24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Shahidi: Sikuona wafuasi wa Chadema wakishambulia polisi

KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

SHAHIDI wa sita wa Jamhuri, Koplo Charles, amedai wakati anachukua picha za video hakuona wafuasi wa Chadema wakishambulia polisi kwa mawe wala walipohutubia hakuna aliyekuwa kashika, fimbo, mawe na marungu.

Amedai alipokuwa jukwaani Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alizungumza kwamba hawataki fujo, hawatafanya fujo na hawataua hata nzi, lakini kuna maneno mengine aliyaona yanashawishi wananchi kuichukia Serikali.

Shahidi huyo alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati akihojiwa na Wakili Peter Kibatala. Alijibu baadhi ya maswali na mengine alidai hakumbuki hadi video iangaliwe tena.

Mahojiano kati ya shahidi huyo na Kibatala yalikuwa kama ifuatavyo:

Swali: Mbowe katika ile video anaonekana akisema Magufuli ni nani… shahidi kwani ni kosa la jinai kuuliza hivyo?

Jibu: Sifahamu hilo, mimi sio mpelelezi.

Swali: Mbowe aliposema Magufuli mwepesi kama karatasi tatizo liko wapi?

Jibu: Inategemea maneno hayo unayatoa kwenye muhtadha gani.

Swali: Kweli au si kweli, Katibu wa Chadema Hananasif aliuawa?

Jibu: Sifahamu.

Swali: Mbowe alisema yuko tayari kwa mapambano ya kudai haki, unafahamu angepambana vipi?

Jibu: Sifahamu.

Swali: Ni sahihi Mbowe alisema hatutaki fujo, hatufanyi fujo na hatuuwi hata nzi?

Jibu: Ni sahihi alisema Mbowe kuwaambia wananchi.

Swali: Unakumbuka uliwapa video wapelelezi wakawaonyesha washtakiwa wakati wanawahoji?

Jibu: Sijawahi kuwapa video.

Swali: Kielelezo kinaonyesha hatua ya maandamano au hakionyeshi?

Jibu: Kinaonyesha.

Swali: Picha yako ya video uliishia wapi kuchukua maandamano?

Jibu: Niliishia maeneo ya Mkwajuni.

Swali: Katika video kuna mtu anaonekana kashika silaha kama fimbo, visu, panga na marungu?

Jibu: Sikuona kama kuna watu waliokuwa wakihutubia jukwaani walishika visu, virungu, panga na mawe.

Swali: Video ilionyesha wafuasi wa Chadema wakiwashambulia polisi?

Jibu: Sijaona chochote.

Swali: Salum Mwalimu alisema maneno gani ya kuvunja sheria?

Jibu: Alisema kama litatokea lolote fuatilieni familia za askari.

Swali: Kumuombea dua mbaya aliyekudhulumu ni kosa la jinai?

Jibu: Kimya.

Swali: Ni kosa la jinai kumuomba Mungu amuue aliyedhulumu?

Jibu: Ni kosa la kutishia kuua kwa maneno.

Swali: Katika hati ya mashtaka hilo shtaka lipo?

Jibu: Halipo.

Shahidi alidai hakumbuki Esther Matiko, John Mnyika, Dk. Vicent Mashinji walisema nini, lakini anakumbuka Halima Mdee alisema kesho watawachinja Magufuli na vibaraka wake.

Swali: Kuichukia Serikali ni kosa?

Jibu: Sio mpelelezi wa kesi mimi

Swali: People’s Power ni nini maana yake?

Jibu: Sifahamu.

Mahakama ilihamia tena katika ukumbi wa mafunzo wa mahakama kuangalia video kwa mara nyingine.

KESI YA MSINGI

Katika kesi ya msingi, Mbowe na wenzake wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani, kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, Bulaya alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Ilidaiwa Februari 16, mwaka huu barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni, Wilaya ya Kinondoni kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa Jeshi la Polisi, Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili; Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Ilidaiwa siku ya tukio la kwanza na la pili, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, katika mkutano wa hadhara, mshtakiwa Heche alitoa lugha ya kuchochea chuki akitamka maneno; “Kesho patachimbika upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii… wizi unaofanywa na Serikali ya awamu ya tano… watu wanapotea… watu wanauawa wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome… “.

Imedaiwa kuwa maneno hayo yalielekea kuleta chuki kati ya Serikali na Watanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles