa. Ni kwa msingi huo raia mwema wa nchi hiyo, Wani Santino Jada alifungua kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), kupinga kutambuliwa na kuapishwa kwa wabunge hao wateule kutoka Juba akilalamikia ukiukwaji huo mkubwa wa taratibu za kuwapata wabunge hao.

Katika uamuzi wake, Jopo la majaji wa EACJ lilikubaliana na mlalamikaji na kuweka zuio kwa wabunge hao kutambulika na kuapishwa kuwa wabunge wa Bunge la Nne la Afrika Mashariki.

Kutokana na hilo, nchi ya Sudan imejiunga na Kenya katika kuwa ya mwisho kuwapata wabunge wake kutokana na mivutano inayoendelea ndani ya nchi zao kuhusu utaratibu wa kuwapata wawakilishi wao katika Bunge hilo la kikanda.

Tayari Bunge la Sudan Kusini limeridhia hoja ya kutengua uteuzi huo wa wabunge wa Sudan Kusini katika Bunge la EALA iliyoletwa bungeni na Spika wa Bunge la nchi hiyo, Antony Lino Makama.

Badala yake, Kamati ya watu sita imeundwa ili kufanya juhudi za kutafuta elimu juu ya kanuni na taratibu za uchaguzi wa wabunge wa EALA na kuileta kwa wabunge wa Bunge la Sudan Kusini.

Kwa maoni yangu, kazi kama hiyo ilipaswa kufanywa mapema na taasisi makini zenye utaalamu huo kama Chuo cha Diplomasia kilichopo Dar es Salaam, Tanzania. Itafaa sana kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuanza kutumia utaalamu wa masuala ya diplomasia, demokrasia na uchaguzi kama ule ulio katika chuo hicho, kinachomilikiwa na kuendeshwa kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Serikali ya Msumbiji.

Ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi CFR nacho kitapaswa kuongeza kasi ya usambazaji wa majarida na vipeperushi kujitangaza kwa elimu na kozi zinazotolewa katika chuo hicho kikongwe kinachotoa elimu ya juu kwa wapigania uhuru wa Bara la Afrika tangu mwaka 1978 kikiwa na hazina kubwa ya mabalozi, wakufunzi, wahadhiri na wawezeshaji wa masuala ya mtangamano, demokrasia ya Katiba, Haki za Binadamu, Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia.

Wakati hayo yakitokea Sudan Kusini, Kenya nayo haikuwa na nafuu. Katika hali ya kushangaza, uchaguzi wa wabunge watakaoiwakilisha Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki ulikumbwa na mizengwe na sarakasi kiasi cha kuchelewa kukamilika hadi mwishoni mwa Juni, 2017.

Wakati fulani, uteuzi wa watoto wa vigogo wa Muungano wa CORD, ambao kwa mgawanyo wana nafasi nne ulibezwa na viongozi wa Jubilee kuwa ni ishara ya ukabila, rushwa na upendeleo, kinyume cha misingi ya Katiba Mpya ya Kenya ya mwaka 2010.

Kwa mfano, ingawa viongozi wa Chama WIPER walitetea uteuzi wa mtoto wa mwanasiasa Kalonzo Musyoka kuwa ulifuata sifa, uwezo na vigezo vya kazi hiyo, Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto alisikika akikemea kuwa uteuzi huo ni dalili ya ukabila, upendeleo na rushwa ya madaraka kwa watoto na ndugu wa viongozi wa Muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya.

Kwa upande mwingine, muungano wa vyama tawala wa Jubilee, ambao unastahili kupata wabunge watano kwenda EALA ulikuwa na wepesi wa kupeleka majina lakini ambayo yalilalamikiwa kwa sababu kadhaa ikiwamo kutokuwa na majina ya kutosha ya wanawake na uwakilishi wa makundi mengine.

Pamoja na kukiuka msingi wa kutochagua wabunge ambao wako katika Bunge la nchi husika kama inavyokatazwa na ibara ya 50 (1) ya Mkataba unaoanzisha Jumuiya ya EAC wa mwaka 1999. Kinyume chake na kwa sababu anazozijua mwenyewe, Spika wa Bunge la Kenya, Justin Muturi alitoa ufafanuzi wa upotoshaji kuwa hakukuwa na ulazima kwa mbunge kujiuzulu katika utumishi wa Bunge la nchi yake ndipo agombee nafasi ya ubunge wa EALA jambo ambalo linapingana na matakwa ya Mkataba wa EAC.

Hii ilikuwa ni katika kutetea na kupendelea wabunge wanaogombea ubunge wa EAC huku wakiwa bado ni wabunge wa Bunge la Kenya kama Mbunge wa Mandera Kaskazini Mohammed Nooru ambaye pia ni rafiki wa karibu wa Spika Muturi.

Inavyoonekana, Spika Muturi yuko tayari kuvunja matakwa ya Mkataba wa EAC ili kumpatia rafikiye ulaji wa Dola za Marekani 14,000 ambazo mbunge wa EALA hujipatia kama jumla ya mshahara na stahiki nyingine kila mwezi kwa miaka yote ya utumishi wake katika Bunge la Afrika Mashariki.

Kwa ujumla, kumekuwa na zaidi ya waombaji 41 wa nafasi ya ubunge wa EAC katika Kenya huku Muungano wa Jubilee ukipendekeza watu 15 kujaza nafasi 5 walizonazo kikanuni.

Kwa upande wao, Muungano wa CORD unaamua kupeleka majina manne tu, likiwamo lile la kijana Kennedy Kalonzo Musyoka kutoka WIPER ili kukwepa mizengwe kama ile iliyotokea katika uchaguzi kama huo nchini Tanzania.

Mizengwe, sarakasi na chenga katika nchi nyingine za Afrika Mashariki zitaendelea kujadiliwa katika safu hii ya makala katika wiki zijazo. Fuatilia!

Deus M Kibamba ni Mtafiti, Mhadhiri na Mshauri wa Masuala ya Demokrasia ya Katiba, Siasa na uhusiano wa Kimataifa. Amekuwa mwangalizi wa Kimataifa katika Michakato ya uchaguzi, Maridhiano na mazungumzo ya kitaifa katika nchi kadhaa za kiafrika. Kwa sasa, Kibamba anafuatilia mchakato wa Mazungumzo ya Kitaifa Katika Nchi ya Sudan ulioanza mwaka 2013.Anapatikana kwa simu: +255 788 758581; email: [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles