30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

TAUSI LIKOKOLA MWANAMITINDO ALIYEKAMATA FURSA NDANI NA NJE YA BONGO

Na AGATHA CHARLES


UNAPO wazungumzia wanamitindo ambao wameyajenga majina yao kuanzia ngazi ya Taifa mpaka ile ya kimataiafa basi huwezi kulikosa jina la mlimbwende wa zamani Tausi Likokola.

Mwanamitindo huyu mkongwe ni kielelezo cha nembo ya urembo hapa Bongo kutokana na jinsi alivyoweza kujenga jina, heshima na mwonekano wake mpaka leo hii akiwa kama mama wa watoto wawili.

Zaidi ya miaka 20 sasa, Tausi ameendelea kujizolea heshima kwenye tasnia ya urembo huku akilinda na kuthamini kipaji alichonacho ambacho kwa sasa ameamua kugawana na warembo wachanga kupitia kipindi chake cha runinga.

Nikiwa kama mmoja ya watu waliohudhuria kwenye onyesho la Lady In Red lililofanyika juma moja lililopita katika ukumbi wa King Solomon, Namanga jijini Dar es salaam, likiwa limeandaliwa na mama wa fasheni, Asya Idarous, nilipata wasaa wa kuzungumza naye mambo kadha wa kadha.

Tausi ambaye anaishi hapa Tanzania na Marekani alikuwa ni mmoja ya wadhamini wa onyesho hili la mavazi lililowakutanisha wadau wa mitindo, warembo na wabunifu wakongwe na wapya.

MJASILIAMALI MAKINI

Ndani ya onyesho hili Tausi alikuwa na mwonekano mzuri wa kimitindo kuanzia viatu, mavazi, utembeaji mpaka uongeaji na Swaggaz lilipomfikia alianza kufunguka kuhusu bidhaa yake ya nywele.

Anasema ‘Tausi Beautiful You Hair’ ni nywele halisi (Human hair) ambazo alianza kuzitengeneza huko Las Vergas, Marekani na hivi sasa zinatengenezwa nchini China.

“Nilipokuwa naji-brand nikaona ningependa vitu ambavyo navitumia na kuvipenda nivipeleke kwa wengine, kwa ujumla nalenga kwenye ubora wa nywele halisi na tayari nimezisambaza kwenye maduka mbalimbali (SPAs) na baadhi ya sehemu nilizozichagua,” anasema Tausi.

UBORA WAKE VIPI?

Imezoeleka nywele bandia hutumika na kutupwa pale zinapochakaa lakini kwa bidhaa hii ya Tausi hali ni tofauti kabisa.

 “Hii nywele unanunua unakaa nayo miaka, unaweza ukaifanya unavyotaka mfano kuziweka rangi, kuzikata au kuziweka mawimbi kama nywele halisi,” anasema Tausi.

ANAMILIKI MANUKATO

Ujasiliamali wake haujaishia kwenye nywele pekee, Tausi amejiongeza hivi sasa anamiliki manukato ambayo yametengenezwa kwa malighafi anazozipenda yeye mwenyewe.

“Nina pafyumu, sipendi ile ya  kunukia yenye marashi makali, mpaka sasa nimetoa aina moja ambayo ni Tausi Dreams yenye mafuta yanayosaidia manukato hayo kudumu muda mrefu,” anasema Tausi.

Anasema ndani ya ujasiliamali huo hivi sasa anatimiza miaka miwili huku akiwa mwandishi wa vitabu vinavyoitwa, The African Princess na The Touch Of An Angel.

SOKONI HALI VIPI?

Tausi anasema soko bado ni gumu kwani watu wengi wapo tayari kununua bidhaa za bei rahisi zisizo na ubora na wakaacha kununua bidhaa bora kwa kuogopa ghalama hivyo amejikuta akiuza manukato yake polepole.

“Kwa upande wa nywele sikutengeneza kwa ajili ya watu wengi, wanakuja lakini hawajawa wengi kiasi niseme bidhaa yangu imetoka kwa wingi,” anasema Tausi.

NYUMA YA KIPINDI CHA RUNINGA

“Wakati mimi nakua nilikuwa na maswali mengi sana ambayo yalihitaji dada ayajibu na siyo mama, maswali mengi yalikuja nilipowaona wasichana wengine wana maswali kama yangu na wakawa wana niomba niwasaidie kwenye mitindo kwa hiyo nikaona nianzishe kipindi cha runinga ambacho kitajibu maswali ya wasichana wengi,” anasema Tausi.

Kipindi chake kinaitwa Tausi Likokola’s African Princess Model Search na kinaruka kupitia kituo cha TV I  ambacho kina maudhui mengi aliyoyaandika kwenye vitabu vyake vya Beautiful You na African Princess ambavyo ndani yake kuna uhalisia wa masuala ya mitindo, uongozi, kujiamini na kujituma.

 “Ukiangalia kipindi changu siyo tu mwanamitindo bali msichana yeyote anaweza kujifunza jinsi ya kutengeneza ngozi yake au namna ya kujikwamua kimaendeleo,” anasema Tausi.

Msimu wa kwanza wa kipindi hicho ulifanyika kwa mafanikio makubwa kwani walipata mrejesho wa kutosha kutoka kwa jamii na hivi sasa wapo mbioni kurudi na msimu wa pili wa kipindi hicho.

Ikumbukwe kuwa mrembo huyu amewahi kufanya kazi chini ya kampuni za kimataifa kama Gucci, Christian Dior, Issey Miyake, Tommy Hilfger na Escada huku akimiliki kampuni zake mbili za Tausi and Friends for Life na Tausi Dreams Ltd.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles