28.6 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

SHIFTA APANGA KUVUNJA REKODI YA KANUMBA

Na JOHANES RESPICHIUS


MWONEKANO wa sura yake umekuwa ukifananishwa na staa wa filamu za kitanzania marehemu Steven Kanumba, huyu ni Ahmed Shifta ‘Shifta’, msanii anayekuja kwa kasi kwenye tasnia hiyo.

Jina lake limepata umaarufu punde alipoonekana kwenye msimu wa pili wa tamthilia ya Siri za Familia inayoruka kupitia kituo cha EATV. Huku uwezo wake wa kuuvaa uhusika kwenye filamu kali kama The Date Some One na Safari ya Gwalu ya msanii Gabo umepandisha chati.

Ndani ya Chombezo Tata wiki hii tupo na Shifta kwa lengo moja la kukujuza mengi ambayo huwenda huyafahamu kuhusu yeye, karibu.

HISTORIA YAKE

Shifta ni mzaliwa wa Igawa, Mbalali mkoani Mbeya, alipotimiza umri wa mwaka mmoja familia yake ilihamia jijini Dar es salaam hadi pale umri wa kwenda shule ulipofika, Shifta alikwenda Kenya kwa ajili ya masomo na baadae akarejea nchini.

 “Nilikuwa na ndoto ya kuwa mwanasheria lakini baadaye ikapotea nikajikuta napenda utangazaji, nilikwenda chuo kusoma Uandishi wa Habari na nilipomaliza nilifanikiwa kupata kazi kwenye redio kadhaa huko Mbeya pamoja na E FM ya Dar es salaam na baadae nikaamua kujiingiza kwenye ulimwengu wa filamu,” anasema Shifta.

JEMBE HALIMTUPI MKULIMA

Anasema mbali na sanaa yeye ni mkulima wa vitunguu licha ya vijana wengi hasa wasanii kukimbia kilimo kwa madai kuwa  hawastahili kufanya kazi hiyo.

 “Ukiamini kwamba umeweka fedha sehemu sahihi haiwezi kupotea lakini ukiipeleka kusiko mwisho wa siku utakuta zinapotea bila kujua, nina uhakika jembe halimtupi mkulima, mtaji  hauwezi kupotea ukiupeleka kwenye kilimo,” anasema Shifta.

ANAIBUA VIPAJI VIPYA?

Shifta anadai yeye ni balozi wa wasanii wachanga kutoka jijini Mbeya na amekuwa akitumika kama daraja la kupitisha vipaji vipya kutoka Nyanda za Juu Kusini kupitia filamu zake.

 “Lengo la kufanya kazi na wasanii wachanga ni kutaka kila mwenye kipaji aonekane na jamii ndiyo maana kuna filamu na tamthilia mbili mpya zimejaa wasanii wachanga wataonekana zitakapoanza kuruka kupitia DSTV,” anasema.

KUFANANISHWA NA KANUMBA

Anasema anajivunia kufananishwa na Kanumba lakini hali hiyo haimfanyi aige kila kitu ambacho alikuwa anakifanya Steven Kanumba.

 “Najivunia kwasababu ni mtu aliyefanya mambo makubwa kwenye sanaa ya Bongo, nitabaki kuwa Shifta na siyo Kanumba lakini nitaenzi juhudi zake za kuitanganza Tanzania kwa kufanya kazi na wasanii wakubwa kutoka Nigeria na Ghana, rekodi ambayo mpaka leo hakuna msanii mwingine aliyeivunja,” anasema.

ASICHOKISAHAU

Shifta anasema imani yake ya kuamini kile anachodhani ni sawa imefanya apate mafanikio kwenye mambo ambayo wenzake wanaona haiwezekani.

 “Kuna siku tulisafiri kwenda Zambia tukiwa na nauli ya kwenda tu, tulipofika tukawa hatuna fedha na mwenyeji wetu bado hatujamuona lakini niliwapa moyo wasanii wenzangu na walishangaa kwani tulifanikiwa kumwona na tukarudi bila tatizo, hakuna msanii ambaye unaweza kumwambia asafiri bila kumpa nauli ya kurudia,” anasema Shifta.

 “Niliwahi kufikiria kuyaweka rehani maisha yangu kwa kuhamia nchi za nje ili nikifanya kazi nzuri watanzania wajivunie kuwa na mtu kama mimi,” aliongezea Shifta.

AWAWEKA TAYARI MASHABIKI

Anasema baada ya ‘The Date Some One’ anatarajia kuachia filamu mbili mpya Lucifer na Alfoncio, ambazo amedhamiria kuzisambaza yeye mwenyewe.

“Filamu ya kwanza nilimpa msambazaji ambapo niliuza mpaka Hakimiliki yangu jambo linaloniumiza sana ila hizi zinazofuata ni bora nisambaze mwenyewe hata kama nitapata kidogo nitaridhika kwa sababu naweza kuifanyia chochote tofauti na ukiiuza kwa Mhindi,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles